Ulimwengu, Coastal ni suala la muda

UONGOZI wa Coastal Union uko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa aliyekuwa straika wa TP Mazembe ya DR Congo, Thomas Ulimwengu baada ya mazungumzo chanya kati ya kikosi hicho cha ‘Wagosi wa Kaya’ na kambi ya nyota huyo.

Taarifa kutoka Coastal Union zilizonaswa na Mwanaspoti zimedai mazungumzo yamefikia hatua nzuri kwa ajili ya mchezaji huyo kwenda kukitumikia kikosi hicho kwa mkataba wa miezi sita hadi mwisho wa msimu huu.

“Kuna kiasi cha fedha tulichokubaliana na tunaendelea kupambana kwa ajili ya kumuingizia kwenye akaunti yake ili aje kwa ajili ya kuendelea na mazoezi na wenzake, nadhani hakuna kitakachoharibika juu ya usajili wake,” kilisema chanzo hicho.

Nyota huyo aliyechezea timu za Soccer Akademia, Moro United, FC Vasby United, AFC Eskilstuna zote za Sweden, hakuwa na klabu yoyote ya ushindani tangu mara ya mwisho alipoachana na kikosi cha Fountain Gate, Julai 1, 2024.

Ulimwengu aliyecheza pia, TP Mazembe ya DR Congo, FK Sloboda Tuzla ya Bosnia and Herzegovina, Al-Hilal Omdurman ya Sudan na JS Saoura ya Algeria, ni pendekezo la Kocha wa Coastal Union, Mohamed Muya, anayetaka asajiliwe ili kuongeza nguvu.

Timu hiyo tayari imekamilisha usajili wa wachezaji watatu kipindi hiki cha dirisha dogo ambao ni Shiza Kichuya aliyecheza Simba na Namungo kisha msimu huu kuachana na JKT Tanzania, huku mwingine ni mshambuliaji, Abdulkarim Segeja aliyeondoka Tanzania Prisons.

Nyota mwingine aliyejiunga na kikosi hicho ni mshambuliaji, James Msuva, ambaye hakuwa na timu pia.