Fedha za mchango wa Lissu zapigwa, mmoja adakwa

Dar es Salaam. Zaidi ya Sh19 milioni kati ya Sh41 milioni zilizochangwa na Watanzania kwa ajili ya kumsaidia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu zimepigwa na wajanja waliogawana.

Kampeni ya kuratibu na kuhamasisha Watanzania kumchangia Lissu anayekabiliwa na kesi ya uhaini, iliendeshwa na baadhi ya makada wa Chadema waliopo ndani na nje ya nchi (Nairobi).

Fedha hizo zilichangwa mwaka 2025 kupitia namba za simu na akaunti za benki zilizokuwa zimewe katika kipeperushi kilichoandikwa ‘Funga mwaka 2025 na Tundu Lissu’ baba wa GenZ kilichosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya Chadema, kinaeleza fedha hizo hazikuchangwa na taasisi hiyo, bali kunadaiwa kumeibuka mtindo wa watu kuchangisha fedha kwa ajili jambo fulani pasipo viongozi wa Chadema kuelezwa zaidi ya kuona mtandaoni.

Inadaiwa makada watatu wa Chadema, majina yamehifadhiwa waliifuata familia na Lissu na kubahatika kuonana na ili Alute Mughwai (kaka yake Lissu) kumwelezea kusudio hilo.

Baada ya kuonana naye walimweleza kuwa wanataka kufanya harambee ya kumchangia Lissu ya kufunga mwaka kwa madai gerezani aliko mahitaji hayamtoshelezi.

“Baada ya Mughwai kusikia hivyo, na vijana waliomfuata anawajua na kuwaamini hakuwa na wasiwasi, na aliwaamini. Wakamshawishi afunge akaunti maalumu za simu pamoja na benki,” kimeeleza chanzo.

Baada ya hapo matangazo ya uhamasishaji wa Watanzania kumchangia Lissu yakaanza hasa mitandaoni na wananchi wakaanza kutuma miamala na Desemba 31, 2025 pazia likafungwa.

Inadaiwa baada ya mchakato huo kufungwa ikatangazwa imepatikana Sh26 milioni, lakini wakati Mugwai anakabidhiwa simu zilizokuwa zikitumika, akaona muamala wa Sh 22 milioni.

“Ndipo alipoenda benki kuomba taarifa na kubaini miamala yote jumla Sh41 milioni. Maana yake Sh19 milioni zimeliwa,” kimeeleza chanzo hicho.

“Mzee akaanza kuwahoji na katika miamala ikaoneka kuna fedha zimetumwa Nairobi (Kenya) kupitia namba za nchi zikienda kwa….huku kwa namba za Kitanzania kuna mtu alijitumia Sh3 milioni.”

Inaelezwa Mughwai aliwapa muda akiwataka vijana hao kurudisha fedha zote zilizokusanywa, lakini haikuwa hivyo kwa sababu inasemekana fedha zilishaliwa.

Inadaiwa Mugwai aliwapa muda huo kuanzia Januari 10, 2026, lakini hakupata mrejesho ndipo alipofungua kesi Arusha na kupewa RB.

Mwananchi limemtafuta Mugwai kuhusu suala hilo, ambapo alijibu kuwa, “siwezi kusema zaidi kwa sababu jambo lipo polisi kwa ajili ya uchunguzi.

“Jambo lipo chini ya upelelezi wa polisi, jaribuni kuzungumza nao kama watawapa taarifa kama unahitaji ufafanuzi zaidi waulize watakupatia,” ameeleza Mughwai.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema amekiri jeshi hilo kumshikilia mkazi wa jiji hilo, Fredrick Mbwambo kada wa Chadema kwa tuhuma za wizi wa fedha zilizokusanywa kutoka kwa wananchi kwa ajili ya Lissu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda Masejo, fedha hizo zilikusanywa kupitia kampeni iliyopewa jina la funga mwaka na Tundu Lissu.

Kamanda Masejo amesema Mbwambo alikamatwa Januari 27, 2025 baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mughwai aliyebaini wizi wa fedha hizo zilizokuwa zimechangwa.

“Ufuatiliaji wa awali umeonyesha kuwa ukusanyaji huo wa fedha ulikuwa ukifanywa kupitia namba mbili za simu za kampuni tofauti ya simu inadaiwa zilihamishiwa kwenye namba mbili za simu moja ikiwa ni ya kampuni ya Tanzania na ya pili ni kampuni ya simu ya nchi jirani,” amesema.

“Kutokana na malalamiko hayo jalada lilifunguliwa kwa mujibu wa taratibu na uchunguzi kuanza sambamba na ukamataji huo, jitihada za kuwatafuta watuhumiwa wengine waliotumiwa kuhusika katika wizi huo pamoja na vielelezo unaendelea ili hatua za kisheria zifuate,” amesema Kamanda Masejo.