Yanga yarejea kileleni, Depu aendelea kutupia

KIKOSI cha Yanga, kimeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo Jumanne Januari 27, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo ulioirudisha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kufikisha pointi 22, umetokana na mabao mawili ya Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ na moja la Prince Dube.

Mechi hiyo ya nane kwa Yanga na 11 upande wa Dodoma Jiji, kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Dodoma Jiji ilianza kufunga dakika ya 40 baada ya Nelson Munganga kumpenyezea pasi Edgar William na kumchambua kipa wa Yanga, Djigui Diarra, kisha mpira ukajaa wavuni.

Kuingia kwa bao hilo, kukaiamsha Yanga na kulisakama lango la Dodoma Jiji ambapo Depu akasawazisha dakika ya 45+5 kwa mkwaju wa penati uliotokana na Frank Assinki kuangushwa eneo la hatari.

Kipindi cha pili dakika ya 60, Depu akaongeza bao la pili akiunganisha kwa kichwa krosi ya Duke Abuya. Hilo ni bao lake la tatu katika mechi mbili za Ligi Kuu msimu huu baada ya kutua Yanga usajili wa dirisha dogo msimu huu.

Dube alihitimisha ushindi huo kwa kufunga bao la tatu dakika ya 66, akitumia mwanya wa mabeki wa Dodoma Jiji kushindwa kuokoa hatari langoni mwao.

Dube ambaye msimu uliopita alifunga mabao 13 katika Ligi Kuu Bara, hili kwake ni bao la nne msimu huu.

Pointi 22 zimeifanya Yanga kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi saba ikiishusha JKT Tanzania iliyokusanya 21 katika mechi 12.

Januari 19, 2026, Yanga ilikaa kileleni baada ya ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa, lakini ikaja kushushwa na JKT Tanzania iliyokuja kuichapa Singida Black Stars bao 1-0, Januari 20, 2026.

Ukiweka kando hilo la Yanga kukaa kileleni, timu hiyo sasa imepata ushindi dhidi ya Dodoma Jiji mara 10 katika Ligi Kuu Bara tangu zianze kukutana kati ya mechi 11 zilizochezwa baina yao, huku moja ikiisha kwa suluhu. Dodoma Jiji haijawahi kuifunga Yanga.

Katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wenyeji Coastal Union walitoka nyuma na kuweka mzani sawa dhidi ya KMC, mechi ikiisha 1-1.

Jammy Simba alianza kutikisa nyavu za Coastal Union dakika ya 45+4 na kuipeleka KMC mapumziko ikiongoza 1-0.

Mapema kipindi cha pili dakika ya 47, Gradi Lassa akaisawazishia Coastal Union na kuitoa kwenye aibu ya kupoteza nyumbani.

Sare hiyo imelifanya benchi jipya la ufundi la KMC chini ya kocha Abdallah Mohamed ‘Bares’ kuambulia pointi ya kwanza tangu kuanza kazi baada ya awali kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya TRA United.

Hata hivyo, matokeo hayo si mazuri kwa KMC kwani bado ipo mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi 11, ikishinda moja, sare mbili na kupoteza nane.

Coastal Union sare hiyo imeifanya kufikisha pointi 10 na kupanda nafasi mbili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kutoka ya 13 hadi 11 na kuzishusha Dodoma Jiji (pointi 10 ikizidiwa tofauti ya mabao) na Singida Black Stars (9).