Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Ruvuma Alan Njiro, amesema kuwa umeme ni nishati muhimu lakini ni hatari endapo hautatumika kwa usahihi, kwani unaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.
Njiro ameyasema hayo Januari 27 alipotembelea shule ya msingi Mwenge na Shule ya sekondari Nasuri iliyopo Wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya utoaji wa elimu ya matumizi salama ya umeme kwa wananchi na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kuhusu faida na athari za umeme.
Kwa mujibu wa Njiro, elimu hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi uelewa mapema ili waweze kujilinda dhidi ya hatari za umeme na pia kuifikisha elimu hiyo kwa familia na jamii zao.
Ameeleza kuwa transfoma hutumika kupoza umeme kabla ya kusambazwa majumbani, hivyo ni hatari kwa mtu yeyote kuichezea au kukaribia miundombinu hiyo.
Njiro amewataka watoto kutoa taarifa kwa wazazi au walezi wao pindi wanapoona mtu akichezea transfoma au nyaya za umeme, ili hatua za haraka zichukuliwe, ameongeza kuwa ushirikiano kati ya TANESCO na jamii ni muhimu katika kuzuia ajali zinazoweza kujitokeza.
TANESCO Ruvuma imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kama sehemu ya mkakati wa kupunguza madhara yatokanayo na umeme, na kulinda miundombinu kwa kuzingatia majukumu yake muhimu ya kuzalisha, kusafirisha, kusambaza na kuuza umeme nchini.




