Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imetangaza zabuni ya kumtafuta mshauri wa ujenzi wa hospitali mpya ya kisasa, hatua inayotekeleza mkakati wa Serikali wa kuimarisha huduma za afya ya rufaa na kupunguza msongamano wa wagonjwa hospitalini hapo.
Mradi huo wa ujenzi unaokadiriwa kugharimu Sh1.3 trilioni, unahusisha usanifu wa majengo, usimamizi wa ujenzi, ushauri wa kiufundi, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na uboreshaji wa mifumo ya kidijitali ya taarifa za wagonjwa.
Akizungumza waandishi wa habari Dar es Salaam leo Alhamisi January 29, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk Delila Kimambo amesema hatua ya kutangaza zabuni ya mshauri ni mwanzo rasmi wa utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaolenga kuibadili Muhimbili kuwa hospitali ya kisasa inayokidhi viwango vya kimataifa.
“Kwa sasa tupo kwenye hatua za awali za kumpata mshauri atakayesimamia ujenzi wa hospitali mpya. Mshauri huyo atahusika katika kuhakiki michoro ya majengo, kusimamia utekelezaji wa mradi na kuhakikisha viwango vya hospitali za rufaa za kimataifa vinafuatwa kikamilifu,” amesema.
Hatua hiyo inatekeleza ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Novemba 13, 2025, wakati akilihutubia Bunge la 13, alipoeleza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Rais Samia alisema Serikali itaongeza uwezo wa hospitali hiyo kutoka vitanda 1,435 vya sasa hadi kufikia vitanda 1,737 ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ili kuifanya Muhimbili kuwa hospitali ya kuaminika na kutumainiwa Afrika Mashariki.
Dk Kimambo amesema hospitali mpya itajengwa ndani ya eneo la Muhimbili Upanga, baadhi ya majengo ya zamani yatabomolewa ili kupisha ujenzi wa majengo machache ya kwenda juu, yenye ghorofa kati ya 11 hadi 15.
“Kwa sasa mgonjwa anapohudumiwa Muhimbili anaelekezwa sehemu moja hadi nyingine, jambo linalochosha na kupunguza ufanisi wa huduma.
“Serikali imetambua changamoto hii na ikaamua kuboresha miundombinu kwa kujenga majengo ya kwenda juu, yatakayorahisisha utoaji wa huduma kwa mpangilio mzuri,” amesema.
Pia, amesema tayari hospitali imeanza kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mradi huo, ikiwamo kuweka mabango yanayoonesha ‘coming soon’ kuashiria ujio wa majengo mapya ya hospitali ya kisasa.
Dk Kimambo amesema baada ya kumpata mshauri, hatua inayofuata itakuwa kuthibitisha michoro iliyopo kabla ya kuanza ujenzi kwa awamu, ili kuhakikisha huduma kwa wagonjwa hazikatizwi wakati wa utekelezaji wa mradi.
“Tunalenga kujenga kwa awamu na kwa tahadhari kubwa. Ndani ya kipindi chote cha ujenzi, huduma hazitasimama. Tumepanga namna ya kuhakikisha wagonjwa wanaendelea kupata huduma bila usumbufu,” amesema.
Pia, alisema ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitano, huku Sh1.3 trilioni zikielekezwa katika ujenzi wa majengo mapya, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, uwekaji wa mifumo madhubuti ya taarifa za wagonjwa na mafunzo kwa wataalamu wa afya.
Kwa sasa Muhimbili hupokea takribani watu 25,000 kwa siku, kati yao wagonjwa 6,000 huonwa na hospitali hiyo, huku ikitoa jumla ya huduma za kliniki 127.
Baadhi ya wagonjwa walipongeza mpango huo, wakisisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa wagonjwa wakati wa ujenzi.
“Ni jambo zuri sana, lakini ni muhimu pia wagonjwa wengi zaidi waelekezwe Mloganzila ili kupunguza msongamano hapa. Kama majengo yatabomolewa, hapa itakuwa finyu zaidi wakati hii ni hospitali ya Taifa,” amesema Jafari Juma (72), mkazi wa Kigamboni.
Katika hatua nyingine, Dk Kimambo amewasisitiza wananchi kusoma risiti zao kwa makini kabla ya kufanya malipo ya Serikali kupitia ‘control number’ ili kuepuka changamoto wanapokwenda kupata huduma.
Amesema hospitali imeweka namba maalumu za mawasiliano kwa ajili ya kushughulikia changamoto na malalamiko ya wagonjwa, ikiwamo huduma za dialysis, maabara, upasuaji, malipo na bili pamoja na ofisi ya mkurugenzi mtendaji.
“Tunalenga kutoa huduma bora. Kama kuna anayehisi hajahudumiwa ipasavyo, tumeweka namba wazi ili kupata mrejesho na kuchukua hatua kwa haraka,” amesema.
Dk Kimambo amesema Muhimbili imefanikiwa kupata ithibati ya maabara na ipo katika hatua za mwisho za kupata ithibati ya famasi, huku maandalizi ya kuimarisha huduma za uzazi kwa mama na mtoto yakiendelea ili kupunguza malalamiko na kuongeza ubora wa huduma.