Dar es Salaam. Baada ya mtu kujitambua kiakili, kielimu au kijamii huanza kulitazama jina lake kwa jicho jipya, wengine huliona halilingani na utu wao wa sasa, ndoto walizonazo au hata hadhi wanayojijengea.
Inaelezwa chanzo cha hali hii mara nyingi ni mabadiliko ya mtazamo, mtu anapopanuka fikra, huanza kujiuliza maswali mapya, je, jina langu linaniwakilisha?” “Ninajivunia nikilitaja hadharani?”
Wengine huathiriwa na mitandao ya kijamii, ulimwengu wa ajira au mwingiliano wa kimataifa ambako majina fulani huonekana rahisi au yanakubalika zaidi, hapo ndipo mgongano wa utambulisho huanza.
Hili ni jambo linalowakumba watu wengi kimyakimya, jina linaweza kuonekana la kizamani, la kubeza, au kubeba kumbukumbu zisizopendeza za utotoni, familia au mazingira waliyokulia kama ilivyo kwa Juma Shaban.
Shaban anasema akiwa darasa la tatu ndipo alianza kulichukia jina hilo (Juma) alilopewa na wazazi wake miaka 34 iliyopita.
“Limekuwa jina ninalolichukia hadi sasa, miaka kadhaa nyuma niliwaza kulibadilisha lakini haikuwa rahisi kutokana na mazingira niliyokuwa nayo.
“Hivi sasa nina uwezo huo lakini tayari limeshazoeleka kuanzia kazini, mtaani na kwenye jamii hivyo naona hata nikibadili haitakuwa na maana tena, japo nalichukia na huwa sipendi kuitwa Juma,” amesema.
Akieleza sababu za kulichukia amesema akiwa darasa la tatu jina hilo lilikuwa likifananishwa kwenye matukio ya ajabu kuanzia kwa walimu wake shuleni hadi mtaani.
“Ilifikia hatua hadi wanafunzi wenzangu wakawa wananitania na kunihusisha na matukio hayo yaliyokuwa yakifanywa na kina Juma wakati ule.”
“Nilianza kulichukia kuanzia pale hadi leo, hata ninapojitambulisha mbele za watu najitaja kwa jina la pili (Shaban),” amesema Juma akifafanua kwamba mama yake aliwahi kumueleza sababu za kuitwa jina hilo ni kwa kuwa alimzaa siku ya Ijumaa.
Mariam Karim pia ni miongoni mwa wanaochukia majina yao, anasema huwa anatamani kuyabadilisha majina hayo lakini anapata shinikizo la kutofanya hivyo kutoka kwa mama yake.
“Huwa sipendi kutumia jina la Karim kwa kuwa ni baba yangu ambaye hakunilea na sikuwahi kumuona japo nasikia yupo.”
“Mama yangu aliniambia hata jina la Mariam pia ni la bibi yangu mzaa baba ambaye alinipa kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa baba, japo alimuacha akiwa na mimba yangu, historia ile imefanya niyachukie majina yangu yote mawili,” amesema Mariam.
Stephano Gikaro yeye anaeleza kulichukia jina la baba na babu yake anayotumia kwenye utambulisho wake.
“Sikuwahi kulelewa na baba yangu, isivyo bahati nilimfahamu nikiwa mdogo lakini hakuwahi kunisaidia kwa chochote hata baada ya mama yangu kufariki na kulelewa na bibi, hivi sasa nina kazi nzuri na baba yangu anafahamika, mara nyingi huwa nikiulizwa wewe ni mtoto wake? Nakataa na kusema ni majina tu yamefanana.
“Huwa natamani nibadili majina yangu yote ili niwe na amani ya moyo, lakini tayari yamekwishazoeleka japo nayachukia,” amesema.
Maana ya majina kidini, kiimani
Mchungaji Daniel Mgogo amesema katika imani majina yana nguvu akitolea mfano maandiko kwamba hata Mwenyezi Mungu kuna watu aliwabadilisha majina alipotaka kuwatumia.
