Dar es Salaam. Utata umeibuka kati ya familia ya Ramadhani Chaulembo, inayoishi Dar es Salaam dhidi ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, kuhusu umiliki wa kiwanja namba 77, kila upande ukidai unalimiliki eneo hilo kihalali.
Kwa mujibu wa familia hiyo ya Chaulembo, eneo hilo ni mali yao halali tangu mwaka 1977, baba yao alipolinunua kutoka kwa Mohamed Zahoro aliyekuwa analimiliki awali, hivyo Halmashauri ya Temeke imelivamia.
Upande wa Halmashauri ya Temeke, unasema unalimiliki eneo hilo tangu mwaka 1980 na kwamba una hati miliki halali, hivyo wanaodai wanalimiliki wanatafuta huruma ya jamii, kwani madai yao hayana msingi.
Akizungumzia hilo, Ijumaa Januari 23, 2026 kwa niaba ya familia hiyo, Juma Chaulembo amedai baba yao Ramadhani Chaulembo, alinunua eneo hilo mwaka 1977 kutoka kwa Mohamed Zahoro aliyekuwa mmiliki wa awali.
Amesema eneo hilo linalojulikana kwa jina la Plot No.77 lililopo Mtoni ni mali yao, kwani liliponunuliwa baba yao alikwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati huo kuhamisha umiliki.
“Akiwa katika hatua za kukamilisha uhamisho wa eneo hilo lenye mita za mraba 100,922 baba yetu alifariki dunia ingawa taratibu za uhamisho zilikuwa zinakaribia kukamilika na zilishaanza kumtambua kama mmiliki halali,” amesema.
Tangu mwaka huo, amesema baba yao alitambulika kama mmiliki halali wa plot hiyo No77 na walikuwa wanalipia kodi ya ardhi kila mwaka.
Juma, ameeleza ulipofika mwaka 2000 katika eneo hilo lililopo karibu na ukanda wa bahari kulitokea mmomonyoko wa udongo.
Kwa sababu hiyo, amesema familia ilienda kuiomba iliyokuwa Halmashauri ya Jiji kabla ya kuhamishiwa Halmashauri ya Temeke, kumwaga taka ili kuzuia mmomonyoko.
“Tulienda kuzungumza nao wakaja tukakaa nao vikao na walitukubalia ombi letu, wakawa wanaleta taka na baadaye lilikaa sawa,” amesema.
Baada ya eneo kukaa sawa, amesema halmashauri hiyo ikaanza kutafuta namna ya kujimilikisha kwa njia za mikato bila kwenda kuiona familia hiyo.
“Wakaanza taratibu za kupima eneo, mwaka 2005, huku eneo linaendelea kusomeka Plot 77 na mmiliki Ramadhani Chaulembo, na wakaja kujenga kiwanda cha gesi bila kuishirikisha familia na hakikufanya kazi,” amesema.
Baada ya kuona uwekezaji wa kiwanda hicho, amesema familia ilishtuka na kuandika barua kwenda kwa Mkurugenzi kuhoji wamepataje umiliki wa eneo hilo kiasi cha kufanya uwekezaji bila ridhaa ya familia.
“Mkurugenzi hakujibu hoja za msingi tukaweka bango la kuzuia watu kufanya kazi katika eneo hilo, ndipo tuliendelea kufuatilia kudai haki ya eneo hili, lakini tunazungushwa,” amesema.
Kwa kuwa walikuwa wanalipia eneo hilo kila mwaka, ameeleza ilifikia hatua waliiomba halmashauri ikahuishe mipaka ijulikane eneo lao linaishia wapi.
“Dhamira yetu ya kufanya hivi ilikuwa njema tulitaka kumaliza mvutano baina yetu na halmashauri kwa sababu tunalipia eneo hili kila mwaka, wao wanang’ang’ania eneo lao,” amesema Juma.
Katika maelezo yake, Juma amesema Januari 9, 2026, maofisa wa halmashauri hiyo walifika eneo hilo saa saba usiku na kuweka matangazo yakieleza kuwa kuanzia Januari 10, 2026 jioni, hakuna mtu anayepaswa kuendelea na shughuli zozote katika eneo hilo, ambalo familia ilikuwa ikilitumia kama maegesho ya malori na magari ya kawaida.
“Usiku wa kuamkia Januari 11, nilishangaa kuona gari aina ya Coaster likishusha watu zaidi ya 100 eneo hili wote wakijitambulisha walinzi, wakinitaka niondoke mara moja pamoja na kuondoa magari yote yaliyokuwa kwenye maegesho,” amesema.
Amesema baada ya kueleza hivyo aliwakatalia akisema eneo hilo ni mali halali ya familia yao, lakini asingeweza kuondoka kwa sababu ndani ya maegesho kulikuwa na mali za watu ikiwemo magari ya wateja wake.
“Baada ya mabishano ya muda, walidai ninazuia utekelezaji wa majukumu yao, ndipo walinikamata na kunifunga kamba kisha walitumia magari aina ya breakdown kuhamisha magari yote yaliyokuwemo, shughuli liliyochukua siku mbili,” amesema.
Baada ya kumaliza kutoa magari hayo, amesema walizungushia utepe na lipo chini ya maofisa wa halmashauri hiyo na wamepiga marufuku shughuli zozote zisifanywe ndani yake.
“Eneo hili ni mali ya familia yetu, halmashauri inatumia mabavu kupora, tunachohitaji basi waje wahuishe mipaka ijulikane sehemu yao iko wapi na familia yetu eneo letu mwisho wapi, inakuaje wanatumia mamlaka vibaya,” amesema Juma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke, Jomaary Satura amekanusha madai yaliyotolewa na familia hiyo, akisema hayana msingi na yanakusudia kutafuta huruma kwa jamii.
Amesema halmashauri hiyo inamiliki eneo hilo tangu miaka ya 1980, hivyo haijafanya uvamizi wowote kwani ina hati halali.
“Halmashauri hatujavamia eneo lolote. Tuna hati miliki halali. Malalamiko hayo si ya kweli. Chaulembo anatoka familia kubwa hapa Temeke, hata wenzake wanamfahamu, ni mtu mjanja mjanja,” amesema Satura.
Katika maelezo yake, Satura amesema eneo hilo awali lilikuwa dampo la taka na baada ya shughuli za utupaji taka kusitishwa, mlalamikaji alianza kulitumia kuegesha magari kwa ajili ya kujipatia kipato.
“Unajua huo ni uvamizi sawa na uvamizi mwingine wanajua wakivamia eneo la Serikali huwa inasahau, baada ya muda fulani wanakuwa na umiliki kamili,” amesema.
Satura, amehoji iwapo mlalamikaji ana hati, kwa nini hataki kwenda kwenye vyombo vya utoaji haki, badala yake anakimbilia kwenye vyombo vya habari, akisema hatua hiyo inaashiria kutafuta huruma kwa jamii.
Amesema eneo hilo si mali yake binafsi, bali ni mali ya umma, akieleza kuwa yeye ni mkurugenzi wa halmashauri na katibu wa baraza la madiwani.
Amesema yeye ni mtendaji mkuu anayesimamia shughuli zote za kiutendaji kwa mamlaka aliyopewa na baraza la halmashauri.