UDOM yafafanua malipo kwa wanafunzi wasiofikia alama za ufaulu

Dodoma. Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umekiri kuwepo kwa gharama za malipo kwa wanafunzi ambao hawajafikia alama stahiki kwenye mitihani (carry over), lakini sababu yao ni kuzalisha wasomi wa viwango na si vinginevyo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa UDOM, Dk Rose Mdami amejibu hoja hiyo leo Jumanne Januari 27, 2026 akieleza mkazo umewekwa kwa vijana wazembe na wanaotaka kufaulu kwa mteremko pasipo viwango.

Kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa na taarifa zinazozunguka zikieleza wanafunzi UDOM    wanalipishwa Sh50,000 hadi Sh70,000 kwa somo moja ambalo mwanafunzi hajafikia ufaulu unaotakiwa. Nyingine ikilalamikia  vyoo vya wanafunzi kujaa jambo ambalo linaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa.

Taarifa hiyo inaeleza jinsi wanafunzi wanavyopata taabu kutokana na kulipia fedha hizo huku ikielezwa kuwa ni mpango ulioanzishwa kama kichaka cha upigaji na makusanyo yasiyo rasmi.

“Mwingine utamkuta anadai madeni mengi kwa marafiki na kwenye magenge ya chakula akipata hilo boom inambidi tu alipe, inabaki shilingi ngapi na ataishi vipi,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa upande wa vyoo inaelezwa kuwa vimejaa kwa muda mrefu lakini baadhi ya maeneo ya chuo hakuna maji, hali inayopelekea vyoo kuziba muda wote na kusababisha tishio na kero na  kwa wanafunzi.

Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Lughano Kusiluka amekiri kuiona taarifa hiyo lakini amesema uongozi utafuatilia zaidi kama kuna mambo ambayo yamejificha isipokuwa anachokijua kila jambo liko wazi, ndipo akaomba mwandishi kuwasiliana na kitengo cha mawasiliano.

“Hili nimelipokea kutoka kwako, lakini tuseme ukweli hayo mambo mengine hayapo na yaliyopo yako wazi,  Kitengo cha Mawasiliano kitatoa ufafanuzi zaidi, lakini asante kwa ushirikiano wako,” amesema Profesa Kusiluka.

Katika ufafanuzi wake Dk Rose amesema suala la kujaa kwa vyoo halipo ndani ya vitivo vyote UDOM, lakini akakiri kwenye malipo ya gharama za mitihani kwamba lipo kwa mujibu wa kanuni za chuo.

“Hilo suala la wanafunzi ku-carry lipo na utaratibu wa malipo upo kwa mujibu wa kanuni za undergraduate za mwaka 2019, kwa hiyo siyo jambo jipya, lengo letu ni kuzalisha watu wenye uwezo mkubwa wa kuja kulisaidia Taifa,” amesema Dk Rose.

Amesema mpango huo haulengi kumkomoa mtu na hakuna anayefelishwa kwa makusudi bali wanalenga kuwafanya vijana na watu wazima wanaokwenda kusoma hapo wajitahidi kuwa na ubora ambao unatakiwa kwenye masoko ya ajira.

“Lakini wanaosema tunawafelisha ili kupata fedha siyo kweli, mtu halipi fedha hizo mkononi bali anapewa namba ya malipo na kiasi anacholipa kinakwenda moja kwa moja serikalini, hakuna chuo kinakubali kutoa wanafunzi wa bora liende na wanaosema hayo ni wale wanaokesha kwenye starehe,” amesema Dk Rose.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, hivi sasa UDOM kina wanafunzi zaidi ya 37,000 lakini wanaokosa alama mara nyingi ni wachache zaidi na hao ndiyo wanatoa taarifa za kukichafua chuo wakitaka kufaulu kwa mtindo wanaotaka, bila kujali wengine ni madaktari ambao lazima waive ili kuwa na viwango bora vya kusaidia watu.