Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Profesa Said Mohammed amesema mtoto asipopata maarifa ya Kuandika, Kusoma na Kuhesabu (KKK) anaathirika katika nyanja zote za ukuaji na ujifunzaji kiakili, kimwili, kijamii na kihisia.
Umuhimu wa mafunzo haya ni kama maziwa ya mama kwa kichanga kwani kadri mtoto anavyokosa maziwa ya mama anakosa msingi wa afya, vivyo hivyo mtoto anapokosa msingi wa KKK anakosa msingi wa elimu.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 29, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa mpango Mkakati wa kisayansi wa kujenga umahiri katika Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa awali Darasa la Kwanza na Pili kwa shule za msingi nchini iliyofanyika jijini hapa.
Uzinduzi huo uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, amesema ili kuimarisha hilo, Necta iliendesha upimaji wa KKK kwa njia ya sampuli tangu mwaka 2015 ambapo walikuwa wakichagua shule mbili hadi tano kwa shule nchini.
Mpango huo ulihusisha walimu huku wakiwa na madodoso kwa lengo la kukusanya taarifa muhimu, hali ya shule, taarifa za wanafunzi, mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, upatikanaji wa vitabu na uwepo wa walimu waliopata mafunzo.
Matokeo ya upimaji katika kipindi chote kati ya 2015 hadi 2023 yalionyesha asilimia 67 hadi 87 walikuwa na umahiri wa kumudu stadi za KKK na umahiri mzuri zaidi ulionekana katika stadi ya kusoma na kuandika.
Kwenye stadi za kusoma, wanafunzi wengi waliweza kusoma kwa ufasaha maneno yaliyoundwa kwa silabi moja au silabi zilizoundwa na konsonanti moja na irabu, kwa maneno yaliyoumbwa na silabi zenye konsonanti muambatano utendaji ulikuwa wastani.
“Kama ungemuuliza mtoto asome neno Mkenda, lingemsumbua kwa sababu ya ile nda ya NDA. Changamoto mbalimbali zilibainika ikiwemo wanafunzi kushindwa kusoma maneno yenye silabi zenye herufi za ving’ong’o kama vile ng’ambo au ng’ombe kutokana na kutamka sauti hiyo na kutoa hewa kwa njia ya mdomo badala ya kutoa hewa kwa njia ya pua,” amesema.
Kushindwa kusoma maneno 50 kwa dakika moja kutokana na ukosefu wa umahiri wa kusoma kwa kasi na ufasaha, huku matamshi ya R na L yakionekana kusumbua wanafunzi kutokana na athari za lugha mama za kikabila mfano Mara ikitamkwa Mala na Subira ikitamkwa Subila.
Kwenye kuandika changamoto zilibainika katika kuandika maneno yaliundwa kwa silabi zenye muundo wa konsonanti pekee, maneno yenye silabi za mfuatano wa konsonanti na kubaini matumizi ya herufi kubwa na ndogo.
Kwenye kuhesabu changamoto ilikuwa kwenye kubaini namba zinazokosekana, kujumlisha namba zinazohitaji kubeba au kutoa namba zinazohitaji kukopa.
Pia kutambua maneno yanayohusisha matendo ya kihisabati kama vile kupungua, kubaki, tofauti na ongezeko wakati wa kufungua mafumbo.
Katika kukabiliana na changamoto hizo walitoa mafunzo kuhusu upimaji wa KKK kwa walimu wa madarasa ya awali hadi darasa la pili, maafisa elimu taaluma, wakuu wa shule za msingi, walimu wa taaluma, maofisa elimu kata, wadhibiti ubora katika mikoa na halmashauri zote nchini.
“Kwa miaka mitatu, pamoja na juhudi za taasisi mbalimbali, Necta pekee liliendesha mafunzo kwa walimu 43,141,” amesema.
