Dar es Salaam. Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman amesisitiza kuwa ardhi ya nchi yake haitatumika kama kambi au njia ya kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Msimamo huo amemueleza Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian katika mazungumzo ya simu yaliyofanyika jana Jumanne usiku, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa vya RFI na DW.
Katika mazungumzo hayo, Mwanamfalme Mohammed bin Salman amebainisha kuwa Saudi Arabia inaheshimu mamlaka na uhuru wa Iran, akisisitiza kuwa nchi yake haitaruhusu anga au eneo lake kutumika kwa operesheni zozote za kijeshi dhidi ya Iran.
Kauli hiyo inatolewa wakati kukiwa na wasiwasi wa kuongezeka kwa mvutano wa kikanda, huku Marekani ikitajwa kuwa huenda ikaishambulia Iran baada ya kuituhumu serikali ya Tehran kuhusika na mauaji na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wa amani, katika maandamano ya kiraia yaliyofanyika mapema mwezi huu.
Katika kuashiria msimamo wake, Rais wa Marekani, Donald Trump alituma manowari kubwa ya kivita, USS Abraham Lincoln katika eneo la Mashariki ya Kati, hatua iliyozidisha taharuki kuhusu hatari ya mzozo wa kijeshi.
Hata hivyo, Rais Pezeshkian alilaani vikali vitisho vya Marekani wakati wa mazungumzo yake ya simu na Mwanamfalme wa Saudi Arabia, akisema kuwa vitisho hivyo vina lengo la kuvuruga usalama wa kikanda.
“Vitisho kama hivyo havichangii chochote katika kulinda amani, bali vinahatarisha zaidi usalama wa eneo,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Ofisi ya Rais Pezeshkian, Rais huyo alizungumzia pia shinikizo na uhasama wa hivi karibuni dhidi ya Iran, ikiwemo vikwazo vya kiuchumi na kile alichokitaja kuwa uingiliaji wa kigeni.
Taarifa hiyo ilinukuu Rais Pezeshkian akisema kuwa hatua hizo hazikufanikiwa kudhoofisha uthabiti wala mshikamano wa wananchi wa Iran, akisisitiza kuwa raia wa nchi hiyo wanaendelea kuwa makini na imara katika kulinda masilahi ya taifa lao.