Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Aisha Ulenge ameitaka Serikali kuendelea kuwekeza katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi na kuhakikisha wanafunzi wa mijini na vijijini wanapata elimu yenye viwango sawa.
Akizungumza leo, Januari 29, 2026, wakati akichangia hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyotolewa Novemba 14, 2025 wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13, Ulenge amesema Tehama itarahisisha mwalimu mmoja kufundisha madarasa mengi kwa wakati mmoja.
Ulenge amesema matumizi ya Tehama yatawezesha kuziba pengo la upungufu wa walimu wa sayansi na kuimarisha upatikanaji wa elimu bora kwa wote.
“Ni muhimu kuhakikisha msingi wa elimu unalenga usawa kati ya wanafunzi wa vijijini na mijini. Teknolojia itasaidia kufanikisha hili,” alisema Mbunge Ulenge.
Aidha, Ulenge amesisitiza maendeleo makubwa ya kiuchumi mkoani Tanga, akitaja viwanda vitatu vilivyokuwa vimekufa kwa muda mrefu ambavyo vimefufuliwa ndani ya siku 100 za Rais Samia.
Miongoni mwa viwanda hivyo ni Kiwanda cha African Harmonies, ambacho kimeajiri watu 218 wa kudumu.
“Kingine ni Kiwanda cha Rolling Steel kinachozalisha nondo tani 30 hadi 40 kwa wiki, ambacho kimeanza kutoa ajira. Vilevile, Kiwanda cha Marine Body nacho kimeanza kutoa ajira,” alisema.
Mbunge huyo pia ameitaka Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya Kiomoni–Mlingama yenye urefu wa kilomita 31.9 kwa kiwango cha lami.
Amesisitiza kuwa hotuba ya Rais Samia imetoa mwelekeo chanya wa maendeleo ya Taifa, huku Tehama ikionekana kuwa nyenzo muhimu katika utekelezaji wa dira hiyo.