Dar/Mbeya. Utekelezaji wa Mpango wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance Act, 2023) umeanza rasmi jana, baada ya wakuu wa mikoa kote nchini kuanza kusimamia kazi ya usajili wa kaya masikini kama kundi la majaribio ya awali ya mfumo huo wa bima ya afya kwa wote.
Jumla ya kaya 276,000 zimebainishwa kuanza kunufaika na awamu ya kwanza ya mpango huo, kundi hilo litatumika kupima ufanisi wa mifumo ya bima ya afya kwa wote kabla ya kuanza kusajili makundi mengine ya wananchi.
Hatua hiyo inatekelezwa siku chache baada ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa kutangaza rasmi kuanza kutumika kwa Kitita cha Huduma Muhimu cha Bima ya Afya kwa Wote kwa awamu ya kwanza.
Akizungumza na Mwananchi jana, Meneja Uhusiano kwa Umma wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), James Mlowe amesema usajili wa kundi hilo unaanza kwa majaribio ili kutathmini kama mifumo iliyopo inafanya kazi kwa ufanisi.
Amesema majaribio hayo yatalenga kubaini namna bora ya kugawanya rasilimali, wakiwamo watumishi wa afya, dawa na vifaa tiba, ili kuhakikisha kasoro zozote zitakazojitokeza zinarekebishwa kabla ya makundi mengine hayajaanza kujiunga na mfumo.
“Kwa sasa tunafanya majaribio kwa kundi hili linalogharamiwa na Serikali ili kuona mwitikio na changamoto zinazoweza kujitokeza. Kuanzia leo usajili umeanza kwa kaya 276,000 na tunatarajia zoezi hili litachukua kati ya mwezi mmoja hadi mwezi mmoja na nusu,” amesema Mlowe.
Amefafanua kuwa orodha ya kaya husika itaonesha vijiji wanakotoka, hatua itakayowezesha watendaji kuwafikia kwa urahisi, kuwasajili na kuwatolea vitambulisho, kazi inayohitaji muda wa kutosha kuifanikisha.
Baada ya kukamilika kwa usajili huo, Mlowe amesema kaya hizo zitaunganishwa na vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoteuliwa na kuanza kupata huduma chini ya mpango huo.
Ameongeza kuwa baada ya hatua zote kukamilika, NHIF itafanya tathmini ya kina kuhusu ufanisi wa mfumo huo na mgawanyo wa rasilimali, kabla ya kuanza kusajili makundi mengine ya wananchi.
Mlowe amesema usajili unahusisha ushirikiano wa watendaji wengi, akieleza kukamilika kwake kutatoa fursa ya kubaini mbinu bora za kuendelea na uandikishaji kwa makundi mengine.
Kwa sasa, amesema katika vituo vya kutolea huduma za afya mchakato unaoendelea ni kuhakikisha mifumo ya kidijitali inasomana vizuri, hususan katika vituo vyote vya Serikali ukilenga kurahisisha utoaji wa huduma.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Elizabeth Nyema amesema Serikali imejipanga kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, baada ya kutoa elimu ya awali kwa wananchi tangu Desemba mwaka jana, na kkwa sasa wako katika hatua za mwisho za kuanza usajili rasmi.
Amesema NHIF inaendelea na taratibu za kuainisha maeneo ya kusajili kaya maskini katika halmashauri zote za mkoa huo, huku matarajio yakiwa ni kuhakikisha wananchi wote wanapata bima ya afya.
“Kilichobaki ni kukamilisha mifumo. NHIF wanakamilisha taratibu zake na sisi tumetoa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya na matumizi yake. Lengo letu ni kumfikia kila mwananchi katika eneo lake,” amesema Dk Nyema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli amesema tayari wameanza utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote kwa kushirikiana na viongozi na mamlaka za ngazi za chini.
Mweli amesema ili kufanikisha zaidi zoezi hilo, halmashauri inatarajia kukutana na watendaji na wenyeviti wa vitongoji, vijiji na kata kwa siku saba, kabla ya kufanya mikutano ya hadhara kwa wananchi kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella amesema tayari wameanza kutoa elimu na hamasa kwa wananchi ili waweze kutambua na kujiandaa na huduma hiyo.
“Usajili bado haujaanza rasmi, lakini tulianza kwa kutoa elimu na hamasa ili wananchi, wakiwamo makundi maalumu, waelewe umuhimu wa huduma hii pamoja na gharama zake,” amesema Yegella.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Florah Luhala amesema baada ya uzinduzi wa bima ya afya kwa wote, halmashauri yao imejipanga kuhakikisha wananchi wanaielewa na kunufaika na huduma hiyo, huku usimamizi wa utekelezaji ukipewa kipaumbele.
