MV New Mwanza itakavyofungua uchumi Tanzania, Kenya na Uganda

Mwanza. Uzinduzi wa kuanza rasmi safari za Meli ya kisasa ya MV New Mwanza unaashiria hatua mpya ya kimkakati katika kuimarisha uchumi, biashara na usafirishaji wa majini katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani za Afrika Mashariki.

Ambayo kwa kuanzia itafanya safari zake kati ya Bandari za Mwanza, Kemondo na Bukoba kisha baadaye itaenda  Port Bell nchini Uganda na Kisumu nchini Kenya.

Meli hiyo, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200, magari 20 na mizigo tani 400, ikitembea kwa kasi ya knoti 16 (km 30 kwa saa) imekuja kama nyenzo muhimu ya kuunganisha masoko ya ndani na ya kikanda, kupunguza gharama za usafirishaji, kuchochea uwekezaji na kuongeza mchango wa maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria katika pato la Taifa (GDP).

Kwa mtazamo wa kiuchumi, MV New Mwanza ni zaidi ya chombo cha usafiri ikiwa ni muundombinu wezeshi unaotarajiwa kuleta mabadiliko katika mnyororo wa thamani wa sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara ya mipakani na utalii.

Kwamujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda meli hiyo imejengwa kwa wakati muafaka na anasema itanufaisha wananchi takribani milioni 3.6 wa mkoa huo, sambamba na kuongeza mchango wao katika pato la Taifa.

“Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa pato la Taifa kwa asilimia 7.2, ukiwa wa pili kitaifa. Kuimarishwa kwa miundombinu ya usafirishaji majini kama hii kutawawezesha wananchi kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa,” alisema Mtanda.

Meli ya kisasa ya MV New Mwanza, ambayo itafanya safari zake kati ya Bandari za Mwanza, Kemondo na Bukoba kisha baadaye itaenda Port Bell nchini Uganda na Kisumu nchini Kenya. Picha na Maktaba



Sifa na Uwezo wa MV New Mwanza

MV New Mwanza ni meli ya kisasa iliyojengwa kwa viwango vya kimataifa, ikiwa na uwezo wa kubeba mizigo hadi tani 400 pamoja na abiria kwa wakati mmoja. Uwezo huo unaifanya kuwa meli ya kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ikilinganishwa na meli zilizokuwapo awali katika Ziwa Victoria.

Mbali na uwezo wa kubeba mizigo mikubwa, meli hiyo imeundwa kwa kuzingatia usalama wa abiria, ufanisi wa safari na kupunguza muda wa usafirishaji. Sifa hizi zinaifanya kuwa mbadala wa kuaminika wa usafirishaji wa barabara, ambao kwa muda mrefu umekuwa na changamoto za gharama kubwa, ucheleweshaji na uharibifu wa bidhaa.

Kufungua fursa za kiuchumi, biashara na utalii

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma ya Meli Tanzania (Tashico), Eric Hamissi anasema tayari wameanza mazungumzo na  Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kutumia meli hiyo kama utalii ndani ya maji  kuendana na dhana ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza utalii nchini.

“Tumeshaanza mazungumzo na TTB. Tunataka meli hii itumike pia kwa utalii ili kuchangia kukuza uchumi kupitia sekta hiyo,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi, Ally Mkino anasema MV New Mwanza inalenga zaidi kukuza uchumi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuimarisha biashara na usafirishaji wa bidhaa.

“Naiona kama mbadala wa MV Bukoba. Uwepo wa meli yenye uwezo wa kubeba mizigo tani 400 utarahisisha sana usafirishaji wa bidhaa, kukuza biashara za uvuvi, kilimo na bidhaa za viwandani,” anasema Mkino.

Anaongeza kuwa meli hiyo itaunganisha biashara kati ya Tanzania, Uganda na Kenya, hasa kwa bidhaa ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikisafirishwa kupitia Ziwa Victoria, zikiwemo mafuta ya kula na mazao ya kilimo.

“Uwepo wa meli kubwa kama hii unaimarisha mnyororo wa ugavi, unaongeza ajira katika sekta za usafirishaji, kilimo na uvuvi, na unachochea uwekezaji katika bandari,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkino, Bandari ya Kemondo Bay inatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na ongezeko la shughuli za kibiashara, hali itakayoongeza mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa eneo hilo.

