ALAF YAZINDUA TUZO YA 10 YA KISWAHILI YA SAFAL 2025

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya ALAF Tanzania imezindua rasmi Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika kwa mwaka wa 2025, ambapo wanaotarajiwa kushiriki shindano hilo wametakiwa kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya kupitiwa na majaji.

Hiyo ni tuzo ya 10 tangu kuanzishwa kwake 2015 na inafadhiliwa na kampuni ya ALAF Limited ya Tanzania na Mabati Rolling Mills ya Kenya (kampuni tanzu za Safal Investments Mauritius Limited).

Akizungumza jijini Dar es Salaam Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited Tanzania, Hawa Bayumi amesema tuzo hiyo inaendelea kukua mwaka hadi mwaka huku ikivutia washiriki wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani.

“Hadi leo hii, zaidi ya kazi 3000 zimeshawasilishwa katika shindano hilo na washindi 29 wameshapokea zawadi zao ndani ya miaka hii 10. Miswada 22 kati ya iliyoshinda imeshachapishwa na Mkuki na Nyota Publishers na iliyobakia ipo kwenye mchakato wa kuchapishwa,” ameeleza.

Kuhusu zawadi alisema katika kipengele cha Riwaya mshindi wa kwanza atazawadiwa Dola 5,000 na Mshindi wa pili Dola 2,500, katika kipengele cha ushairi mshindi wa kwanza ataondoka na Zawadi ya Dola 5,000 na Mshindi wa pili Dola 2,500 wakati katika kipengele kipya cha hadithi fupi kutakuwa na mshindi mmoja tu atakayepokea Dola 2500.

Miswada itaanza kuwasilishwa kuanzia leo hii tarehe 28 Januari hadi tarehe 31 Machi 2026 ambapo zoezi hilo litafungwa rasmi ili kuwapa majaji nafasi ya kupitia miswada husika. Hafla ya utoaji tuzo inatarajiwa kufanyika Julai 2026 ambapo washindi watatangazwa.

“Tunatoa rai kwa waandishi duniani kote watumie fursa hii kujitangaza, wachapishe kazi zao ili wachangie katika kukuza lugha adhimu ya Kiswahili,” amesisitiza Bi. Bayumi.

Amebainisha kampuni ya ALAF inajivunia na itaendelea kutoa mchango wake katika kukuza lugha ya Kiswahili kama chachu ya maendeleo ya kiuchumi, taaluma na utamaduni nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Dk.Ramadhani Kadallah ameipongeza ALAF Kwa jitihada zake ze Mukunza Lugha ya Kiswahili.”Tutaendelea kushirikiana na waandaaji kwani tuna maslahi makubwa na jambo hili.”

Mmoja wa washindi wa mwaka jana, Bashiru Abdallah alitoa Rai Kwa watunzi kutumia fursa hii kujitangaza na kuhakikisha wanaiandaa kazi zao vizuri ili wawe katika nafasi nzuri ya kushinda. “Ukiachia kushinda, tukio hili ni sehemu nzuri yakukutana na watu mbalimbali na kubadilishana uzoefu,” alisisitiza.

Tuzo hiyo, iliyoanzishwa mwaka wa 2014 na Dkt. Lizzy Attree (Mkurugenzi wa Tuzo ya Caine) na Dkt. Mukoma Wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell), lengo kuu likiwa ni kutambua kazi nzuri za uandishi kwa lugha za Kiafrika sambamba na kuhimiza kazi za tafsiri kutoka lugha moja hadi nyingine miongoni mwa lugha za Kiafrika.

Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (Mabati Rolling Mills Limited ya Kenya na ALAF Limited nchini Tanzania) kwa pamoja yanajulikana kama The Safal Group. Safal Group ndiyo mzalishaji mkubwa wa bidhaa za kuezekea Barani Afrika ambapo kampuni hiyo inafanya jumla ya shughuli za uwekezaji 36 katika mataifa 11 Barani Afrika.