Masharti mapya ya mikopo ya asilimia 10, Nida yatatajwa

Dodoma. Serikali imetangaza kulegeza masharti ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu, lakini sharti kuu ni lazima iwalenge Watanzania, ikiwemo kuwa na Kitambulisho cha Taifa (Nida).

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Januari 29, 2026, na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni, kama ilivyo utaratibu wa kikanuni.

Waziri Mkuu amekiri kuwepo na mlolongo mrefu wa upatikanaji wa mikopo hiyo, ambayo imekuwa na vikwazo visivyowezekana kwa baadhi ya wakopaji, hasa kwenye suala la dhamana za nyumba na barua za udhamini kwa watumishi.

Swali hilo limeulizwa na Mbunge wa Segerea (Chaumma), Agnesta Kaiza, aliyehoji ni namna gani Serikali inaweza kupunguza masharti hayo, kwani Watanzania wengi wanashindwa kufikia ndoto zao kwa kupata mikopo hiyo.

Kaiza amesema Serikali imefanya maboresho ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa kupeleka fedha katika baadhi ya benki ili yakopeshe wanawake, vijana na wenye ulemavu, ambao kimsingi hawakuwa na uwezo wa kukopesheka kwenye taasisi nyingine.

“Lakini benki zimeweka masharti makubwa kwa walengwa kupata mikopo hii, na mara nyingi vigezo vinawatoa nje wahitaji kutokana na kukosa dhamana. Je, Serikali haioni ni vyema kubadilisha mtindo huu wa ukopeshaji?” amehoji Kaiza.

Mbunge huyo ametoa mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambako zipo Sh91 bilioni ambazo hazijakopesheka kwa sababu ya hitaji la dhamana, na akauliza kama fedha hizo zingeshapeleka tabasamu kwa wananchi kwa kuwainua kiuchumi.

Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema: “Ni kweli Serikali ilibadilisha utaratibu wa ukopeshaji kwa kuanza kutoa fedha kupitia mabenki. Baadhi ya halmashauri ziliendelea na utaratibu wa awali. Lengo la kufanya hivi lilikuwa ni kudhibiti utaratibu wa vikundi hewa kwa watumishi wasiokuwa waaminifu.”

Dk Mwigulu amesema mpango huo ulikuwa na malengo mahsusi ya kuhakikisha makundi hayo yanakuwa sehemu ya wanufaika, lakini urejeshaji wa fedha haukutimia kwa kiwango kikubwa.

Amesema hivi karibuni alikutana na wafanyabiashara ndogondogo, machinga na mama lishe, ambao moja ya mambo waliyozungumzia ni mikopo ya asilimia 10 na masharti yake.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, ni lazima mikopo hiyo iende kwenye uhalisia, kwani machinga hawezi kuwa na hati ya nyumba wala kuwa na udhamini wa mtumishi wa Serikali.

“Maelekezo ya Serikali ni kulegeza masharti ya hati ya nyumba, barua za udhamini na vigezo vingine. Wenzetu wa benki walikuwepo, na niliwaambia utaratibu uwe ni kuwapambanua ili wanufaika wawe Watanzania kweli na wawe na Kitambulisho cha Taifa (Nida). Kwa ambaye hatakuwa na kitambulisho hicho, anatakiwa kuchunguzwa na kuombwa vielelezo zaidi,” amesema.

Ametoa sababu kwa watakaokosa vitambulisho kwamba anatambua wapo watu ambao alisoma nao sekondari hadi chuo kikuu, lakini baadaye alishangaa kuona wakifanya kazi nchi jirani na kuwanufaisha watu wa huko.

Amesema Serikali hivi karibuni ilitenga Sh 200 bilioni kwa ajili ya vijana, lakini bajeti ijayo itatenga asilimia tano kwa ajili ya kuweka msingi wa kuwajengea maeneo ya kufanyia biashara machinga, na ikibidi kulipia maeneo ambayo watu watapisha ili kutoa nafasi ya biashara.

Baada ya majibu hayo ya Dk Mwigulu, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, aliweka msisitizo kwa wakurugenzi wa halmashauri kusimamia maelekezo ya Waziri Mkuu, akisema zipo biashara ambazo hazihitaji kuwepo kwa ofisi wala vitu vingine zaidi ya uaminifu, akitoa mfano wa biashara za mitandaoni.

Mikopo hiyo imekuwa na malalamiko makubwa, ikiwemo kutolewa kwa watu wasiokuwa na vigezo, huku Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zikiibua upigaji wa fedha hizo.

Aprili 13, 2023, aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliielekeza halmashauri zote nchini kusitisha utoaji wa mikopo hiyo kuanzia Aprili hadi Juni 2023, wakati Serikali ikijipanga kuweka mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo.

“Katika mkutano huu wa Bunge, kuliibuka hoja kuhusu kiasi kidogo cha fedha za mikopo zitokanazo na asilimia 10 ya makusanyo ya halmashauri kinachotolewa kwa makundi maalum kutokidhi matakwa ya kuyainua makundi hayo kwa kufanya shughuli za uzalishaji au biashara,” alisema Majaliwa.

Katika hoja hiyo ilielezwa kuwa kumekuwa na changamoto katika baadhi ya halmashauri kutoa fedha hizo kwa watumishi wa halmashauri au vikundi hewa badala ya walengwa, na kusababisha fedha za mikopo hiyo kutorejeshwa.

Machi 29, 2023, wakati akipokea taarifa ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka 2021/2022, Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kuangaliwa upya utaratibu wa utoaji wa mikopo, ikiwemo kuangalia namna ya kutumia mabenki kupitishia mikopo hiyo.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu ameielekeza Wizara ya Afya kuzingatia viwango rasmi vya gharama za huduma na kuharakisha mpango wa kutunga sheria itakayoweka viwango vinavyofanana nchini kote ili kuondoa hali ya baadhi ya maeneo kuwa na viwango tofauti.

Ametoa maelekezo hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani, aliyetaka kupata kauli ya Serikali kuhusu viwango wanavyotozwa wananchi kama gharama ya kumuona daktari ambaye ni mwajiriwa na analipwa mshahara na Serikali.

Dk Mwigulu amesema kwa mujibu wa utaratibu wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, wananchi wanahimizwa kujiunga na mifumo ya bima ili kupunguza changamoto ya kuchangia gharama wanapohitaji huduma hospitalini.

Amesema makundi yaliyoainishwa kisheria kama watoto chini ya miaka mitano, wajawazito, wazee na wenye magonjwa ya mlipuko yanaendelea kupata msamaha wa kuchangia gharama hizo.

Kuhusu changamoto ya mifumo hospitalini, Dk Mwigulu amesema Serikali itafuatilia kwa karibu ili kuondoa uzembe na visingizio vinavyochelewesha wagonjwa, huku taasisi husika zikielekezwa kurekebisha mapungufu ya kimfumo, kwa kuwa huduma za afya hazipaswi kusubiri.