Libase Gueye aanza na moto, Simba ikiichapa Mashujaa 2-0

LIBASE Gueye, mechi yake ya kwanza Ligi Kuu Bara ndani ya Simba akicheza dhidi ya Mashujaa, amefanikiwa kufunga bao, huku akionyesha kiwango kilicholeta matumaini mapya ndani ya kikosi hicho katika ushindi wa mabao 2-0.

Winga huyo ambaye Januari 17, 2026 alitambulishwa kuwa mchezaji wa Simba akitokea Teungueth FC ya kwao Senegal, alifunga bao hilo dakika ya 27 kwa ufundi mwingi akimtesa kipa wa Mashujaa, Patrick Munthali.

Uchezaji wake wa kuhama upande kushoto na kulia, ulikuwa ukiwatesa walinzi wa Mashujaa wakiongozwa na nahodha, Mpoki Mwakinyuke.

Dakika ya 40, Samson Madeleke katika jitihada za kumzuia Gueye, alijikuta akimchezea vibaya ndani ya boksi, mwamuzi Ahmed Arajiga kutoka Manyara akaamuru mkwaju wa penalti ambao hata hivyo, Kibu Denis aliyechukua jukumu la kupiga, akakosa baada ya Munthali kuokoa.

Hata hivyo, kipindi cha pili, mabadiliko yaliyofanywa kwa kuingia Seleman Mwalimu kuchukua nafasi ya Kibu, yalizaa matunda baada ya mshambuliaji huyo kufunga bao dakika ya 75.

Wakati Gueye akifunga bao hilo akiitumia pasi ya Kibu Denis, huku pia akisababisha penalti akitumika kwa dakika 77 kisha kumpisha Naby Camara, mwisho wa mechi akatangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.

Mbali na Gueye, nyota wengine wapya wa Simba walioanza kikosini mechi hiyo ikiwa ya kwanza kwao Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo Alhamisi Januari 29, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Dar, Clatous Chama, Nickson Kibabage, Anicet Oura na Djibrilla Kassali, walionyesha uwezo mzuri.

Kassali ambaye ni kipa raia wa Niger, aliokoa mchomo mmoja wa hatari dakika ya 65 uliopigwa na Hassan Ali ‘Cheda’.


Oura, alitumika kwa dakika 82 kabla ya kumpisha nyota mwingine mpya mzawa, Baraka Mwangosi, huku pia Ismael Touré akipata nafasi ya kucheza akiingia dakika ya 82 kuchukua nafasi ya Rushine De Reuck.

Mechi hiyo ambayo Simba imepata ushindi uliofanya kufikisha pointi 16 na kupanda kutoka nafasi ya sita hadi nne baada ya mechi saba, imeibua matumaini kuelekea wikiendi hii itakapocheza dhidi ya Esperance katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker katika mechi ya leo alifanya mabadiliko ya wachezaji wanne ya kikosi kilichoanza ukilinganisha na kile kilichocheza dhidi ya Esperance katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Barker aliwaanzisha David Kameta, Libasse Gueye, Anicet Oura na Clatous Chama kuchukua nafasi za Shomari Kapombe, Naby Camara, Jonathan Sowah na Elie Mpanzu.

Kwa upande wa Mashujaa, kipigo hicho ni cha pili mfululizo katika ligi baada ya kutoka kuchapwa 6-0 na Yanga, Januari 19, 2026. Matokeo yanayofanya kuendelea kusalia nafasi ya nane ikiwa na pointi 13.

SIMBA: Mamadou Tanja, David Kameta, Rushine De Reuck, Wilson Nangu, Nickson Kibabage, Yusuph Kagoma, Clatous Chama, Morice Abraham, Libasse Gueye, Kibu Denis na Anicet Oura.

Benchi: Hussein Abel, Ladaki Chisambi, Ismail Toure, Anthony Mligo, Naby Camara, Neo Maema, Daud Semfuko, Seleman Mwalimu, Baraka Mwangosi na Vedastus Masinde.

MASHUJAA: Patrick Munthali, Mpoki Mwakinyuke, Samwel Onditi, Abdulnasir Assa, Salum Kihimbwa, Hassan Ali, Selemani Bwenzi, Jafari Kibaya, Mapinduzi Balama, Mohamed Salum na Samson Madeleke

Benchi: David Uromi, Yusuf Dunia, Mgandila Shabani, Crispin Ngushi, Frank Magingi, Lameck Kayonga, Abdul Bakari, Mudathir Saidi, Seif Rashid na Imani Bahati.