Baraza aupotezea usajili dirisha dogo

WAKATI kesho Ijumaa Januari 30, 2026 dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufungwa, Kocha wa Pamba Jiji, Francis Bara amesema hawana mpango wowote wa kuongeza mchezaji akiamini kikosi kilichopo kinaweza kufanya makubwa hadi mwisho wa msimu huu.

Hata hivyo, pamoja na msimamo huo wa benchi la ufundi, tayari timu hiyo imeondokewa na wachezaji wanne kati ya 30 waliosajiliwa dirisha kubwa.

Waliotimka kipindi hiki cha dirisha dogo ni Abdallah Kheri aliyekwenda Singida Black Stars, Abdallah Iddy (Muembe Makumbi City), Saleh Masoud na Arijifu Amour.

Timu hiyo katika Ligi Kuu Bara msimu huu, imecheza mechi kumi na kukusanya pointi 16 zinazowafanya kuona bado wapo kwenye njia ya kufikia malengo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza amesema kutokana na kikosi alichonacho na matokeo wanayompa haoni sababu za kuongeza yeyote.

Amesema ameamua kufanya hivyo ili kuwapa nafasi nyota wake ambao anaona wameelewa mfumo na falasafa yake, hivyo jukumu kubwa kwake ni kuwaongezea zaidi maujanja ili wawe bora zaidi.

“Sioni sababu ya kuongeza kwa sababu waliopo wananipa matokeo mazuri na matumaini, hivyo bora nielekeze nguvu zaidi kwao ili wawe bora, kuleta wachezaji ambao wataharibu falsafa siyo poa,” amesema kocha huyo.

Baraza aliyewahi kuzinoa timu za Biashara United (wakati wa Ligi Kuu) na Dodoma Jiji, ameongeza kuwa mipango yake ni kuona Pamba Jiji inafanya vizuri na kuonesha soka la ushindani akifafanua kuwa hadi sasa anaridhishwa na matokeo ya timu hiyo.

Amesema kutokana na ugumu wa Ligi na malengo yake ataendelea kuijenga timu kuhakikisha inawania nafasi nne za juu katika msimamo na kwamba iwapo itamlazimu kuongeza mchezaji, ataangalia beki mmoja.

“Ikinibidi naweza kuongeza beki mmoja ambaye naye sitakuwa wa kumtegemea sana ni yule wa kusubiri benchi kwa kuwa maeneo yote yapo fiti, kiujumla nataka Pamba Jiji bora na yenye ushindani,” amesema kocha huyo raia wa Kenya.