Hatari inayowakabili wanaotumia mafuta wakati wa kujamiana

Dar es Salaam. Wakati matumizi ya mafuta yakiwa maarufu kwa wengi kama kilainishi wakati wa kujamiiana, wataalamu wa afya wameonya kuwa yanaweza kuleta madhara makubwa kwa afya ya mwanamke, ikiwamo kuharibu kinga asilia ya uke na kuongeza hatari ya maambukizi.

Wataalamu hao wanaeleza tabia hiyo imekuwa ikichangia wanawake wengi kupata maambukizi ukeni, wakifafanua kuwa kiasili uke hujilinda kwa kutoa ute unaopunguza msuguano na kuzuia maambukizi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo linaeleza vilainishi vinavyotumika kwenye maeneo ya siri vinapaswa kuwa na pH inayofanana na ya uke ili kuepuka kuharibu kinga ya asili ya mwili. pH ni kipimo cha asidi au alkalini (uchachu) wa mazingira ya ndani ya uke, ambacho huonesha kama uke uko katika hali salama ya kiafya au la.

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa mafuta ya kawaida ya kupaka mwili au ya chakula hayajapitiwa kitabibu kwa matumizi ya ndani ya uke, hivyo matumizi yake hubaki kuwa na hatari zisizotabirika kiafya.

Akizungumza na Mwananchi jana, Januari 28, 2026 katika mahojiano maalumu, daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na kinamama, Elias Kweyamba, anaonya matumizi holela ya mafuta na vitu vingine mbadala wakati wa kujamiiana, akisema vinaweza kusababisha madhara kwa afya ya mwanamke.

Anasema zamani KY Jelly ilikuwa ikitumika kama mbadala na ilikuwa salama, lakini ilipigwa marufuku nchini baada ya kubainika kutumika visivyo.

Kuhusu matumizi ya mafuta, anasema kuwa ingawa hupunguza msuguano, yanaweza kuleta changamoto kiafya.

“Baadhi ya mafuta yana kemikali zinazoweza kuua bakteria wazuri wanaolinda uke, hali inayoongeza uwezekano wa maambukizi,” anasema.

Anaongeza kuwa mafuta yanaweza kubaki ukeni kwa muda mrefu hata baada ya kuosha, jambo linaloweza kuvutia bakteria na kusababisha uchafu usio wa kawaida.

Mkazi wa jiji la Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) anasema alianza kutumia mafuta ya kupaka mwili baada ya kukosa ute wa kutosha wakati wa kujamiiana.

“Mwanzoni niliona yananisaidia kupunguza maumivu, lakini baada ya siku chache nilianza kuwashwa na uchafu usio wa kawaida. Nilipofika hospitali niliambiwa nina maambukizi,” anasema.

Neema (si jina lake halisi), mfanyakazi wa sekta binafsi, anasema hakujua madhara ya kutumia mafuta hadi alipokumbana na matatizo ya kiafya.

“Tulikuwa tunatumia mafuta kwa sababu tulidhani ni suluhisho la haraka. Baadaye nikaanza kupata harufu mbaya na maumivu. Daktari alinieleza kuwa mafuta yanaweza kuharibu bakteria wanaolinda uke,” anaeleza.

Kwa upande wake, Rehema, mama wa watoto wawili, anasema matumizi ya mafuta yalimsababishia usumbufu wa muda mrefu.

“Hata baada ya kuosha nilihisi kama mafuta yanabaki. Nilianza kupata maambukizi ya mara kwa mara hadi nilipopata ushauri wa daktari na kuacha kabisa,” anasema.

Akizungumzia ushuhuda huo, Dk Kweyamba anasema matukio hayo yanafanana na anachokiona kwa wagonjwa wengi hospitalini.

“Mafuta yanaweza kusaidia kwa muda mfupi kupunguza msuguano, lakini yakibadilisha mazingira ya uke huacha mwanamke katika hatari ya maambukizi,” anasema.

Akitoa onyo pia kuhusu mate, Dk Kweyamba anawatahadharisha wanaoyatumia kama mbadala wa ute, akisema yana bakteria wa mdomoni ambao hawafai kuwepo ukeni.

