Mambo matano ndani ya Agenda 2030 ya NMB

Dar es Salaam. Benki ya NMB imezindua mpango mkakati wa miaka mitano kuanzia 2026 hadi 2030, unaojulikana kama Agenda 2030, ambao umeweka mkazo katika maeneo matano makuu, ikiwemo kuboresha huduma kwa wateja, kuimarisha mabadiliko ya kidijitali, matumizi ya kimkakati ya data na kufadhili sekta muhimu za uchumi.

Uzinduzi wa Agenda 2030 umefanyika leo Januari 28, 2026, sambamba na benki hiyo kutangaza mafanikio ya mpango mkakati uliopita (MTP 2025), uliomalizika kwa kuvunja rekodi ya kifedha kwa kupata faida ya Sh1.1 trilioni kwa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema katika kipindi cha utekelezaji wa mpango wa miaka mitano uliopita, benki hiyo imeendelea kuimarisha utendaji wake kifedha na mchango wake katika uchumi wa taifa.

Amesema katika mwaka 2025 pekee, faida baada ya kodi ilifikia Sh750 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 16 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, huku mapato ya jumla yakifikia Sh1.82 trilioni na mali zote za benki kufikia thamani ya Sh17.2 trilioni.

“Kwa kipindi chote cha utekelezaji wa MTP 2025, NMB imepata matokeo madhubuti, yaliyojumuisha utendaji imara wa kifedha na mchango mpana katika kuchochea na kuwezesha shughuli za kiuchumi,” amesema Zaipuna na kufafanua.

Amesema katika kipindi hicho cha miaka mitano, benki ilizalisha faida ya Sh2.7 trilioni, huku mikopo yote iliyotolewa ilikuwa na thamani ya zaidi ya Sh27.6 trilioni, wakati amana za wateja zilifikia Sh12.4 trilioni, huku akaunti za wateja zikiongezeka hadi kufikia milioni 9.9.

Zaipuna amesema Agenda 2030 inalenga kupanua wigo wa shughuli za NMB nje ya huduma za kawaida za kibenki, sambamba na kupanua uwepo wa benki hiyo nje ya mipaka ya Tanzania.

“Mpango mkakati huu mpya umejengwa juu ya mafanikio yaliyopatikana, na unaweka dira ya ukuaji endelevu unaoongozwa na mteja, teknolojia na tija ya kiutendaji,” amesema Zaipuna katika hafla iliyokwenda sanjari na uzinduzi wa matawi ya benki hiyo yanayotembea kwa ajili ya huduma vijijini.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, ameipongeza bodi ya wakurugenzi na wafanyakazi wa NMB kwa mafanikio yaliyopatikana katika mpango ulioisha, akisema benki hiyo imeendelea kuyaishi maono ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mheshimiwa Rais anawasubiri kwa hamu kwenye gawio lake Juni mwaka huu. Kwa mafanikio haya, nina uhakika anatamani sana kukutana nanyi. Mimi nilitumwa niwapongeze na hapa niseme tu, na kuwashukuru sana sio tu kwa mafanikio makubwa mliyopata, bali kwa kuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa uchumi endelevu wa nchi yetu,” amesema Mchechu.

Mchechu amesema Serikali inaitazama NMB kwa jicho la karibu, huku akiahidi kuwa watasimama imara katika kuhakikisha benki hiyo inakuwa na bodi ya wakurugenzi iliyo imara ili kuendeleza mafanikio hayo ya sasa kwa miaka kadhaa ijayo.

“Kama mwanahisa wa NMB aliyeshika hisa za Serikali, nayazungumza haya kwa kina na ndio maagizo niliyonayo, fanyeni kazi, leteni uzalishaji wenye tija, onesheni mfano kwa wengine na tutasimama nanyi katika kila hali, ingawa tunapenda mtuongoze kwenye raha,” amesisitiza Mchechu.