Dar es Salaam. Kanusho la Jeshi la Magereza dhidi ya taarifa inayodaiwa kuwa ni ujumbe wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kutoka gerezani kwenda kwa familia ya hayati Mzee Edwin Mtei, limeibua mjadala mpana ndani na nje ya mitandao ya kijamii.
Mjadala huo umejikita kuhoji sababu za Jeshi la Magereza kukanusha ujumbe huo ilhali umetolewa na chama chake, wakati Lissu bado ni mahabusu na hajahukumiwa, hivyo kikatiba bado ana haki zote za msingi.
Taarifa hiyo ilianza kusambaa baada ya Januari 24, 2026, wakati wa mazishi ya Mzee Mtei, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa, alisema chama hicho kilipokea ujumbe wa rambirambi wa kurasa tisa kutoka kwa Lissu akiwa gerezani, ambao baadaye ulisambazwa kwa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Katika ujumbe huo uliobeba kichwa cha habari “Hotuba ya Heshima kwa Edwin Mtei”, Lissu alimuelezea marehemu kama kiongozi jasiri wa kisiasa na mtumishi wa umma aliyekuwa na msimamo thabiti dhidi ya uchawa, akisema maisha yake yalijaa busara.
Hata hivyo, Jeshi la Magereza, kupitia taarifa iliyosainiwa na Msemaji wake Elizabeth Mbezi Januari 25, 2026, lilikanusha uhalali wa ujumbe huo, likisema si sahihi na unalenga kupotosha umma.
“Taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuwa ni ujumbe wa Tundu Antipasi Lissu uliotoka gerezani si sahihi bali ni ya kupotosha umma,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Jeshi hilo liliongeza kuwa mawasiliano yote ya watu waliopo gerezani husimamiwa kwa mujibu wa sheria na huthibitishwa ili kuhakikisha hayakiuki taratibu wala kuhatarisha usalama.
Akijibu kanusho hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Chadema, Gervas Lyenda, amesema chama kimeshangazwa na msimamo wa Jeshi la Magereza, akisisitiza kuwa ujumbe huo ulitoka kwa Lissu.
“Ujumbe wa Lissu kwenda ndani ya chama si lazima upitie kwa mkuu wa gereza, wala sheria haijaeleza hivyo,” amesema Lyenda katika mahojiano maalumu na Mwananchi Januari 26, 2026.
Mjadala huo umechochea maoni kutoka kwa wadau wa sheria. Wakili Jebra Kambole aliandika kupitia mtandao wa X akihoji kwa nini mjadala uelekezwe kwenye barua badala ya haki za mahabusu, ikiwemo kushiriki mazishi ya watu wa karibu.
Naye Wakili Michael Mwangasa amesema kisheria mahabusu anaruhusiwa kuandika barua, akisisitiza kuwa Lissu si mfungwa kwani bado hajahukumiwa.
“Katiba inatamka wazi kuwa mtu hahesabiwi kuwa na hatia kabla hajathibitishwa na mahakama. Mawasiliano ya mahabusu na mawakili, ndugu au marafiki ni haki ya kikatiba,” amesema.
Amesema magereza ni mahali pa kumuhifadhi mtuhumiwa, si kumwadhibu, akieleza kuwa kanusho la Jeshi la Magereza linaibua maswali zaidi kuliko majibu.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Boniface Mwabukusi, amehoji kupitia mtandao wa X sababu za Magereza kukanusha ujumbe huo badala ya kumruhusu Lissu mwenyewe kuzungumza.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, amesema kwa uzoefu wake wa kufanya kazi na Lissu kwa zaidi ya miaka 15, hana shaka kuwa ujumbe huo ni wake.
“Ule ni ujumbe wa Lissu. Ni mwandiko wake na hata mtindo wa maneno ni wa Lissu. Ukisoma unahisi kama anaongea mbele yako,” amesema.
Baadhi ya wananchi nao wameeleza kupitia mitandao ya kijamii kuwa ni Lissu mwenyewe ndiye mwenye mamlaka ya kukanusha au kuthibitisha uhalali wa ujumbe huo.
Reuben Kingamkono ameandika kuwa, “Kama kweli ujumbe haukutoka kwa Lissu, kwa nini wasimruhusu yeye mwenyewe aseme?”
Naye Thadei Mhabuka kupitia mtandao huo wa X ameandika kuwa kwa mtu anayefuatilia mazungumzo ya Lissu ujumbe unaodaiwa si wake ni wake.
Utaratibu wa mahabusu, mfungwa
Kanuni za Usimamizi wa Magereza za mwaka 1968 kifungu cha 11(1) kinaeleza kuwa mahabusu ambaye bado hajahukumiwa anaruhusiwa kuandika na kupokea barua katika nyakati zilizoorodheshwa, na pia wakati mwingine wowote endapo mkuu wa gereza ataona kuna umuhimu au sababu ya kuruhusu kufanya hivyo.
Lakini hali hiyo ni tofauti na kwa anayetumikia kifungo jela. Kila barua anayoandikiwa mfungwa au iliyoandikwa na mfungwa italazimika kugongwa muhuri unaoonyesha kuwa imesomwa na kuonyesha imeidhinishwa au haijaidhinishwa.
Pia, ofisa mkuu wa gereza au ofisa aliyepewa mamlaka kwa mujibu wa aya ya (1) anaweza kukataa kuidhinisha barua yoyote endapo ataona kuwa maudhui yake hayafai, au ikiwa barua hiyo ni ndefu kupita kiasi.
Kwa mujibu wa kanuni, endapo barua iliyoandikwa na mfungwa haitaidhinishwa, mfungwa huyo atajulishwa sababu za kutokuidhinishwa kwa barua hiyo na atapewa fursa ya kuiandika upya.