CCM Simiyu yaapa kuilinda amani, umoja na mshikamano

Maswa. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu kimewataka wanachama wake kuendelea kuwa mabalozi wa amani, umoja na mshikamano ndani na nje ya chama katika kuadhimisha miaka 49 tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1977.

Hayo yamebainishwa leo Januari 29, 2026, katika Kata ya Isanga, Wilaya ya Maswa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 49 ya chama hicho kimkoa.

Amesema kuwa CCM imeendelea kudumisha misingi ya amani, umoja na mshikamano tangu kuanzishwa kwake na kwamba wanachama wanapaswa kuilinda misingi hiyo hususan katika kipindi cha maadhimisho na kuelekea michakato mbalimbali ya kisiasa.

“Tunapoadhimisha miaka 49 ya CCM, ni lazima tusisitize amani, umoja na mshikamano ndani ya chama chetu na Taifa kwa ujumla. Wanachama wa CCM wanapaswa kuwa mabalozi wa amani popote walipo,” amesema.

Ameongeza kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu “Tumechagua amani na utulivu kwa maendeleo ya nchi yetu”, inaakisi dhamira ya chama ya kulinda utulivu wa kisiasa na kijamii kwa maslahi ya wananchi.

Kwa upande wao, wanachama wa CCM waliohudhuria maadhimisho hayo wameeleza kuwa ujumbe wa amani unaendana na historia na misingi ya chama hicho.

Mwanachama wa CCM kutoka Kata ya Sukuma, Lulu Kaaya amesema amani imekuwa alama ya utawala wa CCM kwa miaka yote.

“CCM kimejengwa juu ya misingi ya amani. Ndiyo maana hata tunapokuwa na tofauti za maoni, tunazitatua kwa njia ya amani,” amesema.

Naye Catheline Daniel, kada wa chama hicho kutoka Wilaya ya Maswa, amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inapaswa kuwa mwongozo wa vitendo kwa wanachama wote hasa katika kipindi hiki cha mvutano wa kisiasa.

“Kaulimbiu yetu hii inatukumbusha wajibu wetu kama wanachama kuhubiri amani na kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga mshikamano wa jamii,” amesema Catherine.

Kwa upande wake, Martine Amos, kada kutoka Maswa, amesema chama kimeendelea kuwa jukwaa la kuwajenga wanachama wake katika misingi ya uzalendo, maadili na mshikamano wa kitaifa.

“CCM kimetujenga kuamini kuwa bila amani hakuna maendeleo. Sisi vijana tunapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani ya chama na Taifa letu,” amesema.

Maadhimisho ya miaka 49 ya CCM mkoani Simiyu yanaendelea kwa ratiba mbalimbali zikiwemo shughuli za kijamii, uhamasishaji wa wanachama na mijadala ya ndani ya chama, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha umoja, mshikamano na utulivu kuelekea hatua zijazo za kisiasa.