Kocha KMC FC akiri mambo magumu Ligi Kuu

BAADA ya sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Coastal Union, kocha Mkuu wa KMC, Mohammed Abdallah ‘Bares’ amesema kikosi chake bado kina hali ngumu, hivyo kinaendelea kupambana kujiondoa mkiani huku akikiri ana kazi kubwa ya kufanya.

Bares ameambulia pointi moja ya kwanza tangu amekabidhiwa kikosi hicho akichukua mikoba ya Mbrazili, Marcio Maximo, ambapo alianza na kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya TRA United, kabla ya juzi kutoka sare na Coastal Union.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bares amesema ana kibarua kigumu kuipambania timu hiyo kuondoka kwenye nafasi mbaya iliyopo na kupata nafasi ya kucheza ligi msimu ujao kutokana na timu kutokuwa katika hali nzuri ya ushindani.

BAR 01


“Bado tunajitafuta, kwa sasa tunajenga misingi mizuri ya ushindani, kikosi kinajipambania kuhakikisha kinafanya vizuri. Ni kweli tupo mkiani, presha ni kubwa kuanzia uongozi, wachezaji hadi benchi la ufundi, hivyo tunaendelea kupambana.

“Pointi hii moja hayakuwa malengo yetu, tulitamani kupata zote tatu lakini kosa moja tulilolifanya tukiwa mbele kwa bao moja ugenini limetunyima nafasi ya kuondoka na ushindi, tutaendelea kupambana ili tuweze kufikia malengo,” amesema Bares.

BAR 02


Bares amesema baada ya kufanya maboresho dirisha dogo la usajili, wachezaji wapya wanaendelea kuzoea kidogo kidogo, hivyo anaamini wakiingia kwenye mfumo watakuwa chachu ya ushindani kikosini kwa kuisaidia timu kutoka mkiani.

“Ligi ni ngumu, mbinu bora na timu iliyokamilika katika uwekezaji kuanzia usajili wa wachezaji bora ndio itakayokusanya pointi nyingi na sisi tunapambana tuweze kufikia malengo ya kuendelea kuwepo katika ligi msimu ujao,” amesema.

KMC ipo nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi tano baada ya kucheza mechi 11, ikishinda moja, sare mbili na kupoteza nane.