Mohamed Bouazizi, alikuwa kijana mdogo nchini Tunisia. Familia yake maskini, kwa hiyo ikawa inamtegemea yeye. Akawa anajishughulisha na umachinga. Askari nao wakawa wakikutana naye wanamnyang’anya bidhaa zake.
Baada ya kunyanyaswa sana na askari, Bouazizi alichoka, akaona ananynyasika kwa kiwango cha kumfika mwisho. Desemba 17, 2010, Bouazizi alijimwagia petroli na kujilipua kisha akazunguka mitaani akiteketea kwa moto, kufikisha hasira zake za kunyng’anywa bidhaa zake na polisi. Januari 4, 2011, Bouazizi alifariki dunia.
Kitendo cha Bouazizi kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia ambao waliingia mitaani kwa siku 10 kulazimisha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Zine El Abidine Ben Ali kung’oka. Na kweli, Januari 14, 2011, Ben Ali aliachia ngazi baada ya kuwepo madarakani kwa miaka 23. Na ikiwa ni siku ya 10 tangu Bouazizi alipofariki dunia.
Muone Micah Xavier Johnson wa Mesquite, Texas, aliyeua askari watano Dallas, Texas Julai, 2016. Polisi walichunguza na kukuta hakuwa na rekodi yoyote ya uhalifu. Nini ambacho kilisababisha raia mwema aue askari? Jibu ni hasira kuona ndugu zake Waamerika weusi wanauawa kikatili, akaona naye aue askari wa Kizungu. Ni ugaidi!
Nyuma ya simulizi za magaidi wengi, unakuta kisa cha kuona wanaonewa. Osama bin Laden alianza vita na Marekani baada ya kuona Wapalestina na Walebanon wakikandamizwa na kunyanyaswa kama watu wasio na ardhi. Mwisho Osama akautikisa ulimwengu. Ni kwamba akili ya ugaidi ikishamwingia mtu, anaweza kuwa na matokeo ya aina yoyote.
Miaka 12 iliyopita nikiwa ofisini usiku, alinifuata mbunge mmoja wa zamani (alikuwa mbunge wakati huo), aliyekuwa na nakala za ushindi wake wa kisheria dhidi ya tuhuma alizokuwa anatupiwa kuhusu kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.
Akiwa mwenye furaha baada ya ushindi huo, aliniambia: “Hizi tuhuma za dawa za kulevya ni za kisiasa tu. Mbaya zaidi nawajua wanaonizushia. Ilifikia wakati nilitaka niwafuate nimpige risasi mmoja baada ya mwingine, nikishawamaliza na mimi nijiue au hata nikikamatwa na kufungwa ingewa sawa, muhimu ilikuwa kuwamaliza.”
Kutoka Bouazizi, Xavier, Osama, mpaka mbunge niliyemhifadhi jina. Halafu pitia nadharia ya Sagan Standard, inayoeleza kuwa “extraordinary claims require extraordinary evidence” – “Tuhuma zisizo za kawaida huhitaji ushahidi usio wa kawaida.”
Sagan Standard ni nadharia iliyotokana na mwanasayansi, Carl Sagan, ambaye aliandika kwenye tamthiliya ya Cosmos, kuwa madai au tuhuma zozote zisizo za kawaida, huhitaji ushahidi ambao unakuwa si wa kawaida. Nadharia hiyo kwa kifupi huitwa ECREE.
Kisha, tuitazame Tume ya Uchunguzi wa Kadhia ya Oktoba 29, 2025. Mwenyekiti na makamishna wake. Yaliyojiri wakati wa kadhia, kabla na yanayoendelea baada yake. Baada ya hapo utabaini upungufu. Tume inahitaji kuongezewa wataalamu.
Tume imesheheni wabobevu wa masuala ya sheria, haki, intelijensia na diplomasia. Mwenyejikiti, Mohamed Chande Othman na Makamu Mwenyekiti, Prof Ibrahim Juma, ni majaji wakuu wastaafu. Ukiongeza na IGP mstaafu, Said Mwema, ni eneo lilelile la sheria, haki, usalama wa raia na intelijensia.
Kuna wanadiplomasia, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Ombeni Sefue, Balozi David Kipya, Dk Stergomena Tax, Balozi Radhia Msuya, na Balozi Paul Meela, ambaye kijeshi ni Luteni Jenerali mstaafu.
