:::::
Rais wa Tanzania amefanya uteuzi wa Viongozi mbalimbali,ambapo amemteua Dkt Ladislaus Benedict Chang’a kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye kabla alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt Moses Kusiluka pia imeeleza kuwa Rais Dkt Samia amemteua Dkt Rahma Salim Mahfoudh kuwa Naibu Gavana,Utawala na Udhibiti wa ndani wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambapo ambachukua nafasi ya Julian Banzi Raphael ambaye amemaliza muda wake. Pia Prof.Muhammad Bakari Kambi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo anachukua nafasi ya Dkt Ellen Makondya Senkjoro ambaye amemaliza muda wake.
Aidha Balozi Wilson Kajumula Masilingi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Uhamasishaji uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini,Mafuta na Gesi Asilia Tanzania (TEITI) ambapo anachukua nafasi ya CPA Ludovic Utouh ambaye amemaliza muda wake.
