Staa Ivory Coast amchambua winga mpya Simba

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wameendelea kuimarisha kikosi chao katika dirisha hili dogo la usajili kwa kumtambulisha winga, Alain Anicet Oura, ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu, lakini usajili huo umetajwa kuwa na pande mbili za kutazamwa.

Hii ni hatua inayofanya mashabiki wa Simba kuwa na matumaini mapya kwa kumuona winga huyo na wachezaji wengine wapya kama vile, Clatous Chama aliyerejea, Nickson Kibabage, Djibrilla Kassali, Libasse Gueye, Ismael Toure wakishirikiana na waliopo kuirejesha timu hiyo kwenye mstari. 

Oura ni nyota wa zamani wa Asec Mimosas, klabu maarufu huko Ivory Coast na staili yake ya kucheza anatajwa kama mchezaji msumbufu na anayeweza kubadili mwenendo wa mechi wakati wowote.

Winga huyo anasubiriwa kuonyesha uwezo wake kama alivyokuwa hapo zamani kabla ya kupata majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa takribani miezi minne hadi kufikia uamuzi wa klabu ya IF Gnistan kumuacha. Kama akifanikiwa katika hilo, Simba itakuwa imelamba dume, lakini ikiwa tofauti ikiwamo kuumia tena na kukaa nje muda mrefu, ni hasara kama ilivyowahi kuwa kwa Aubin Kramo na sasa Mohamed Bajaber.

SIMB 01


Nyota wa zamani huko Ivory Coast, Arsene Hobou ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha taifa hilo kilichoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) mwaka 1988, amethibitisha ubora wa mchezaji huyo aliyezaliwa Desemba 7, 1999.

“Nilimfurahia sana akiwa Asec. Ni mchezaji mzuri sana kwa sababu ni winga mwenye madhara, ni mzuri ana kwa ana (1 vs 1) pia anaweza kutumika kama namba 10. Nilidhani angefanikiwa Finland lakini majeraha yamemzuia. Sikusikia habari zake kwa muda mrefu hadi kuona Simba imemtambulisha,” amesema Hobou.

Hobou aliongeza kuwa, kurudi nyumbani Afrika si jambo baya kwa mchezaji kwani ni sehemu ya kujipanga upya.

“Simba ni klabu kubwa, yenye historia na mashabiki wengi Afrika Mashariki na inaweza kuwa sehemu ya hatua nyingine kubwa katika maisha yake ya mpira,” amesema.

Oura, ambaye hajacheza soka la ushindani kwa zaidi ya miezi minne na nusu kutokana na kusumbuliwa na majeraha, anajiunga na Simba akiwa na matumaini makubwa ya kurejea kwenye ubora wake.

Baada ya kujiunga na Gnistan ya Finland wakati huo akitokea Afrika Kusini ambako alizichezea Muaither SC na Stellenbosch, Oura alicheza mechi tano na kutoa asisti moja.

SIMB 02


Hata hivyo, Septemba 13, 2025, alipata majeraha ambayo ilibidi kufanyiwa upasuaji. Ingawa alikuwa akitarajiwa kurejea baada ya miezi miwili, hali yake ilikwenda tofauti na klabu ya Finland iliamua kuachana na winga huyo.

Kwa usajili huo, Simba inatajwa kulamba dume, lakini changamoto kubwa ni kuhakikisha anarejea kwenye kiwango chake bila ya kukumbana tena na majeraha kama ilivyokuwa kwa Mohammed Bajaber.

Usajili wa Oura pia unaashiria jinsi Simba wanavyojiandaa na maisha bila ya kumtegemea Elie Mpanzu ambaye kiwango chake kwa sasa kinaonekana kushuka chini ya makocha wanne tofauti.

Mpanzu alikuwa mchezaji muhimu katika eneo la ushambuliaji la Simba msimu uliopita, lakini baada ya kuondoka kwa kocha Fadlu Davids, Wanasimba bado hawajaona makali yake licha ya kufunga katika mechi iliyopita ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kwa upande wake, kocha wa Simba, Steve Barker ambaye aliwahi kufanya kazi na winga huyo wakati akiwa Stellenbosch msimu wa 2023/24, amesema kuwa usajili huu ni sehemu ya mkakati wa kuboresha kikosi hicho kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine.

“Tunataka kuhakikisha kikosi kinaendana na malengo yetu ya kushindana kuanzia katika ligi, mashindano ya kimataifa na kuongeza kiwango cha wachezaji mmoja mmoja kila wakati,” amesema.

Oura pamoja na wachezaji wengine wapya kwenye kikosi cha Simba, wana kibarua kizito wikiendi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuhakikisha wanapindua meza katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis kwa kusaka ushindi wao wa kwanza hatua ya makundi.

Simba imeanza vibaya michuano hiyo ya kimataifa kwa kupoteza mechi tatu za kwanza katika kundi D na kuweka rekodi mbovu zaidi katika hatua ya makundi ya michuano hiyo tangu 2003.