Amesema mtaala unataka mwanafunzi akifika darasa la tatu awe amemudu stadi za KKK ili kuendelea kujifunza kwa ufanisi hivyo mafunzo waliyotoa kwa walimu na uzoefu uliopatikana sasa kumekuwa na kuimarika kwa ufaulu katika ngazi ya upimaji wa darasa la nne na mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Takwimu za upimaji wa kitaifa darasa la nne mwaka 2022 hadi mwaka 2025 zinaonyesha kupungua kwa wanafunzi wasiomudu stadi za KKK na mwaka 2022 waliofika darasa la nne walikuwa 25,841 waliokosa stadi hizo.
“Mwaka 2023 walipungua na kufikia 15,616, mwaka 2024 wakapungua tena na kufikia 8,960 na mwaka jana wakifika 5,847, huu ni ushahidi kuwa hatua zinazochukuliwa na serikali zimekuwa na matokeo chanya,” amesema.
Baada ya kuonekana kwa hali hiyo waliona hakuna haja ya kuwatambua wanafunzi hao wanapofika darasa la nne kwani wanakuwa wamechelewa hivyo waliamua kuanzisha upimaji wa kitaifa darasa la pili ngazi ya shule.
“Tumefanya zoezi hili Novemba 18 hadi 20 Novemba mwaka jana katika shule 20,864 ambapo wanafunzi 1,789,884 walifanya upimaji huo na ndani yake walichopeka kwa mara ya kwanza umahiri wa basic English language,” amesema.
Amesema Necta iliandaa ratiba moja kwa shule zote nchini na mwongozo wa upimaji, zana ya upimaji, mfumo wa kompyuta uliotumika kuwasajili wanafunzi, kupandisha maswali na kunasa alama huku walimu wakisimamia upimaji, walifanya usahishaji na kurekodi alama katika mfumo wa kompyuta.
“Wakati tunatangaza zoezi hili, ilidhaniwa kuwa ni kitu kisichowezekana, bila shaka hofu sasa imeondoka na kila mdau wa elimu ataamini kuwa kilichopangwa kinawezekana,” amesema.
Amesema KKK ikisimama, elimu ya msingi, sekondari na elimu ya juu itakuwa imara huku akitolea mfano wa ufaulu wa hesabu ngazi ya sekondari ambalo limekuwa likionekana gumu.
Amesema hisabati kwa ngazi ya A Level ndiyo lililoongoza kwa kuonyesha kiwango kizuri cha ufaulu katika mtihani wa kidato cha sita kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2023 hadi 2025.
Ufaulu wa somo hilo umefikia viwango vya juu, umekaribia kufikia asilimia 100, mwaka 2023 ulikuwa asilimia 96.86 na mwaka 2024 ulikuwa asilimia 97.51.
“Somo la Advanced Mathematics umeendelea kuwa miongoni mwa yanayotoa idadi kubwa ya watahiniwa wanaopata wastani wa daraja A ikilinganishwa na masomo mengine. Mwaka 2023 lilikuwa na watahiniwa 1,239 waliopata A likifuatiwa na Kiswahili lililokuwa na watahiniwa 1,064,” amesema.
Amesema mwaka 2024 watahiniwa 2,013 walipata A huku kemia ikiwa na watahiniwa 1,083, mwaka 2025 Advanced Mathematics lilishika nafasi ya pili kwa kutoa watahiniwa 1,209 waliopata A baada ya Basic Applied Mathematics kuongoza kwa watahiniwa 1,246.
Kwa upande wa O Level somo linaitwa Basic Mathematics, ndiyo somo ambalo ufaulu wake kidato cha pili hauna tofauti na ule wa kidato cha nne.
Pamoja na ufaulu wake kuwa chini ya wastani lakini limekuwa likiimarika kwa zaidi ya asilimia 5.
“Wapo wanaotaja umbali kuwa sababu ya somo hilo kupungua lakini umbali huu utakuwa na shida na hesabu pekee, vipi shule za bweni, wapo wanaotaja ari na motisha ya walimu kuwa huenda inachangia hesabu kushuka kiwango lakini je ari inashuka kwenye hesabu tu vipi masomo mengine wanayofaulu vizuri,”
“Wengine wanadai hesabu imefanywa kuwa somo la lazima linafanywa na wanafunzi wote lakini ukiangalia baiolojia nayo ni lazima ni sayansi inafanywa na wanafunzi wote lakini ukiangalia tathmini baiolojia inafanya vizuri,” amesema.