Mambo ya Oktoba 29 yana pande mbili, mosi ni ushawishi wa mitandao. Kuna watu walishinda na kukesha mitandaoni wakishawishi vijana kuingia mitaani. Hao waliokuwa wakiwashawishi wenzao, hawaishi Tanzania, na hawakushiriki moja kwa moja.
Waliokuwa wakishawishi watu kuingia mitaani, hakuna miongoni mwao ambaye msiba umeripotiwa kwenye familia yake, ndugu kujeruhiwa au kukamatwa na kushikiliwa mahabusu. Je, hawana ndugu, au waliwatahadharisha ndugu zao kutoshiriki maandamano?
Unaweza kujiuliza pia, unashawishika vipi kwenye ushawishi ambao anayekushawishi yeye hashawishiki? Mmoja wa waliokuwa wakishawishi watu mitandaoni alikuwa akitoa taarifa nyeti bila ushahidi wala uthibitisho. Pamoja na hivyo, aliongeza wafuasi, maana yake aliaminika.
Ulitolewa ushawishi kuwa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), lilikuwa tayari kwa mapinduzi ya Oktoba 29. JWTZ, walitokeza kueleza msimamo wao kuhusu viapo vyao na utii kwa Amiri Jeshi Mkuu. Pamoja na hivyo, bado aliyetoa taarifa za jeshi kuhusu mapinduzi, aliaminika, akaongeza ufuasi.
Hili ndilo eneo ambalo naona Tume ya Uchunguzi inahitaji wataalam zaidi. Kwanza kabisa, Tume ilihitaji tangu awali, na inahitaji hata sasa wataalamu wa saikolojia. Mmoja wa wataalamu hao lazima awe mbobevu wa saikolojia ya mitandao na intaneti (cyberpsychologist).
Rais Samia Suluhu Hassan, alisema kuna watu waliingia barabarani Oktoba 29, 2025, kwa kufuata mkumbo. Ni sahihi. Tatizo la kufuata mkumbo linagusa saikolojia, vilevile sayansi ya jamii. Tume ulihitaji mwanasaikolojia ambaye ni mbobevu wa sayansi ya jamii.
Uhusiano wa kijamii ni sosholojia. Kuna ombwe kiasi gani baina ya mamlaka na wananchi? Tume ya Uchunguzi ingekuwa na safu nzuri kama ingekuwa na mwanasosholojia ambaye angeweza kuwasikiliza watu, ama watoa maoni, mashuhuda au waathirika, na kuwasaidia makamishna wenzake kujenga muktadha bora wa kijamii.
Lazima mambo yatazamwe ndani zaidi, tena kwa kina, kuliko kutafsiri matokeo. Ghasia za Oktoba 29 ni matokeo. Je, vifuani watu wana nini? Vichwani wanawaza nini? Kwa nini wafuate mkumbo? Je, walifuata mkumbo au walipata sababu ya kutimiza yaliyokuwa ndani ya vifua vyao?
Ni kweli, walishawishiwa, lakini ilikuwaje wakashawishika? Kuna uongo mwingi ulihubiriwa, kwa nini watu watekwe na uongo? Wataalamu wa saikolojia na sosholojia wangeweza kuisaidia Tume, vilevile wabobevu wa sera za elimu. Elimu ya Tanzania inasaidia kiasi gani watu kuhoji na kutafsiri kila wanachoambiwa?
Uchambuzi wa masuala ya haki ni muhimu. Uzuri Tume ina wabobevu. Wakati unajiuliza ilikuwaje matukio ya Oktoba 29 yakaanzia Kimara, wengine wana hitimisho tayari kwamba ni eneo ambalo watu wana vinyongo, walivunjiwa nyumba bila fidia, kupisha upanuzi wa barabara miaka nane iliyopita.
Kuhusu wageni kujiingiza au kushiriki kadhia ya Oktoba 29, naamini Tume ina wataalamu wa kulijengea muktadha mzuri hilo, lakini vema kutazama mifumo ya utoaji haki, inawaumiza kiasi gani watu? Rushwa, kila nyanja.
Miaka minne iliyopita, kuna kijana anayeitwa Hamza Mohammed, aliishangaza dunia kwa kuwafyatulia risasi polisi. Tukio la Hamza halikuwa la kawaida. Lilihitaji umakini na uangalifu wa hali ya juu kulifuatilia. Tiba ya jamii ni kutibu nyufa, siyo kufunika. Tume ya Uchunguzi iisaidie nchi kuepuka kutengeneza magaidi dhidi ya serikali yao