Afariki kuliko kufa kila kitu, mafyatu huishi ‘kiafariki’!

Kuna bara linaitwa Afariki aka Fyatuland. Ajabu, imejiliwa utajiri na umaskini wa kutengenezwa kadhalika! Sizungushi. Nafyatua mshononi tena bila huruma.

Nataka tufikiri pamoja juu ya maajabu haya tena bila aibu wala woga. Munene anasafiri kwa mindinga mia tena mtaani. Mafyatu awazugao ni waajiri wake wanafyatuana kwenye ngwarangwara na misongamano!

Ajabu, pamoja na dhuluma hii, kunakuwa na amani bila haki! Hakuna anayeuliza zaidi ya kuumia kimya kana kwamba chapaa au doh inayotumika siyo kodi yake! Mafyatu hawajui, na munene hajui.

Hakuna anayetaka kujua japo wote wanajua. Wote hawajui isipokuwa Fyatu Mfyatuzi mwana wa Mfyatukizo kijukuu cha Mfyatuliko wa Mfyatuko! Wanajua ila wanajifanya hawajui! Wanajitoa ufahamu kwa kujifyatuafyatua kifyatu!

 Munene anatumia njuluku nyingi kuliko hata miradi ya umma iliyokwamishwa kwa hujuma! Huku siyo kuumizana bila sababu? Kwani, mnene hawezi kuwe na msafara reasonable? Nawaona wakizindua miradi hewa! Nani amzindue nani ili wote tuzinduke tuache kuzingua, kuzinguliwa, na kuzinguana?

Twende kazi. Tufikiri pamoja tena kwa umoja. Jiulize kimya kimya. Kwanini kwenda kuzindua, mfano, mradi wa madafu laki moja kwa kutumia mamilioni kwenye msafara na kulipana posho?

Kwani lazima wewe? Huku si wanene kuwanyonya wakondaji na kugeuza madogo kuwa makubwa na kuleta hasara na madhara makubwa? Hivi si aibu na ufisadi mkubwa?

 Naona wanene wakishindana kwa misafara ya ndinga! Nani ajuaye kesho watashindana kwa misafara ya mapipa kwenda kutanua ghaibu? Kwa israfu na ubinafsi huu, mafyatu wanaingizwa hasara na mateso kiasi gani? Nani anapoteza muda kuuliza maswali haya au kufanya mahesabu? Nani afanye hivi wakati anapaswa awe na PhD ya hesabu au sayansi? Kama huna PhD, usijipotezee wala kutupotezea muda kuhoji au kufanya mahesabu.

Kuna mwanamuziki fyatu kama mimi aliyewahi kuimba, japo akilalamika kinamna, kuwa unaibiwa kuku, unauza ng’ombe kwa kesi yake! Unaibiwa madafu mia, unaunda tume inayotumia milioni kuchunguza wizi! Huku ni kuunda tume au kuchuuzana? Je huu si wizi ndani ya wizi? Baadhi ya wahalifu wanaiba au kuua. Ajabu, wanaunda tume ya kujichunguza!

Kwani, haya hayapo? Kwa Afariki iliyofishwa ikafariki na kuitwa Afariki, kila kitu kinawezekana! Kisichowezekana kinawezekana na kinachowezekana, hakiwezekani! Pamoja na kufariki, Afariki imeshindikana! Haifi moja kwa moja na kuzikwa!

Kwa Waafariki, waliofariki wanapiga kura! Kwao, mbwa analinda nyama na jambazi akalinda benki! Na amani inatamalaki! Waliofishwa wanapata na waliowaua! Katika Afariki, haki ilifariki na amani ilitawala! Uhuru na usawa vilifariki bila kufarakana! Katika haki, kila mmoja amefariki.

Katika Afariki, sijui kwa vile imefariki, munene anapangiwa njuluku mingi kuliko wizara! Kwanini katiba zinaruhusu wanene kupanua na kutanua ulaji kulisha walaji wenzao ilhali mafyatu wanafyatuliwa na umaskini? Je huku si kufariki? Wamekosea wapi wanaoiita Afariki wakijua ilivyofariki?

Kwa Afariki, fikra tunduizi zimefariki. Nani anapoteza muda kufikiri? Yanini kuumiza kichwa? Kwanini wadosi wetu wanatumia misafara mirefu ya helkopta na michuma ya bei mbaya ilhali madawa hos, magari ya wagonjwa, na watoy wanakalia mawe ukiachia mbali kutopate elimu bure? Kwanini kampeni ni bora kuliko maisha ya mafyatu? Kufyatua vilivyo, wajanja wanatoa ahadi wasitekeleze! Huku siyo kugeuzana mafala? Kama haitoshi, wanene wanakula bure wakati watoy hawana msaada wowote! Si waliwahi kuahidiwa malife bora kwa wote? Si wana bora maisha?

Sijui kwanini wadosi wanapenda kutangatanga badala ya kukaa ofisini na kuchapa kazi? Je, ofisi zinawasha au zinawafanya wasipige kampeni hata kabla ya kipenga kupulizwa?

Kwa nini wanene wanapenda kupokelewa na umati bila kuchelea kupoteza muda na njuluku vya umma? Wanatumia muda mwingi maulajini wakijihudumia na kutalii badala ya kuhudumia mafyatu?

Huku si kuwatumia mafyatu ikiwahadaa unawatumia? Kuna siku, Afariki wanene watakwenda kuzindua sherehe ya ng’ombe kujifungua! Je, wanazindua au kufungua wanayofungua au kutafuta namna ya kufungua mifuko ya umma walipane na kufungua mishipi wakati mafyatu wakifungishwa mishipi? Huu nao ni ushipa! Tafadhali usiniulize. Hii ndiyo Afariki ulikofariki uwezo wa kuhoji. Kwanini kuhoji au kuhojiwa ili kufarakanishana na kuondoa amani?

Kwa Afariki, uongozi, ukweli, na uongo vinafanana! Vitu viliupindua utu! Hata aibu ilifariki! Unaweza kufanya vitu vya aibu na bado ukajisifu au kusifiwa! Hivi kuendesha magari kwenye barabara zenye mashimo siyo aibu?

 Nani anaona aibu iwapo wahusika wanajaza matumbo na mifuko yao? Dawa hos hakuna japo magari ya kuzua, sorry, kuzuia ghasia yanapatikana! Kila mwaka, tunanunua ndinga, sorry magari ya bei mbaya aka oil guzzlers badala ya trekta lau tulime tuzalishe na kula wote! Hata hivyo, wingi wa chakula utashibisha wengi, bongo zao zitafufuka, kuacha kufariki, kuanza kufikiri, na kuhoji kila kitu! Nani anataka hili? Iweje, na kwanini?

Japo ni jina, jina baya humharibu mwenyewe. Tangu tuwe Afariki, kila kitu kilifariki kulhali! Kumbe naweweseka usingizini!