RC KHERI JAMES AKERWA NA MWALIMU ALIYEMFUKUZA MWANAFUNZI KISA KAKOSA RIMU

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, ameonesha kukerwa na kitendo cha Mkuu wa Shule moja mkoani humo aliyerudisha nyumbani wanafunzi waliochelewa kuleta rimu baada ya shule kufunguliwa, akibainisha kuwa uamuzi huo umekosa hekima na busara.

Akizungumza kuhusu hali ya lishe na upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni, RC Kheri James amesema viongozi na watumishi wa umma wanapaswa kutumia busara katika maamuzi yao, hususan yanayogusa ustawi wa watoto. 

Amehimiza kuachana na mtazamo wa kudhani kuwa wazazi na walezi wote wana uwezo sawa wa kiuchumi, akisisitiza kuwa hali za maisha hutofautiana na hivyo maamuzi yanapaswa kuzingatia uhalisia wa jamii.

Aidha, amewataka viongozi kuacha tabia ya kujisahau na badala yake waweke mbele maslahi ya wanafunzi, akisisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi na changamoto ndogo za vifaa zisigeuzwe kuwa kikwazo cha watoto kupata elimu.