ACT-Wazalendo wakwama tena kesi 14 za uchaguzi Zanzibar

Arusha. Chama cha ACT-Wazalendo kimeendelea kukumbwa na pigo la kisheria baada ya Mahakama Kuu ya Zanzibar kutupilia mbali kesi nyingine 14 zilizokuwa zimewasilishwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge katika majimbo ya Pemba.

Uamuzi huo umefanya idadi ya kesi za kupinga matokeo ya ubunge Zanzibar kufikia 33, kufuatia kesi nyingine 19 zilizotupwa juzi na mahakama.

Kesi 14 zilizofutwa Pemba zilihusisha majimbo ya Wete, Gando, Kojani, Micheweni, Konde, Wingwi, Ole, Ziwani, Wawi, Chake Chake, Chonga, Kiwani, Chambani na Mkoani.

Mahakama Kuu ya Zanzibar imezitupilia mbali kesi hizo za waliokuwa wagombea ubunge wa ACT-Wazalendo baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililodai kuwa haina mamlaka ya kusikiliza mashauri yanayotokana na uchaguzi wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uamuzi huo ulitolewa jana, Januari 28, 2026, na Jaji Haji Suleiman Khamis, aliyekuwa akisikiliza mashauri hayo.

Hatua hiyo imefuatia uamuzi wa juzi, Januari 27, 2026, ambapo mahakama hiyo ilitupilia mbali kesi nyingine 19 za Unguja, baada ya kukubaliana na hoja kwamba Mahakama Kuu ya Zanzibar haina mamlaka ya kusikiliza mashauri yanayotokana na uchaguzi wa wabunge wa Tanzania.

Katika uamuzi wa sasa, walalamikaji walikuwa Mohamed Said Issa na wenzake 13, waliowafungulia mashauri wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo hayo 14 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (AG).

Katika mashauri hayo, Mohamed na wenzake waliwasilisha maombi ya kuondolewa sharti la kuweka dhamana ya gharama za uchaguzi katika majimbo husika. Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliwasilisha pingamizi la awali, ukipinga mamlaka ya mahakama hiyo kusikiliza maombi hayo.

Msingi wa uamuzi wa Mahakama kuhusu maombi ya sasa yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, Masajala ya Pemba, yanafanana na uamuzi wa Januari 27, 2026, na kuwa pingamizi la mamlaka lililoamuliwa hapo ni sawa na lililowasilishwa katika maombi ya sasa.

Jaji Haji Suleiman Khamis katika uamuzi wake amesema Mahakama imezingatia mawasilisho yaliyotolewa na kuchambua aina ya maombi pamoja na unafuu uliokuwa ukiombwa.

Amesema ni misingi ya kisheria iliyothibitika kuwa mahakama inaweza kuchukua taarifa ya kimahakama kuhusu maamuzi yaliyotolewa na mahakama zenye mamlaka husika, akisisitiza kuwa utekelezaji wa kanuni ya stare decisis hauzuiliwi na eneo la kijiografia la masijala, hivyo hauondoi nguvu ya kisheria ya uamuzi husika.

Jaji Khamis ameongeza kuwa uamuzi uliotolewa juzi ulihusu moja kwa moja suala la mamlaka ya usikilizaji, ambalo pia limeibuka katika maombi ya sasa.

Ameeleza kwa kuwa maombi yote ya awali na ya sasa yaliwasilishwa katika masijala tofauti ambazo ni sehemu ya Mahakama moja na zinazoongozwa na sheria na kanuni zinazofanana, hakuna msingi wa kisheria wa kurudia kusikiliza hoja iliyokwishaamuliwa.

“Kurudia kusikiliza hoja ambayo tayari imeamuliwa ni kuilazimisha mahakama na wahusika kurudia mchakato bila sababu za msingi, hali ambayo ni kinyume na misingi ya ufanisi na uadilifu wa kimahakama,” amesema jaji huyo.

Aidha, kesi nyingine 19 zilizotupwa Unguja zilihusisha majimbo ya Nungwi, Kijini, Mkwajuni, Chaani, Tumbatu, Bimbwini, Mtoni, Mwera, Welezo, Pangawe, Mwanakwerekwe, Chumbuni, Mpendae, Amani, Malindi, Kiembesamaki, Makunduchi, Dimani na Shaurimoyo.

Kutokana na uamuzi huo wa mahakama, kesi zote zilizofunguliwa na ACT-Wazalendo kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge Zanzibar uliofanyika mwaka jana zimefutwa.

Baada ya kufutwa kwa kesi zote Zanzibar, ACT-Wazalendo sasa kimebaki na kesi chache za kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge upande wa Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kesi za ubunge ambazo bado ziko mahakamani zinahusisha majimbo ya Ilala, jijini Dar es Salaam, ambako matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Mussa Zungu, yanapingwa katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Kesi nyingine ni ya jimbo la Lindi Mjini mkoani Lindi, inayosikilizwa katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mtwara. Aidha, kuna kesi zinazohusu Jimbo la Tunduru Kusini mkoani Ruvuma (Mahakama Kuu Masjala Ndogo Songea), Jimbo la Rungwe mkoani Mbeya (Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mbeya) na Jimbo la Kigoma Mjini (Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma).

Tofauti na majimbo mengine, Kigoma Mjini, kesi imefunguliwa na wapiga kura wanne ambao ni Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali.

Wapigakura hao walifungua kesi dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando maarufu Baba Levo, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika uchaguzi mkuu uliopita, Baba Levo alitangazwa mshindi baada ya kumshinda mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliyekuwa mbunge wa zamani wa jimbo hilo.