“Mfano ni Sauli kuwa Paulo, Sarai kuwa Sara na wengine ambao inawezekana hawakuandikwa, hivyo katika imani jina lina nguvu.”
“Hata katika maisha ya sasa kuna watu walitamkiwa majina mabaya na hadi leo yanawatesa, hivyo unapopewa jina angalia na maana yake, ingawa sio kwamba atakayepewa jina zuri ataenenda vizuri japo kuna imani katika majina,” amesema.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema ki kawaida katika dini wazazi wanapaswa kuwapa watoto majina mazuri.
Amesema katika sehemu ya malezi ya Kiislamu mzazi atakayepuuza jambo hilo anakuwa amepuuza haki muhimu ya mtoto wake.
“Mtume alikuwa anapenda majina mazuri, alibadilisha majina yenye maana mbaya mfano Harb (vita) na kuwa Salim (mwenye amani), jina la Asiyah (muasi) na kuwa Jamilah (mzuri) na kuonyesha umuhimu wa jina katika Uislamu,” amesema.
Amesema jina si alama pekee ya utambulisho, bali hujenga heshima na malezi ya saikolojia na kiroho kwa mtoto hivyo katika Uislamu jina lina uhusiano wa karibu na imani, tabia na hatima ya mtu,” amesema Sheikh Mataka.
Mwanasaikolojia, Daniel Sendoro amesema zipo nadharia zinazoaminisha watu kwamba majina yanaweza kutengeneza tafsiri ya maisha ya mtu.
“Zipo hadithi za kusadikika kwamba majina yanashabihi katika maisha ya mtu, hata hivyo sio kila wakati na wakati wote inakuwa hivi, haina maana ukiitwa jina zuri ndiyo litashabihi maisha yako,” amesema Sendoro ambaye pia ni Mchungaji.
Amesema ni vizuri watu kuheshimu majina waliyopewa na watu waliowaleta duniani, na badala ya kulikataa moja kwa moja, mtu anaweza kwanza kulielewa na kuelewa alipewa kwa sababu gani, lina maana gani, na linaakisi nini kuhusu wazazi au jamii.
“Thamani ya mtu haiko kwenye herufi za jina, bali kwenye matendo, maadili na mchango wake kwa jamii, ukijikubali wewe mwenyewe, hata jina lako litapata maana mpya.”
“Pambana kutengeneza utu wako ili usilinganishwe na majina kwamba unaitwa Bahati basi wewe utegemee kuishi kwa bahati, haipo hivyo jina linaweza kuwa na maana lakini sio kwenye kila wakati,” amesema.
Ukitaka kubadili fanya haya
Mmoja wa maofisa wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) aliyeomba hifadhi ya jina amesema mchakato wa kubadili majina ni mrefu na unapotaka kubadili lazima ubadili nyaraka zote.
“Ingekuwa mifumo inaingiliana ingekuwa rahisi, lakini uanze kubadili kuanzia shule hadi nyaraka nyingine ni mchakato, huwa tunashauri kwenda kwa Kamishna wa viapo anakupa nyaraka ya kuonyesha huyu ni fulani lakini anayetambulika pia kwa majina ya fulani,” amesema.
Akizungumzia kwa muktadha wa kisheria, wakili kiongozi wa kampuni ya uwakili ya Haki Kwanza, Aloyce Komba amesema hatua ya kwanza kabisa ya kubadili majina ni kumuona mwanasheria mwenye hadhi uwakili ili akutengenezee kiapo kinaitwa Deed Poll.
“Hicho kiapo utaapishwa na Kamishna wa viapo na kusajiliwa kwa Msajili wa Hati Wizara ya Ardhi ambako utalipia kisha atachapisha tangazo kwenye gazeti la Serikali na hapo utakuwa umebadili majina.
Amesema baada ya hapo utaanza mchakato wa kubadili na majina kwenye vyeti vyako kila eneo ambako kuna maeneo utafanikiwa na kwingine utafeli kubadili moja kwa moja labda uanze upya mchakato wa kuvipata.