Ushindi wa Museveni wapingwa mahakamani | Mwananchi

Dar es Salaam. Katika hatua mpya ya mgogoro wa kisiasa ulioibuka tangu uchaguzi wa urais wa Uganda uliofanyika Januari 15, 2026, ushindi wa Rais Yoweri Museveni umeanza kutafunwa kisheria mbele ya Mahakama Kuu ya Uganda.

Hii imejiri tangu Januari 17, 2026, baada ya mgombea wa Urais Robert Kasibante, aliyeshika nafasi ya sita katika matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi kufungua pingamizi mahakamani dhidi ya ushindi huo, akisema uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kama ilivyotangazwa.

Kasibante, akizungumza katika maombi yake ya kesi, amesema mchakato mzima wa uchaguzi ulikuwa na dosari kubwa, ikiwemo matumizi ya vifaa vya utambuzi vya kisasa (Biometric Voter Verification Kits – BVVK) vilivyoshindwa kufanya kazi kwa kiwango kikubwa siku ya kura, hivyo kuathiri mchakato wa upigaji wa kura katika maeneo mengi.

Amedai zaidi tume haikutumia mfumo wenye uwazi wa kisheria wa kusajili na kutangaza matokeo, na pia kulikuwa na udhibiti wa mawasiliano ya umma ulioenda kinyume na taratibu, akisema uchaguzi huo umekosa uhalali kisheria.

“Mchakato mzima wa uchaguzi ulikuwa umetawaliwa na kasoro, na tunahitaji mahakama iweze kuchunguza kwa kina ili kulinda kura ya wananchi wa Uganda,” Kasibante amesema mbele ya Mahakama.

Pia anaomba Mahakama kuiagiza Tume ya Uchaguzi kutoa nyaraka na vifaa vyote vya uchaguzi ili kutumika kama ushahidi kamili wa kile anachokitaja kama kasoro zinazoathiri imani ya umma kuhusu uhalali wa matokeo hayo.

Kwa upande mwingine, Tume ya Uchaguzi ya Uganda kupitia Mwenyekiti wake, Jaji Simon Byabakama, imesisitiza uchaguzi uliendeshwa kwa mujibu wa katiba, sheria za uchaguzi na sheria nyingine zinazotumika, akisema madai ya Kasibante hayana ushahidi wa kutosha wa kuathiri matokeo ya uchaguzi.

Katika majibu yake mahakamani, Rais Museveni, kupitia timu yake ya mawakili, amewasilisha utetezi wake mbele ya Mahakama Kuu nchini humo akiomba kesi hiyo itupiliwe mbali kwakuwa haina mashiko ya kisheria.

Wakili aliyemwakilisha Museveni amesema  pingamizi hilo halina msingi wa kikatiba na ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai ya uvunjifu wa sheria unaoweza kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo, akisema uchaguzi ulifanyika kwa mujibu wa katiba na sheria zote zinazohitajika na kuwa masuala yaliyotajwa na Kasibante hayana nguvu ya kisheria.

Kiini cha mgogoro kipo hapa

Mgogoro huu wa kisiasa katika taifa hilo la Afrika Mashariki, umetokana na uchaguzi uliofanyika chini ya mazingira magumu, ikijumuisha kuzimwa kwa huduma za mtandao kitaifa,  na  udhibiti mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama uliolalamikiwa kulenga zaidi wapinzani wa kisiasa.

 Uchaguzi huo, ambao ulitangazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa Museveni alipata zaidi ya asilimia 71 ya kura dhidi ya Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine aliyepata asilimia 24.7, umeibua malalamiko mengi ya udanganyifu wa kura na udhibiti wa wapinzani, hatua ambazo wapinzani nchini humo wanaziita kuzuia ushindani wa haki.

Imeripotiwa pia kuzuka kwa ghasia, mateso na vifo kwa baadhi ya wafuasi wa upinzani na vifo kadhaa kufuatia tukio uchaguzi huo hali iliyokoleza joto la kisiasa na kuibua mijadala mikubwa kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini Uganda.

Hayo yalipelekea mpinzani mkuu wa Rais Museveni, Bobi Wine, kuyakimbia makazi yake baada ya kuripoti kuzingirwa na vikosi vya ulinzi na usalama na ameendelea kuwa mafichoni mpaka sasa licha ya vitisho kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Uganda, Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mtoto wa Rais Museveni.

Mzozo huo sasa unasubiriwa kupata hatima yake mahakamani, ambapo inasubiriwa kusikiliza hoja zote kwa kina kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho juu ya pingamizi lililowasilishwa na Robert Kasibante kupinga kisheria uchaguzi huo, hatua ambayo itaamua hatima ya ushindi wa Museveni na kutafsiri demokrasia ya Uganda.