MSHAMBULIAJI mpya wa TRA United ya Tabora, Enock Jiah, amesema amefurahi kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kukaa kwa muda bila kucheza soka la ushindani kufuatia kuachana na Fanja FC ya nchini Oman, huku akiweka malengo ya kucheza tena soka nje ya Tanzania.
Jiah anayemudu kucheza pia kama kiungo mshambuliaji, amejiunga na TRA United kwenye dirisha dogo la usajili msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili na nusu, ambapo alitambulishwa klabuni hapo Januari 23, 2026.
Nyota huyo ameungana na Mzamiru Yassin, Denis Nkane, Athuman Songoro na Mussa Halili waliosajiliwa dirisha dogo kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Ettienne Ndayiragije.
Kabla ya kusajiliwa, Jiah alifanya majaribio na kikosi hicho kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika Januari 13, 2026 visiwani Zanzibar, ambapo alifunga bao moja, huku kiwango chake kikiwavutia TRA United.
Akizungumza na Mwanaspoti, Jiah amesema usajili huo ni fursa nzuri kwake kuendeleza safari yake ya soka huku akiwa na malengo ya kufanya vizuri na kurejea nje ya nchi kucheza soka la ushindani.
“Usajili huu kwangu ni fursa nzuri ya kuendeleza fani yangu wakati ambao nasubiri ofa za nje ya Tanzania kwani bado nina malengo ya kurudi huko,” amesema Jiah.
Nyota huyo wa zamani wa Ihefu, Coastal Union, KM-KM, Mwadui na Mbeya Kwanza, amesema Ligi Kuu Bara ni sehemu sahihi kwake kwa sasa kwani imepiga hatua kubwa, hivyo itamsaidia kuimarika, kurejesha utimamu, ushindani na kufikia malengo yake.
“Ushindani ni mkubwa wa nafasi na kila mchezaji ni mzuri na anajituma, kwa hiyo ni moja ya sababu ya mimi pia kujituma zaidi ili kuwa na uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza cha mwalimu Ettienne Ndayiragije,” amesema Jiah na kuongeza;
“Nimefurahi kurudi kwenye ligi ya nyumbani kwani kwa sasa ni moja ya ligi kubwa Afrika na inaendelea kukua kila siku na upinzani ni mkubwa sana kwa timu zote. “Malengo yangu kwa sasa ni kuhakikisha naisaidia timu kumaliza ligi katika nafasi za juu ili kupata nafasi ya kucheza mashindano ya CAF na kupandisha thamani ya timu na yangu pia.”