SERIKALI KUENDELEA KUTEKELEZA MKAKATI WA KUKABILIANA NA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

Na Saidi Lufune, Dodoma
SERIKALI imeweka vikosi vya kudumu vya Askari katika Kata za Bwiti na Mwakijembe kwa lengo la kuwawezesha askari Wanyamapori kuwahi mwitikio haraka katika matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu wanapovamia maeneo ya wananchi.
Hayo yamesemwa na Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb.), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Twaha Said Mwakioja (Mb.) aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti Tembo wanaojeruhi na kuharibu mali majumbani na mashambani.
Amesema kuwa hatua hiyo ni mkakati wa kitaifa unaotekelezwa na Serikali katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu sambamba na kutumia teknolojia za kisasa hasa visukuma mawimbi (GPS collars); ndege nyuki (Drones) pamoja na mabomu baridi katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo katika Wilaya ya Mkinga.
Halikadhalika wakati akijibu swali la Mhe. Edibily Kazala Kinyoma (Mb.) aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia Wananchi wa Kitongoji cha Katoto waliopisha Mradi wa Kitalu cha Makere Forest Reserve, Mhe. Chande amesema tayari Serikali imefanya tathmini ya kaya na makazi kwa wananchi wa kitongoji cha Katoto na kugawa eneo la ukubwa wa Hekta 4,446 katika kitongoji cha Nyantuku kijiji cha Kagerankanda ambapo kila kaya ilipewa eneo la kujenga la ukubwa wa mita 32 kwa 64 na hekari 3 kwa ajili ya shughuli za kilimo.
“Wananchi wa Katoto waliohamishwa walishapatiwa fidia ambayo ni ardhi kwa ajili ya makazi, kilimo na mifugo ikiwa ni pamoja na Serikali kuwapatia usafiri wa mali zao kipindi walichokuwa wanahama.
Hadi kufikia Mwezi Oktoba, 2025 uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Kasulu ulifanikiwa kuhamisha wananchi wote kutoka kitongoji cha Katoto na kwenda kitongoji cha Nyantuku kijiji cha Kagerankanda.” Alisema Mhe. Chande.