Ouma: Tunakwenda Kongo kuchukua pointi tatu

KIKOSI cha wachezaji 21 cha Singida Black Stars, kimeelekea nchini Congo kucheza mechi ya nne hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Otoho d’Oyo itakayofanyika Februari 1, 2026.

Kocha wa Singida Black Stars, David Ouma amesema wameenda kuandika historia nyingine kumataifa kwa kupata pointi tatu wakiwa ugenini.

Singida Black Stars inauendea mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda bao 1-0 nyumbani dhidi ya timu hiyo, wikiendi iliyopita zilipokutana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Ushindi huo umeiweka Singida katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne sawa na Stellenbosch iliyopo nafasi ya pili katika kundi C linaloongozwa na CR Belouizdad yenye pointi sita, huku Otoho d’Oyo ikishika mkia na pointi tatu.

OU 01


Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma amesema wanaenda kucheza mchezo mgumu ambao wao wameubeba kama fainali kwani umeshikilia uamuzi wa nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali ambayo ameitaja kuwa itabaki katika historia bora kwa klabu yao.

“Tunakwenda tukiwa na malengo sawa kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji, hivyo mipango ipo vizuri na kila mchezaji anatambua umuhimu wa mchezo huo ambao kwetu ni kama fainali kutokana na kubeba hatma yetu. Hatutarajii mchezo rahisi, tumejiandaa kwenda kushindana na kucheza kwa kumuheshimu mpinzani wetu ambaye pia anasaka pointi tatu kama ilivyo upande wetu, mbinu bora na kujitoa kwa wachezaji ndio kutatupa nafasi ya kusonga nafasi inayofuata,”  amesema Ouma.

OU 02


Ouma amesema anatambua ubora na upungufu wa wapinzani wao, hivyo amefanyia kazi katika uwanja wa mazoezi na ataendelea kusuka mbinu bora kabla ya mechi hiyo.

Wachezaji walioondoka ni Metacha Mnata, Amas Obasogie, Abdallah Said ‘Lanso’, Miraj Hassan, Kennedy Juma, Mukrim Issa, Abdulmalick Zakaria, Idd Khalid, Morice Chukwu na Khalid Aucho.

OU 03


Wengine ni Emmanuel Keyekeh, Idriss Diomande, Marouf Tchakei, Mtange Linda, Deus Kaseke, Lamine Jarjou, Mossi Nduwumwe, Joseph Guede, Harson Muaku, Mishamo Daudi na Elvis Rupia aliyetupia bao la ushindi mechi iliyopita.