“Wafanyabiashara wachangamkie fursa hasa kwenye kusaka taarifa kufahamu ratiba za meli, uwezo wake wa kubeba mizigo na wafuate taratibu zote zilizoainishwa kwenye usafirishaji bidhaa ili waweze kunufaika na wafanye tafiti za masoko kwa Kenya na Uganda bidhaa ambazo  zinahitajika mfano bidhaa za kilimo kama mchele ni miongoni mwa bidhaa zinazohitajika sana,” anasema.

Amewataka wakulima kuongeza uzalishaji kwakuwa kutakuwa na unafuu wa usafirishaji wa mizigo hivyo waongeze uzalishaji kunufaika na fursa hiyo.

Meli ya kisasa ya MV New Mwanza, ambayo itafanya safari zake kati ya Bandari za Mwanza, Kemondo na Bukoba kisha baadaye itaenda Port Bell nchini Uganda na Kisumu nchini Kenya. Picha na Maktaba



Ajira na uhamishaji wa ujuzi

Kwa mujibu wa Hamissi, ujenzi wa MV New Mwanza umeleta manufaa ya moja kwa moja kwa rasilimali watu ambapo kupitia mradi huo, wahandisi wa meli na mafundi walipata mafunzo kwa vitendo, ujuzi ambao utatumika katika miradi mingine ya kimkakati nchini.

Anasema jumla ya ajira takribani 500, rasmi na zisizo rasmi, zilitolewa kwa nyakati tofauti wakati wa ujenzi wa meli hiyo, hatua iliyosaidia kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea uchumi wa ndani.

Wafanyabiashara wazungumza

Wafanyabiashara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa wameeleza matarajio makubwa juu ya MV New Mwanza wakisema meli hiyo ni suluhisho kwa changamoto za usafirishaji wa mizigo.

“Hii meli nimeshaitumia mara mbili au tatu. Ni nzuri sana na abiria wanaridhika. Changamoto ni miundombinu ya kupakia mizigo North Port na gharama ya usafirishaji ambayo kwa sasa ni Sh30,000 kwa tani. Tunatarajia ipungue hadi Sh25,000,” alisema  Mabula Kija, mfanyabiashara wa ndizi katika soko la Tanpile jijini Mwanza.

Mfanyabiashara wa mazao ya samaki alisema meli hiyo itasaidia kusafirisha bidhaa za uvuvi, ikiwemo samaki wa kukaushwa (vibambala), bila hasara ya kuharibika kutokana na kuchelewa.

Mfanyabiashara wa nafaka Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Karim Juma anasema kuanza kwa safari za meli hiyo ni fursa kubwa ya kibiashara na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara hasa kwa wafanyabiashara wa Kenya na Uganda ambao mara kadhaa wamekuwa wakitumia usafiri kwa njia ya barabara kupitia malori.

Subira Maulid, mfanyabiashara mwingine Bukoba anasema, “Tulikuwa tunapata hasara kutokana na ucheleweshaji na uharibifu wa bidhaa. Meli hii itatuwezesha kufikisha bidhaa haraka, salama na kwa ubora unaokidhi mahitaji ya soko,”

Naye Willelimia Anthony, mjasiriamali wa parachichi na ndizi anasema ujio wa MV New Mwanza utapunguza hasara na kufungua masoko mapya hadi Uganda na Kenya kwakuwa wafanyabiashara hawatotegemea masoko ya ndani pekee.

Huku,  Mkazi wa Isevya mkoani Tabora akisema mkoa huo ni mzalishaji mkubwa wa tumbaku (asilimia 60 ya uzalishaji wa kitaifa), pamba na mazao ya chakula, hivyo meli hiyo itatumika kusafirisha mazao hayo kwa ufanisi.

Zaidi ya manufaa ya kiuchumi

Wakati wa ziara yake jijini Mwanza, Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa ujenzi wa meli hiyo.

“MV Mwanza itarahisisha usafiri kati ya Kampala na Mwanza. Nitarudi na taarifa hii kwa Serikali ya Uganda ili kuendelea kuimarisha biashara ya pamoja,” alisema.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dk Bwire, alisema MV New Mwanza ni meli ya kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na itabadilisha sura ya usafirishaji na biashara katika Ziwa Victoria.

“Meli hii siyo ya abiria na mizigo pekee, bali ni kichocheo cha utalii na ushirikiano wa kikanda kati ya Tanzania, Uganda na Kenya,” alisema.