Mambo matatu yaliyombeba Profesa Mukandala kupewa tuzo

Dar es Salaam. Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili (Chalufakita) kimempa tuzo Profesa Rwekaza Mukandala, mhadhiri na aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kwa mchango wake mkubwa katika kukuza na kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Tuzo hiyo imetolewa leo Januari 28, 2025 jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 tangu chama hicho kuanza shughuli zake baada ya kusajiliwa rasmi mwaka 2016.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Chalufakita, Dk Mussa Hans amesema tuzo hiyo imetolewa kutokana na mchango wa Profesa Mukandala katika kuendeleza taaluma na matumizi ya Kiswahili, hususan wakati wa uongozi wake akiwa makamu mkuu wa UDSM.

Amesema miongoni mwa hatua muhimu alizosimamia ni kuanzishwa kwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili baada ya kuunganisha taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili na idara ya Kiswahili. Taasisi hiyo ilipewa hadhi ya kuwa na idara mbili ambazo ni idara ya lugha ya Kiswahili na isimu pamoja na idara ya fasihi, mawasiliano na uchapishaji, zote zikijikita katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili.

“Hali hii ilifanya UDSM kuwa chuo cha kwanza duniani kuwa na idara mbili zote zikisimamia maendeleo ya lugha ya Kiswahili. Tunatambua pia kuwa kwa sasa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar nacho kina idara mbili zinazojihusisha na taaluma ya Kiswahili,” amesema Dk Hans.

Mwenyekiti wa Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili (CHALUFAKITA),Mussa Hans akimkabidhi tuzo Mhadhiri na aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala leo Januari 28,2026 jijini Dar es Salaam.



Ameongeza kuwa Profesa Mukandala pia alipitisha pendekezo la kurasimisha matumizi ya Kiswahili katika mikutano mbalimbali ya chuo, ikiwemo Baraza la Chuo, hatua iliyochangia kukuza matumizi ya lugha hiyo katika ngazi za juu za kitaasisi.

Sababu nyingine ni mhadhara alioutoa Mei 21, 2024 kwa lugha ya Kiswahili, jambo lililomfanya kuwa mwanazuoni wa kwanza duniani kutoa mhadhara huo kwa Kiswahili ilhali si mtaalamu wa lugha hiyo.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Profesa Mukandala ameishukuru Chalufakita kwa kutambua mchango wake, akisema uzalendo na mapenzi yake kwa lugha ya Kiswahili ndivyo vilivyomsukuma kuchukua hatua hizo.

Amesema aliamini kuwa matumizi ya Kiswahili katika ngazi mbalimbali za chuo, ikiwemo Baraza la Chuo, yangesaidia kuikuza lugha hiyo kwa kuitumia mara kwa mara. Ameongeza kuwa alitoa mhadhara wake wa uzinduzi wa uprofesa kwa Kiswahili ili ueleweke kwa wananchi wengi zaidi, hasa kwa kuwa mada aliyowasilisha iligusa jamii moja kwa moja.

“Ajali ya Mv Bukoba iliwagusa Watanzania wengi. Bado kuna maswali mengi, hivyo nikaona ni vyema kuwasilisha kwa Kiswahili ili wengi waelewe, tofauti na kama ningetumia Kiingereza,” amesema.

Akiendelea, Profesa Mukandala amesema hoja kwamba vyuo vikuu haviwaandai vijana kukabiliana na soko la ajira inaweza kushughulikiwa kwa kuimarisha matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia, akieleza kuwa vijana wengi wanaelewa zaidi Kiswahili kuliko Kiingereza.

“Ni wakati sasa tuelekeze nguvu zetu katika lugha ya kufundishia kama sehemu ya kukabiliana na changamoto hiyo,” amesema.