Sh23.4 bilioni kuimarisha miradi ya umwagiliaji

Dodoma. Serikali imekabidhi vitendea kazi vyenye thamani ya Sh23.4 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji nchini, huku Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) ikipongezwa kwa mchango wake katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa.

Vitendea kazi hivyo ni pamoja na mitambo mikubwa 19 ya kuchimba visima vyenye uwezo wa kufikia kina cha mita 300 hadi 1,800, magari 17 ya kubeba vifaa na malighafi, trela mbili pamoja na pikipiki 23.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo Jumatano, Januari 28, 2026, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema hatua hiyo itaongeza kasi na ufanisi katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji kote nchini.

Amesema Serikali imeongeza bajeti ya maendeleo ya sekta ya umwagiliaji kutoka Sh46.5 bilioni mwaka wa fedha 2021/22 hadi Sh308.7 bilioni mwaka 2025/26, akisisitiza kuwa wizara itaendelea kusimamia na kufuatilia upatikanaji wa fedha ili miradi ikamilike kwa wakati. Aidha, ameiagiza bodi na watumishi wa NIRC kusimamia ipasavyo rasilimali hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa, amesema hafla hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Agosti 8, 2022, linalolenga kuimarisha sekta ya umwagiliaji nchini.

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo akizungumza katika hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) jijini Dodoma.



Ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita imekabidhi mitambo mikubwa 19 ya kuchimba visima, magari 16 ya kusaidia shughuli za uchimbaji, trela mbili na pikipiki 23. Ameongeza kuwa NIRC imepanga kuchimba visima 67,000 ndani ya kipindi cha miaka mitano, vitakavyohudumia eneo la hekta 16,000.

“Katika mwaka huu wa fedha pekee, visima 1,027 vimepangwa kuchimbwa, ambapo tayari visima 260 vimeshachimbwa kwa majaribio katika mikoa 12,” amesema Mndolwa.

Ameongeza kuwa tume imenunua pampu 1,000 kwa ajili ya kutoa maji katika vyanzo mbalimbali, zitakazogawiwa kwa makundi maalum ya wanawake na vijana. Kwa sasa, NIRC inaendelea kutekeleza miradi 146 ya umwagiliaji, ambapo 18 imekamilika na ipo tayari kukabidhiwa.

Mndolwa amesisitiza kuwa watumishi wa tume wako tayari kutekeleza majukumu yao na kwamba NIRC imejipanga kuongeza eneo linalomwagiliwa ili kufikia lengo la kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo (wa nne kutoka kulia) akikata utepe wa makabidhiano ya vitendea kazi kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Raymond Mndolwa na kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.



Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema kuwa asilimia 72 ya wakazi wa mkoa huo wanategemea kilimo, hivyo ujio wa vitendea kazi hivyo ni mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

Kwa upande wao, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile, pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga, wameipongeza Serikali na Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa unaofanywa katika kilimo cha umwagiliaji.