Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe limeanzisha msako aliyetengeneza video na kusambaza mtandaoni ikionyesha tukio la zamani ambalo askari walikwenda kutoa msaada kwa wananchi na kutengenezea taarifa ya uongo kwamba askari polisi amevamiwa na wananchi na kuporwa silaha kisha kuchomwa.
Jeshi hilo mkoani Njombe, limekanusha taarifa hizo zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii nchini zikiambatana na picha mjongeo ambazo zinaeleza uwepo wa askari polisi wa mkoa huo kuchomwa moto na kisha kuporwa silaha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, jana Januari 28, 2026 ametoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo wakati akizungumza na waandishi wa habara mkoani hapa.
Banga amesema kuwa katika Mkoa wa Njombe hakuna tukio la askari polisi kuchomwa moto kisha kunyang’anywa silaha kama taarifa zinavyoonyesha kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Amewaonya watu ambao wanashiriki katika kuandaa na kusambaza taarifaa za uongo na upotoshaji kuwa watachukuliwa hatua za kisheria endapo watabainika kuhusika na vitendo hivyo.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wenye tabia za kuandaa na kusambaza taarifa za uongo na upotoshaji kwa njia mbalimbali kuacha kwani ni kinyume cha sheria za nchi na maadili ya Mtanzania,” amesema Banga.
Amesema hakuna faida yoyote kwa watu wanaofanya matukio ya kusambaza taarifa za uongo na upotoshaji kwa jamii na taifa kwa ujumla zaidi ya yote huishia sehemu ambayo haifai.
Amesema jeshi hilo linaendelea kumfuatilia mtu ama watu waliochukua na kutumia picha mjongeo ya tukio la zamani ambalo askari walikwenda kutoa msaada kwa wananchi na kutengenezea taarifa hiyo ya uongo na kisha kuisambaza katika mitandao ya kijami.
Amesema polisi wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na wananchi kupitia programu za polisi jamii ili kubaini na kuzuia uhalifu sambamba na kufanya doria, misako na operesheni katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha maisha na mali za wananchi zinakuwa salama wakati wote.
Baadhi ya wananchi wakizungumzia tukio hilo akiwemo Peter Stephano amesema tukio hilo limezua taharuki kwa baadhi ya wananchi mkoani humo lakini kupitia taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi wanaweza kuendelea na shughuli zao kwa amani.
“Hii taarifa ilitushtua kwamba askari kuchomwa moto na kuporwa silaha mbona hatari sana,” amesema Stephano.