Dodoma. Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu ametilia shaka ukamilishaji wa Katiba mpya kutoka na mtindo wa kuja kwa alichoita vipande badala yake akapendekeza mambo manne ili kufikia hatua hiyo.
Ado ametoa mapendekezo hayo leo Jumatano Januari 28, 2026 wakati akichangia hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Novemba 14, 2025 wakati akizindua Bunge la 13.
Kwenye hotuba hiyo, Rais Samia aligusia suala la mchakato wa Katiba mpya ambapo aliahidi ndani ya siku 100 za utawala wake mchakato utaanza kwa kuunda Tume ya maridhiano ambayo itapendekeza njia ya kutumia.
“Lakini mheshimiwa Mwenyekiti, nilifarijika juu ya ahadi ya Mheshimiwa Rais, ukiacha ile ya kuponya majeraha ya uchaguzi 2025 lakini kwenye hili la kufufua mchakato wa Katiba mpya hilo ni jambo jema kabisa,” amesema Ado.
Hata hivyo, ameonyesha hofu na mashaka kuwa mchakato huo umetaja vipande vipande jambo alilosema linatia mashaka, lakini akapendekeza mambo manne ili kufanya mchakato uende vizuri.
Amesema kipande ambacho kimeanza kwa sasa ni Tume ya usuluhishi ndani ya siku 100 za kiongozi huyo madarakani wakati yeye anapendekeza mchakato mzima ushughulikiwe kwa wakati mmoja.
“Tunataka Serikali ije na ratiba kamili kushughulikia suala la Katiba mpya, Serikali ituambie mtindo ambao itautumia kwa wananchi wa Tanzania ili kujipatia Katiba yao,” amesema.
Ameyataja mambo hayo ni hitaji la kuzifanyia mapitio sheria zinazosimamia mchakato wa Katiba mpya ambao ndani yake kutakuwa na sheria ya mabadiliko ya Katiba mpya na sheria ya kura ya maoni.
Nyingine ni mchakato wa kura ya maoni ambao utaruhusu kuwa na mkutano wa kitaifa kwa ajili ya kupata muafaka wa pamoja kwa ajili ya masuala ya Katiba mpya na lazima kuwepo na timu ya wataalamu, ambayo itaandaa mchakato wa Katiba mpya kabla ya kufikia kura ya maoni.
Mbali na suala la Katiba mpya, kingine ametaja sakata la waliokamatwa katika kipindi cha machafuko ya Oktoba 29, 2025 akiitaka Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Katiba na Sheria wafanye uchunguzi wa kina na kujiridhisha kama watu wote wametoka.
“Ahadi ambayo Rais aliitoa kuwaachia watu waliokamatwa kwenye matukio, kuwa huru inapaswa uchunguzi ufanyike kama watu wote kweli wameachiwa huru, mtu mmoja akitekwa ama kuwekwa ndani, ukoo mzima unakuwa kwenye huzuni,” amesema.
Amezungumzia suala la amani akisema, ni eneo ambalo haliwezi kuwa na maana kama halitakwenda na haki kwani vitu hivyo viwili lazima viendane kwa pamoja.
“Amani ni zao la demokrasia na haki, hakuna demokrasia bila haki na hakuna amani bila haki, na bila amani hakuna maendeleo, kama ukisisitiza juu ya amani bila haki hakutakuwa na amani,” amesema Ado.
Ado ambaye ni Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo amesema ukiwa unazungumzia amani hata ukikesha kuwaambia watu wapende amani na wapende nchi yao lakini bila kusisitiza haki hakuna amani.
Kingine ametaja sakata la waliokamatwa katika kipindi cha machafuko ya Oktoba 29, 2025 aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Katiba na Sheria wafanye uchunguzi wa kina na kujiridhisha kama watu wote wametoka.
“Ahadi ambayo Rais aliitoa kuwaachia watu waliokamatwa kwenye matukio, kuwa huru inapaswa uchunguzi ufanyike kama watu wote kweli wameachiwa huru, mtu mmoja akitekwa ama kuwekwa ndani, ukoo mzima unakuwa kwenye huzuni,” amesema.
Kwa upande wa jimbo lake amesema bado kuna shida ya maji licha ya kuwepo kwa mradi wa Sh3.4 milioni huku akipeleka kilio cha hitaji la kukatika katika kwa umeme, ambako hufikia mara 20 kwa siku.