Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kuwanasa wakazi wawili wa Mabogini Kilimanjaro na Tanga waliodaiwa kumteka Aiti Ramadhani (Mazura) na kuwashurutisha ndugu zake kutoa fedha.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa sehemu ya mtandao wa watu wanaoendesha uhalifu wa utekaji katika mkoa huo huku wakidai fedha kutoka kwa ndugu wa mateka hao ili wawaachie huru.
Watuhumiwa hao Stephano Elias (27), mkazi wa Kilimanjaro na Moses Joseph (26), wanadaiwa kumteka Aiti na kisha kuishurutisha familia yake iwalipe Sh14 milioni kama sharti la kumuachia huru.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, utekaji huo ulifanyika wiki iliyopita katika eneo la machifoni Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Amesema watuhumiwa hao walikamatwa Januari 19, 2026 katika Wilaya ya Handeni na kisha kumsalimisha mateka huyo kwenye familia yake.
“Hawa ni wahalifu walio katika mtandao hatari wa utekaji watu na kuwashikilia kinyume cha sheria, bado tunawafanyia mahojiano na uchunguzi utakapokamilika tutawafikisha mahakamani wakajibu tuhuma zinazowakabili,” inaeleza taarifa hiyo.
Katika tukio jingine, Kamanda Mchunguzi amesema jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 55 wakiwamo vijana wanaotumia silaha za jadi yakiwamo mapanga na kupora, pikipiki, simu za mikononi, friji na televisheni.
Amesema katika msako huo, Jeshi la Polisi limenasa jumla ya simu 25 za mkononi, pikipiki 50 zikiwemo 28 zisizokuwa na namba za usajili, madumu ya mafuta ya kula, televisheni saba na friji nne.
“Hawa vijana wanaojulikana kwa jina la vishandu, tunawasaka popote walipo hadi tuhakikishe mtandao huo unamalizika na kukomeshwa kabisa ili wananchi waishi kwa amani,” amesema Mchunguzi.
Amesema katika msako huo, pia, Jeshi la Polisi linamshikilia Ali Bwengo kwa tuhuma za kujihusisha na unyang’anyi wa kutumia silaha uliofanyika hivi karibuni Amboni jijini Tanga.