Fursa wananchi kuwekeza kampuni hizi Afrika Mashariki 

Dar es Salaam. Katika kuchochea uchumi wa mtu mmojammoja na Taifa kupitia uwekezaji, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imehimiza wananchi kuwekeza kupitia ununuzi wa hisa katika kampuni kubwa zilizopo Afrika Mashariki.

Miongoni mwa kampuni hizo 14, ni KCB, Safaricom, CRDB, NMB, Bank of Kigali, Vodacom, Tanga Cement, Twiga Cement, MTN Uganda ambazo zimeingia ubia na mfuko wa pamoja wa uwekezaji wenye hisa za kampuni hizo uitwao iTrust EAC Large Cap ETF.

Imeelezwa mwananchi ambaye ni mwekezaji wa kawaida akinunua hisa kwenye mfuko huo wenye jumla ya kampuni hizo ni sawa na kuwekeza katika kampuni hizo zilizopo Uganda, Kenya Tanzania na Rwanda ikiwa ni sawa na mtawanyiko wa uwekezaji.

Mfuko huo wa uwekezaji wa iTrust East Africa Community Large Cap Exchange Traded Fund (ETF) umeorodheshwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), kufuatia mwitikio wa wawekezaji ulioufanya uzidi lengo la ukusanyaji wa fedha kwa asilimia 540 ishara inayothibitisha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika soko ya mitaji ya Tanzania.

Akizungumza leo Jumatano Januari 28, 2026 katika hafla ya kuorodheshwa kwa mfuko huo wa uwekezaji wa pamoja wa kampuni ya itrust finance limited katika soko la hisa la DSE, Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama amesema mauzo ya vipande vya mfuko huo yamepata mafanikio ya asilimia 540, ambapo kiasi cha Sh54 bilioni kimepatikana, ikilinganishwa na lengo la Sh10 bilioni.

“Huu ni mfuko wa kwanza wa kikanda wa kampuni kubwa (large-cap) Afrika Mashariki kuorodheshwa Tanzania, jambo linaloashiria mafanikio makubwa kwa iTrust Finance Limited na maendeleo ya masoko ya mitaji katika ukanda huu,” amesema Mkama.

Amesema mfuko huo unasimamiwa na iTrust Finance Limited, huku Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikihudumu kama msimamizi wa mali (custodian), na uko chini ya uangalizi na idhini ya CMSA.

Amehimiza wananchi kuwekeza huku akisema CMSA itaendelea kuunga mkono bidhaa bunifu zitakazoimarisha masoko ya mitaji na kukuza maendeleo ya uchumi jumuishi.

Akitaja miongoni mwa sababu za kukua kwa uwekezaji amesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, ambapo wawekezaji wamepata fursa ya kuwekeza kwenye Mfuko huu kwa kutumia mfumo wa mauzo wa Kieletroniki. Mfumo huu umewezesha ushiriki wa wawekezaji wengi, mijini, vijijini na diaspora.

Pamoja na elimu ya uwekezaji inayotolewa kwa umma na CMSA kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya fedha, kuhusu fursa na faida zinazopatikana katika uwekezaji kwenye soko ya mitaji.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance, Faiz Arab, amesema mfuko huo ulianza rasmi kuwekeza Januari 20 na tayari umeonesha matokeo chanya, ukiwa umeongeza thamani ya mali halisi (NAV) kwa asilimia 6.49 ndani ya wiki yake ya kwanza ya uendeshaji kutoka Sh1,000 hadi Sh1,064.

 “Uorodheshaji huu unaashiria debut ya kwanza ya masoko ya mitaji kwa mwaka 2026, na pia unaufanya kuwa ETF ya pili kuorodheshwa katika DSE,” amesema Arab.

Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa DSE, Emmanuel Nyalali, amesema uorodheshaji wa iTrust EAC Large Cap ETF unaimarisha jitihada zinazoendelea za kuboresha utofauti wa bidhaa za uwekezaji, kuongeza ukwasi wa soko na kupanua wigo wa ushiriki wa wawekezaji.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabu, ofisa wa benki hiyo, Elvis Ndunguru amesema mafanikio ya usajili yanaakisi imani ya wawekezaji katika mfumo wa udhibiti na taasisi za masoko ya mitaji nchini.

“NBC, kama msimamizi wa mali wa mfuko huu, inafanya kazi kwa karibu na Absa Kenya na Absa Uganda kama wasimamizi wenza (sub-custodians) ili kuuwezesha muundo wa uwekezaji wa kikanda wa ETF hii,” amesema.