Vijana wakali wa Tehama kukumbatiwa kukuza uchumi

Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kuwakumbatia na kuwaendeleza vijana wenye vipaji katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama),  ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini, hususan katika kipindi ambacho matumizi ya teknolojia za kidijitali yanaendelea kushika kasi, ikiwemo akili unde (AI).

Hatua hiyo inatekelezwa kupitia Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kutumia teknolojia kama kichocheo kikuu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Serikali imesema uchumi wa kidijitali unajengwa kwa kiasi kikubwa na kampuni changa za Tehama,  kwa kuwa ndizo zinazobeba dhamana ya ubunifu na uundaji wa ajira, hivyo ni muhimu kuziwekea mazingira rafiki ya ukuaji na maendeleo.

Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Tisa la Mwaka la Tehama (TAIC-2026) lililoandaliwa na Tume ya Tehama na kuwakutanisha wataalamu mbalimbali jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa, alisema Serikali itaendelea kuibua na kuhimiza masuluhisho ya kiteknolojia yanayolenga kuleta mabadiliko ya kiuchumi.

Alisema mkazo unawekwa katika kukuza ushiriki na ushindani endelevu wa kampuni za Tehama za ndani, ikiwemo uwezeshaji wa mitaji kwa kampuni changa, usimamizi na mikakati ya kukuza teknolojia za kidijitali zinazoibukia, usalama wa mitandao, usimamizi wa data pamoja na kujenga ujuzi wa Tehama kwa watumiaji na wataalamu wa huduma za kidijitali.

“Tutaendelea kuibua na kuleta masuluhisho ya kiteknolojia yatakayosaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika sekta za huduma, uzalishaji na maeneo ya utawala,” alisema Mkapa.

Alieleza kuwa ufikiwaji wa uchumi wa kidijitali unafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa vijana na hata kwa vizazi vijavyo, huku akitaja ubunifu wa Tehama na uanzishwaji wa kampuni changa za Tehama kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa.

“Nimetaarifiwa kuwa mmejadili masuala haya kwa kina na hata kupata uzoefu kutoka kwa wageni wa nchi mbalimbali walioshiriki kongamano hili. Serikali inaendelea na taratibu za kuandaa sera ya kampuni changa na imefikia hatua nzuri,” alisema.

Aliongeza kuwa ni jukumu la wadau wote kuwahamasisha vijana kuwa wabunifu, kuanzisha kampuni na biashara changa, na hatimaye kujiajiri, huku akizihimiza kampuni changa kujisajili katika mfumo wa usajili wa Tume ya Tehama.

Katika hatua nyingine, alisema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika biashara mtandao, kama fursa jumuishi inayowawezesha wananchi kubuni na kuuza bidhaa na huduma zao kwa njia ya kidijitali.

“Napenda kuielekeza Tume kuboresha kwa haraka mfumo wa utambuzi na usajili wa wataalamu wa Tehama ili nchi iwe na programu ya kitaifa ya kuwaendeleza wataalamu wake, kwani ni kiungo muhimu katika kufikia uchumi wa kidijitali,” alisema.

Akizungumza kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkunde Mwasaga, alisema jukumu la Tume ni kujenga uwezo wa jamii kutumia mifumo ya Tehama, akisisitiza kuwa mustakabali wa dunia unaelekea zaidi katika matumizi ya AI.

“Jukumu letu ni kuhakikisha tunawatambua vijana wenye vipaji walipo, kuwajengea uwezo na kuwaendeleza pamoja na kampuni changa. Uchumi wa kidijitali unajengwa na watu wenye vipaji,” alisema.

Alifafanua kuwa vijana wanaojihusisha na ubunifu wa teknolojia wakiwa wadogo, ikiwemo utengenezaji wa maroboti, wana msingi mzuri wa kuwa wataalamu mahiri hapo baadaye, jambo linalotoa picha ya mafanikio makubwa ya taifa katika siku zijazo.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Huawei Tanzania, Boniface Ntimba, alisema kutokana na dunia kuelekea katika mapinduzi ya kidijitali, kampuni hiyo imeona umuhimu wa kuunga mkono juhudi za Serikali na Tume ya Tehama.

“Ndiyo maana sisi kama Huawei tunashirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Serikali katika miradi ya Tehama, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo na kuajiri wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani na programu zetu za mafunzo,” alisema.