KIKOSI cha Simba, leo Alhamisi kinashuka kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa, huku nyota wawili wa timu hiyo, wakikalia kuti kavu la kuachwa kabla ya dirisha dogo halijafungwa Januari 30, 2026.
Nyota hao ni viungo, Mkenya Mohammed Bajaber aliyejiunga na timu hiyo akitokea Kenya Police FC ya kwao Kenya na Neo Maema, aliyetua kikosini humo kukitumikia kwa mkopo, baada ya kuondoka Mamelodi Sundowns ya kwao Afrika Kusini. Wote wamesajiliwa dirisha kubwa msimu huu.
Mmoja kati ya nyota hao, ni lazima aondoke kwa ajili ya kupisha usajili wa kiungo mshambuliaji raia wa Congo Brazzaville, Inno Jospin Loemba, ambaye tayari amewasili nchini kwa lengo la kukitumikia kikosi hicho.
Sababu kubwa ya Bajaber au Maema mmoja wao kuondoka kabla ya dirisha halijafungwa kesho Ijumaa, ni kupisha usajili wa Loemba na kukamilisha idadi kamili ya wachezaji 12 wa kimataifa wanaotakiwa kikanuni.
Simba ambayo dirisha hili dogo la usajili hadi jana mchana ilikuwa imetambulisha wachezaji wapya sita wakiwamo watano wa kigeni, tayari imefikisha idadi ya wachezaji 12 wa kimataifa, hivyo ujio wa Loemba, lazima mwingine achomolewe.
Loemba anajiunga na Simba baada ya kuachana na Colombe Sportive du Dja et Lobo ya Cameroon, ambayo msimu wa 2024-2025, aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo, kufuatia kumaliza na pointi 65, ikishinda mechi 19, sare nane na kupoteza tatu.
Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali za Inter Club de Brazzaville, JS de Talangai na AS Otoho zote za kwao Congo Brazzaville, ametua nchini Tanzania tangu juzi usiku, ambapo muda wowote atatambulishwa kukitumikia kikosi hicho.
Loemba anakuwa nyota wa sita wa kigeni kusajiliwa na Simba katika dirisha hili dogo, akiungana na kipa, Mahamadou Tanja Kassali aliyetoka AS FAN Niamey ya kwao Niger na beki Ismael Olivier Toure kutoka FC Baniyas ya Falme za Kiarabu (UAE).
Wengine ni kiungo mshambuliaji Clatous Chama aliyerejea Msimbazi akitokea Singida Black Stars, winga Libasse Gueye kutokea Teungueth FC ya kwao Senegal na Alain Anicet Oura raia wa Ivory Coast aliyeondoka IF Gnistan ya Finland.
Ongezeko la nyota hao, kunaifanya Simba kufikisha nyota 13 wa kigeni sambamba na waliokuwepo ambao ni Neo Maema, Mohammed Bajaber, Naby Camara, Elie Mpanzu, Rushine De Reuck, Alassane Kante na Jonathan Sowah, ambao lazima mmoja wao aondolewe.
Hata hivyo, kumekuwa na misuguano ya nani aondolewe kati ya wawili hao, kwani uongozi unahitaji Maema kwa sababu ya kutoridhishwa sana na kiwango chake, ingawa Kocha, Steve Barker anatamani aendelee kubaki, huku upande mwingine ukitaka atolewe Bajaber kutokana na majeraha ya mara kwa mara yanayomkabili.
Akizungumzia usajili wa Simba unaoendelea, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema kabla ya dirisha kufungwa kwa siku zilizobaki, watakuwa wameboresha kikosi hasa eneo la mbele, lakini suala la nani anaachwa, linabaki kuwa ndani ya uongozi na muda ukifika itafahamika.
Hadi sasa, Wachezaji wa kimataifa ambao hawatakuwa na kikosi cha Simba baada ya dirisha dogo kufungwa Januari 30 mwaka huu ni Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala, Joshua Mutale, Chamou Karaboue na Moussa Camara.