WAKATI wachezaji wakiwa katika maandalizi ya kuanza kwa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) 2026, nyota wa mchezo nchini, Jimmy Brown, ametaja sababu zilizomfanya asicheze michuano hiyo msimu uliopita.
Mchezaji huyo aliyewahi kuchezea Kurasini Heat, ABC, UDSM Outsiders, JKT na Ukonga Kings amesema kutoshiriki kwake kulitokana na kutokubaliana na utaratibu wa malipo ulivyokuwa umeandaliwa na baadhi ya timu.
“Kuna timu ziliniahidi zitakuwa zikinilipa wakati ligi inaendelea. Mimi niliwakatalia, nikawaambia tuandikishiane kwanza mkataba,” amesema Brown aliyewahi kucheza nchini Singapore, Ufilipino na Malaysia.
Amesema katika mashindano ya BDL mwaka huu atacheza kutokana na baadhi ya timu kuonyesha nia ya kumsajili.
Hata hivyo, nyota huyo hakupenda kutaja majina ya timu zilizomtaka kwa madai kuwa ni mapema mno.
Kuhusu maandalizi ya ligi hiyo, amesema amekuwa akifanya mazoezi ya kukimbia katika uwanja wa mpira wa miguu eneo la Kurasini, na nyakati za jioni akifanya hivyo kwenye Uwanja wa Bandari uliopo Kurasini jijini humo.
Akizungumzia wachezaji wa kigeni, amesema wameongeza ushindani kwa wachezaji wazawa kupambana ili kuonyesha uwezo na kuing’arisha ligi hiyo.
“Katika ligi ya mwaka huu ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa kutokana na timu kuonekana kujipanga kufanya usajili mzuri,” amesema Brown.
Nyota huyo anayecheza nafasi ya namba moja (power forward), ni mmoja wa wachezaji walioiwezesha UDSM Outsiders kucheza fainali dhidi ya JKT, mwaka juzi. Tarehe ya kuanza kwa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) itatangazwa baada ya kamati ya mashindano ya ligi hiyo kukutana na uongozi wa Chama cha Kikapu Mkoa Dar es Salaam (BD).