“Bakteria wa mdomoni wakifika ukeni wanakuwa chanzo cha maambukizi kwa sababu mazingira ni tofauti,” anasema.

Anasema kiasili maumbile ya mwanamke hujiandaa yenyewe kwa kutoa ute unaorahisisha tendo na kulinda uke dhidi ya michubuko na maambukizi.

“Ute huo ni sehemu ya ulinzi wa mwili wa mwanamke. Ukikosekana na tendo likaendelea, kuna hatari ya michubuko na maambukizi,” anasema Dk Kweyamba.

Kwa mujibu wa daktari huyo, ukavu wa uke unaweza kusababishwa na sababu mbalimbali, ikiwamo msongo wa mawazo, changamoto za kisaikolojia, matatizo ya mahusiano, mabadiliko ya kibaolojia na maambukizi kwenye tezi zinazozalisha ute.

Anaeleza kuwa baadhi ya wanawake hutumia vitu mbadala ili kupunguza msuguano, lakini hatua hiyo inapaswa kufanyika kwa uangalifu mkubwa.

Anasema sababu kubwa ya ukavu wa uke ni msongo wa mawazo unaotokana na hofu ya magonjwa, ujauzito usiotarajiwa, changamoto za mahusiano na shinikizo la maisha.

“Kwa mwanamke, stress huathiri utoaji wa ute, na kwa mwanaume huathiri nguvu za kiume,” anasema.

Tafiti mbalimbali za kisayansi zinaonesha matumizi ya mafuta au vitu visivyoundwa mahsusi kwa afya ya uke yanaweza kuwa na athari kwa afya ya mwanamke, hasa pale yanapotumika mara kwa mara.

Utafiti uliochapishwa katika Journal of Women’s Health Julai 3, 2013 ulibaini kuwa wanawake waliotumia petroleum jelly na baby oil ndani ya uke walikuwa na uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya bakteria (bacterial vaginosis) na fangasi ikilinganishwa na wale wasiotumia.

Sababu kuu ni kwamba mafuta hayo yanabadilisha pH na microbiome ya uke, hali inayochangia kuondoa bakteria wanaolinda uke na kufanya mazingira kuwa rafiki kwa vijidudu hatarishi.

Kwa upande mwingine, tafiti zilizochunguza vilainishi (lubricants) vilivyotengenezwa kisayansi, hasa vya maji (water-based) na silicone, zimeonesha kuwa vinaweza kusaidia kupunguza maumivu na ukavu bila kuathiri sana bakteria wa asili wa uke, endapo vitatumika kwa usahihi.

Dk Kweyamba anawashauri wanawake wanaokumbana na changamoto hiyo kufika hospitalini kwa uchunguzi na ushauri wa kitaalamu badala ya kujitibu wenyewe.

Anasema maambukizi yanatibika, na endapo tatizo linahusisha homoni au vichocheo, zipo dawa salama zinazotolewa kwa ushauri wa daktari.

Anaeleza kuwa mawasiliano mazuri, maandalizi ya kimapenzi na afya ya akili ni msingi wa afya bora ya uzazi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na kinamama, Dk Abdul Mkeyenge, anasema wanaume wanatakiwa kuwaandaa wenza wao wakati wa kujamiiana.

“Wengi wanapokuwa na wenza hawawaandai vizuri, baadaye, wakati wa tendo, unamkuta mwanamke akiwa mkavu, hajapata ule ute ambao ndiyo kilainishi kutoka mwilini.

“Ukimwandaa vizuri, kuna majimaji anayatoa ndiyo yanayosaidia kulainisha sehemu za siri, hata baadaye ukija kumwingilia hatahisi maumivu yoyote wala karaha.

“Wanaume wengi hawawaandai wenza wao ipasavyo, hivyo baadaye wanapata michubuko na wanaumia. Hapo ndipo mwanaume anatafuta suluhisho la haraka kwa kutumia mafuta kama kilainishi, lakini kiafya haitakiwi,” anasema Dk Mkeyenge.