Kesi ya Bwana Jela kughushi msamaha wa Rais kwa wafungwa yakwama

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama, na wenzake wawili, wanaoshtakiwa pamoja na mashtaka mengine kwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa watatu raia wa China, sasa itaendelea kusikilizwa Februari 24, 2026.

Mbali na Mkama, washtakiwa wengine ni aliyekuwa Ofisa Tehama wa gereza hilo, Sibuti Nyabuya, na mfanyabiashara Joseph Mpangala, mkazi wa Mbezi.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 25517/2024, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, ilipangwa kuendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka leo, Alhamisi, Januari 29, 2026.

Hata hivyo, usikilizwaji huo umekwama kutokana na Hakimu Mhini kutokuwepo, na badala yake imeahirishwa na Hakimu Mkazi Mkuu Hassan Makube kwa niaba ya Hakimu Mhini hadi Februari 24, 2026.

“Kesi hii inakuja kwa ajili ya usikilizwaji. Hata hivyo, kwa leo hatuna shahidi na hakimu anayeisikiliza yuko likizo. Kwa hiyo tunaomba tarehe nyingine ya kusikilizwa mbele ya hakimu husika,” amesema Wakili wa Serikali, Clemence Kato, baada ya kesi hiyo kuitwa.

Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Makube, baada ya kujadiliana na washtakiwa hao ambao wakili wao hawakuwepo mahakamani leo kuhusu tarehe ambayo mawakili wao watakuwa na nafasi, ndipo akaipanga hadi Februari 24, 2026.

Washtakiwa wote wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya Taifa na kuwasilisha mahakamani fedha taslimu ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh7.5 milioni.

Mashtaka katika kesi hiyo

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote watatu wanakabiliwa na kosa la kuongoza genge la uhalifu. Wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 1, 2022 hadi Januari 30, 2023 jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu, waliongoza genge hilo na kujipatia Sh45 milioni kutoka kwa wafungwa namba 585/2019 Song Lei, 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Huang Quin.

Shtaka la pili ni la kughushi barua ya msamaha wa Rais, linalowakabili washtakiwa Mkama na Nyabuya.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Desemba 21, 2022 katika ofisi za Gereza la Ukonga, wilayani Ilala, walighushi barua yenye kichwa cha habari “Nyongeza ya msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru”, wakidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa nyongeza ya msamaha kwa wafungwa hao watatu, ilhali wakijua taarifa hiyo si ya kweli.

Shtaka la tatu, ambalo linamhusu Mkama pekee, ni la kuwasilisha nyaraka ya kughushi. Inadaiwa kuwa Desemba 27, 2022 katika ofisi za Gereza la Ukonga, Mkama aliwasilisha barua hiyo ya kughushi kwa Ofisa Tawala wa gereza hilo, P7411 A/INSP Lusekelo Oden Mwanjati, akimtaka atekeleze maelekezo yaliyokuwa yameainishwa kwenye barua hiyo.

Shtaka la nne linawahusu washtakiwa wote watatu, likiwa ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. Inadaiwa kuwa kati ya Desemba 1, 2022 na Januari 30, 2023, walijipatia Sh45 milioni kutoka kwa wafungwa hao kwa madai kuwa fedha hizo zingesaidia utekelezaji wa barua ya msamaha, wakati wakijua kuwa msamaha huo haukuwahi kutolewa.

Kwa mujibu wa maelezo ya awali yaliyosomwa mahakamani, wafungwa hao watatu wenye asili ya China walihukumiwa Machi 18, 2016 kutumikia vifungo tofauti baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na nyara za Serikali, na walikuwa hawajuani kabla ya kufungwa.

Desemba 21, 2022, Mkama na Nyabuya, ambaye wakati huo alikuwa Ofisa Tehama wa gereza hilo, walitengeneza barua ya kughushi iliyoonesha kuwa imesainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, ikidai wafungwa hao wameongezwa kwenye orodha ya waliopata msamaha wa Rais.

Desemba 27 na 28, 2022, Mkama aliwaita wafungwa hao ofisini kwake akiwa na Mpangala, kuwaonesha barua hiyo pamoja na hati ya kuwatoa gerezani, na kuwaambia watoe Sh45 milioni kama sharti la kuachiwa.

Fedha hizo aliwaelekeza wazikabidhi Mpangala, jambo ambalo walifanya, ingawa hawakuwahi kuachiwa.

Sakata hilo lilibainika baada ya wakili wa mmoja wa wafungwa, Song Lei, Aloyscious Mandago, kuambiwa na mteja wake kuwa wamepata msamaha wa Rais.

Baada ya kufanya uhakiki, wakili huyo aligundua barua hiyo ni ya kughushi na taarifa zikapelekwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Baada ya uchunguzi, washtakiwa walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Hadi sasa mashahidi sita kati ya 17 wa Jamhuri wamekwishatoa ushahidi.

Washtakiwa wote wamekana mashtaka yanayowakabili, na kesi inaendelea kusikilizwa.