Moja ya masuala makubwa yanayosubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania ni kuanza kwa mchakato wa katiba mpya ndani ya siku 100 za kwanza za awamu hii ya uongozi, kama alivyoahidi Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13.
Hoja ya katiba mpya pia imeainishwa wazi katika Dira ya Taifa ya Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), jambo linaloonesha uzito na umuhimu wake kwa mustakabali wa taifa.
Katiba ni nyenzo kuu katika ujenzi wa taifa lolote, kwa sababu ndiyo mkataba wa msingi kati ya watawala na watawaliwa.
Katiba inapaswa kuwa mali ya wananchi, ikiweka mwelekeo wa namna wanavyotaka kuongozwa na kuongoza. Wananchi ndiyo watawaliwa, kwa mantiki hiyo, katiba halisi inapaswa kutungwa kwa ushiriki wao wa moja kwa moja.
Ukisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, maneno ya mwanzo yanasema: ‘Sisi Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.’
Kauli hii inaonesha kuwa katiba ilitungwa kwa niaba ya wananchi kupitia Bunge Maalum la Katiba. Hata hivyo, uhalisia unaonesha kuwa Bunge hilo halikuwa Bunge Maalum la Katiba kwa maana ya uwakilishi mpana wa wananchi, bali lilikuwa Bunge la chama kimoja cha CCM lililojigeuza kuwa Bunge la Katiba na kupitisha Katiba ya chama hicho kuwa Katiba ya nchi.
Kwa muktadha huo, Watanzania hawajawahi kuwa na Katiba yao iliyotungwa kwa ushiriki wa wananchi.
Hivyo basi, wazo la katiba mpya chini ya uongozi wa Rais Samia ni fursa adhimu kwa Watanzania kupata katiba yao ya kwanza ya wananchi. Ni wajibu wa kila Mtanzania kuichangamkia fursa hii kwa dhati, hasa ikizingatiwa kuwa mchakato huo umo katika Dira ya Taifa na Ilani ya CCM. Rais Samia anabeba nafasi ya kipekee ya kuwaongoza Watanzania kuelekea kupata Katiba inayotokana na sauti ya wananchi wenyewe.
Lengo la uchambuzi huu unaohusu katiba ni kutoa elimu kwa umma kuhusu Katiba, sheria, haki na wajibu.
Kwa kuwa mwaka huu ni mwanzo wa mchakato mwingine wa katiba mpya baada ya mchakato wa Katiba ya Warioba kusimama njiani, ni muhimu kutambua upungufu wa Katiba iliyopo ili yasijirudie. Wananchi wakielimishwa kuhusu katiba, watakuwa na uwezo wa kutoa maoni yenye tija juu ya aina ya katiba wanayoitaka.
Hakuna jambo lililo muhimu kwa taifa kuliko katiba. Ndiyo msingi wa utawala, haki, wajibu na mshikamano wa kitaifa.
Ndani ya Dira ya Taifa ya 2025/2050 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025/2030, suala la katiba mpya limepewa kipaumbele.
Rais Samia aliahidi kuanza mchakato huu ndani ya siku 100 za kwanza, jambo linaloipa katiba uzito unaostahili.
Kwa mujibu wa wataalamu wa sheria duniani kote, katiba inapaswa kupitiwa mara kwa mara ili iendane na mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Kwa ukweli, Katiba ya sasa ya Tanzania imepitwa na wakati kitambo, na kama marekebisho ya msingi yangefanyika mapema, baadhi ya matukio makubwa yaliyotokea yangeweza kuepukika.
Kwa mtazamo wa kihistoria, Katiba ya kwanza ya Tanganyika ya mwaka 1961 ilikuwa ya Uhuru iliyotungwa nchini Uingereza bila ushiriki wa Mtanzania yeyote.
Katiba ya pili ya mwaka 1962, ya Jamhuri, ilitungwa na wabunge wa TANU pekee bila kuwashirikisha wananchi.
Katiba ya tatu ya mwaka 1964, ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, nayo ilitungwa bila ushiriki wa wananchi, ikiridhiwa na Bunge la Tanganyika pekee licha ya madai ya ridhaa ya Zanzibar bila kumbukumbu za maandishi.
Katiba hiyo ya Muungano ilikusudiwa kuwa ya muda, ikiweka msingi wa kuandaliwa kwa Katiba ya kudumu kupitia Tume ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba chini ya uongozi wa Rashid Mfaume Kawawa.
Wiki ijayo, tutajadili Katiba ya Mpito ya mwaka 1965 na Katiba ya kudumu ya mwaka 1977.