VAIBU la Azam FC baada ya kushinda kwa mara ya kwanza hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho Afrika, limemfanya kocha wa kikosi hicho, Florente Ibenge kusema kwa sasa anaiona nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali.
Wikiendi iliyopita, Azam ilikuwa nchini Kenya kucheza dhidi ya Nairobi United mechi ya tatu kundi B katika Kombe la Shirikisho Afrika na kupata ushindi wa mabao 2-1 ulioifanya kukusanya pointi tatu na kukamata nafasi ya tatu nyuma ya vinara Wydad yenye tisa, AS Maniema (6) na Nairobi United haina kitu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema, kwa sasa malengo ya timu hiyo ni kuhakikisha inafanya vyema katika mechi zingine zilizosalia ili kutinga hatua inayofuata.
Alisema ushindi dhidi ya Nairobi United ni gia yao kwenda kufuzu robo fainali akisema sasa wachezaji wake wamepata pa kuanzia kwa kutoa hofu ya kutoshinda hatua waliyopo.
“Ingawa bado kundi letu ni gumu, lakini tutahakikisha tunatengeneza ushindi wa pili ingawa tutakutana na timu ngumu lakini tunataka kulipa kisasi.
“Mpango wetu wa kwanza ni kuhakikisha tunatengeneza ushindi wa pili kwani ushindi huu wa ugenini umewapa wachezaji imani ya kwamba wanaweza kubadilisha matokeo wakati wowote,” alisema Ibenge.
Jumapili ya wiki hii, Azam itakuwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kucheza dhidi ya Nairobi United, kisha Februari 8, 2026 itaikaribisha AS Maniema uwanjani hapo na kumalizia makundi ugenini ikiifuata Wydad ya Morocco mechi ikipigwa Februari 15, 2026.
Kabla ya kurudiana na Nairobi United, Azam leo Alhamisi itacheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya TRA United kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.
Ni mechi ambayo Ibenge ataitumia kwa mambo mawili, kusaka ushindi wa kuiweka Azam nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, pia kuwaweka fiti zaidi wachezaji wake kwenda kusaka ushindi mwingine kimataifa.
Ubora wa TRA United na aina ya matokeo inayoyapata katika ligi hasa hivi karibuni ikitoka kushinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Singida Black Stars (3-1) na KMC (3-0), kinakuwa kipimo kizuri kwa Azam kabla ya kucheza na Nairobi United.