January 28, 2026 imekuwa siku ya huzuni kwa wadau na wapenzi wa soka Tanzania baada ya kuagwa na kuzikwa kwa mwili wa nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Manyika Sr.
Kuanzia asubuhi hadi jioni simanzi ilitawala katika nyuso za waliokusanyika kumuaga shujaa huyo aliyeacha kumbukumbu nzuri katika soka nchini.
Vilio na majonzi zaidi viliikumba nyumba ya marehemu iliyopo Malamba Mawili huko Mbezi jijini Dar es Salaa, saa tano asubuhi, mara baada ya mwili wake kuwasili.
Mazingira yaligubikwa na ukimya mzito uliokatizwa na vilio vya uchungu kutoka kwa ndugu, jamaa, marafiki, majirani, viongozi wa michezo pamoja na wachezaji wa zamani waliofika kutoa heshima zao za mwisho.
Mwili wa marehemu ulipokelewa na familia kisha kufanyika maombi mafupi ya awali nyumbani, kabla ya maandalizi ya ibada rasmi. Baadaye, ibada maalum ya kumuaga Manyika Sr ilifanyika mchana katika Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam Parokia ya Mt. Yohane wa Msalaba, Malamba Mawili, ikihudhuriwa na umati mkubwa wa waombolezaji waliokusanyika kumuombea na kumkumbuka kwa mema aliyoyatenda ndani na nje ya uwanja. Katika kipindi chote cha maombolezo, wachezaji wenzake wa zamani walionekana kuwa bega kwa bega na familia, wakitoa faraja. Miongoni mwao walikuwepo Sekilojo Chambua, Philip Alando, Ally Mayay pamoja na wachezaji na makocha wengine.
Baada ya kukamilika kwa ibada ya mchana, msafara ulielekea Makaburi ya Kinondoni, ambako Manyika Sr alipumzishwa katika makazi yake ya milele. Manyika Sr, aliyezaliwa Februari 19, 1972, alifariki dunia alfajiri ya Januari 26, 2026 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya St. Monica, Dar es Salaam, ambapo ameacha alama isiyofutika katika soka la Tanzania, kwanza kama kipa mahiri, baadaye kama kocha. Kabla ya umauti, alikuwa Kocha wa Makipa wa Namungo FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara.
Mwaka 2003, Manyika Sr aliiongoza Taifa Stars kutwaa ubingwa wa Kombe la Challenge (CECAFA), ushindi uliolipa taifa heshima ukanda huu wa Afrika Mashariki. Kabla ya hapo 1999 aliiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, na mwaka 1998, aliisaidia Yanga kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mafanikio yaliyobaki kuwa historia muhimu ya klabu hiyo.