Shiza Kichuya aibukia Coastal Union

WINGA wa zamani wa Simba na Mtibwa Sugar, Shiza Kichuya amejiunga na Coastal Union akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba JKT Tanzania.

Kichuya ambaye ameitumikia JKT Tanzania kwa misimu miwili akitokea Namungo, amesaini mkataba wa mwaka mmoja Coastal Union na muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa ndani ya kikosi hicho.

Chanzo cha kuaminika kutoka Coastal Union kimelieleza Mwanaspoti wamemalizana na mchezaji huyo wanayeamini atakuwa chachu ya kuipambania timu kuhakikisha inafikia malengo ya kuendelea kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

“Hatupo vizuri sana na ligi msimu huu ni ngumu.Baada ya kuona ushindani ni mkubwa benchi lilipendekeza kuongezwa nyota wazoefu ili waweze kusaidiana na damu changa na hatimaye kufikia malengo tuliyojiwekea mwanzo wa msimu.

“Haijawa rahisi kunasa saini ya Kichuya kwani ni mchezaji ambaye alikuwa na ofa nyingi, tunamshukuru kwa kuichagua Costal Union tunaamini atakuwa kufanya kazi bora kutokana na uzoefu na ubora alionao,”  kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa kuthibitisha taarifa hizo, Kichuya amesema yeye ni mchezaji, hivyo ana uwezo wa kucheza timu yoyote ambayo inampa maslahi anayoyataka.

“Ni kweli mimi ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na JKT Tanzania na kuhusu kujiunga na Coastal Union mpira ni mchezo wa wazi, kama ni hivyo mtaniona uwanjani nikiipambania timu, kuthibitisha sio kazi yangu ni kazi ya klabu mimi ni kucheza,” amesema Kichuya.