Amesema katika mabadiliko haya ya kisera wadau wa elimu wanapaswa kuja na majibu ya kisayansi ya kutatua changamoto za kielimu.
Amesema katika upande wa hesabu ni vyema kutokomeza woga juu ya hesabu na mwaka 2024 Necta ilibadili mfumo wa mitihani kutoka kuchagua hadi maswali mchanganyiko ambayo iliongeza ari ya ufundishaji kwa walimu na wanafunzi.
Pia alitaka dhihaka iachwe kwenye somo la hesabu kwani dunia inaendeshwa na sayansi na hisabati ni sayansi huku akitaka mbinu za ufundishaji hisabati ni lazima zitumike kuanzia ngazi ya KKK.
“Singapore imefanikiwa sana katika hisabati na wamefanikiwa sana kupitia njia ya CPA (Concrete Pictorial Abstract) wanafunzi lazima wafundishwe kwa vitendo, kama tulivyoona kwenye maonyesho kutakuwa na michezo ya hisabati, kurukaruka, kuhesabu,” amesema.
Ufundishaji wa CPA ni mzuri lakini unahitaji kujitoa, kucheza na tafiti zinaonyesha kuwa wanafunzi wanaelewa kwa asilimia 10 kama watajifunza kwa njia ya kusoma lakini uelewa utapanda na kufika 20 kama watasoma na kusikia na utafika asilimia 30 kama watakachofundishwa watakiona kwa macho.
Uelewa huo utafika asilimia 50 kama watasoma, watasikia, wataona na kufanya study tour. Wanafunzi wataelewa hadi asilimia 70 kama walichojifunza watakuwa na uwezo wa kukielezea, kukiandika na kushiriki katika mazoezi ya vitendo.
“Watafika hadi asilimia 90 kama watafika hatua ya kuunda na hii sasa ndiyo haya mabadiliko ya kisera ambapo ndani yake kuna mtaala wa elimu ya mkondo wa amali ambapo pamoja na nadharia vitendo vimepewa nafasi kubwa na sisi Necta katika miongozo ya utahini tumetoa asilimia 60 katika kusimamia upimaji wa ngazi ya shule,” amesema.
Alichokisema Waziri Mkenda
Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda ametaja mambo matano yatakayozingatiwa katika utekelezaji wa mpango mkakati huo kwa watoto wa darasa la awali hadi la pili kwa shule zote nchini.
Profesa Mkenda amesema mkakati huo utakwenda kuimarisha ufundishaji kwa kufanya mafunzo endelevu kwa walimu na kusimamia namna bora ya kufundisha elimu ya awali, darasa la kwanza na pili.
“Pia tutakuwa na maendeleo endelevu ya walimu ya kuwaandaa, kuwashirikisha hasa katika kuandaa vifaa vya kufundishia, tutahakikisha kunakuwapo na nyenzo za kufundishia na kujifunzia ambazo zinapatikana kila eneo nchini kwani miongoni mwake ni vizibo vya chupa za soda,” amesema.
Sehemu ya nne ni kufanya upimaji ili kuhakikisha kuwa mpango unaenda vizuri kama ilivyokusudiwa kupitia tathmini na upimaji.
“Mwisho ni ushirikishwaji wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wake. Sisi hatutaeleza mengi sasa hivi, tutakusikiliza lakini kuanzia hapa baada ya uzinduzi, tutakuwa tunaeleza, tutasimamia na kufuatilia na wenzetu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,” amesema.
Amesema watajitahidi kila mwaka kutoa mrejesho kuonyesha mwenendo wa utekelezaji wa mpango huo utakaochukua miaka mitano kuanzia mwaka 2026 hadi 2030/2031.