Dar es Salaam. Serikali imeandaa mpango mkakati wa kisayansi wa kujenga umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la pili ili kukabiliana na changamoto ya uwepo wa wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma.
Mpango mkakati huo utakaotekelezwa ndani ya miaka mitano unalenga kuhakikisha kila mtoto anamudu stadi za msingi afikapo darasa la tatu kupitia njia za kisayansi, shirikishi na bunifu.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Profesa Said Mohamed matokeo ya Upimaji wa Taifa wa KKK kwa Darasa la Pili mwaka 2023 yanaonesha kuwa, asilimia 78.92 ya wanafunzi waliofanya upimaji walifanya vizuri katika kusoma, asilimia 69.6 kuandika na asilimia 62.56 kuhesabu.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa, bado baadhi ya wanafunzi wasiofikia umahiri unaohitajika, hasa kuandika na kuhesabu, hivyo mpango mkakati huo utasaidia kumaliza tatizo hilo katika hatua za awali za elimu ya msingi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Januari 29, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan amesema mkakati huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050 inayosisitiza maendeleo ya rasilimali watu na Taifa linaloongozwa na maarifa na uadilifu.
Sambamba na hilo ameutaja mkakati huo kama utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 iliyolenga kumuwezesha mwananchi kuwa na maarifa, stadi, maadili na uwezo wa kuchangia maendeleo na ustawi wa Taifa.
Amesema kama nchi inaweza kujenga miundombinu imara, kukuza maarifa na teknolojia, lakini endapo hakukuwa na juhudi za kuimarisha msingi wa awali wa kufundisha watoto, ni kama kujenga juu ya msingi dhaifu na matokeo yameonekana miaka ya nyuma.
“Tunajenga juu ya msingi dhaifu ambao hauko sawasawa na kwa maana hiyo watoto wakitoka kuhitimu masomo yao darasa la saba, kidato cha nne kidogo mambo yanakuwa si mazuri,” amesema Samia.
Amesema hiyo ndiyo sababu ya kufanyika kwa maboresho ya mtalaa wa elimu ya lazima kuwa miaka 10 ili kuhakikisha watoto wanapikwa kisawasawa.
Rais Samia amesema mtoto anayemudu stadi za KKK anakuwa na uwezo wa kuelewa maarifa mapya, kufikiri kwa kina, kudadisi na kushiriki kikamilifu katika kujifunza, hivyo ni jukumu la walimu na wizara kusimamia wizara kuzalisha kwa wingi zana hizo ili watoto wawe na fursa ya kuzitumia na kuelewa yanayofundishwa.
“Nimetembelea maonesho, nimeona watoto watakavyoshirikishwa, kutengeneza maumbo, kutengeneza namba kwa kutumia mchanga, msasa, pumba na vitu vidogo vilivyopo nchini, tumesogea sana na tutasogea kwa sababu nyenzo tunazotumia ni za hapa ndani,” amesema.
Amebainisha kuwa, katika dunia ya sasa Taifa lolote linalotaka kujenga uchumi shindani, huwekeza mapema katika stadi za awali za mafunzo, kwa kuwa jambo hilo si la hiari bali ni wajibu wa Serikali, wazazi na jamii kwa jumla.
Akizungumzia mkakati huo kisayansi Profesa Mohamed amesema mtoto asipopata maarifa ya KKK, anaathirika katika nyanja zote za ukuaji na ujifunzaji kiakili, kimwili kijamii na kihisia.
Amesema ili kuimarisha hilo, Necta iliendesha upimaji wa KKK kwa njia ya sampuli tangu mwaka 2015 ilipokuwa ikichagua shule mbili hadi 5 nchini.
Mpango huo ulihusisha walimu huku wakiwa na madodoso kwa lengo la kukusanya taarifa muhimu, hali ya shule, taarifa za wanafunzi, mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, upatikanaji wa vitabu na uwepo wa walimu waliopata mafunzo.
Amesema mtalaa unataka mwanafunzi akifika darasa la tatu awe amemudu stadi za KKK ili kuendelea kujifunza kwa ufanisi, hivyo mafunzo waliyotoa kwa walimu na uzoefu uliopatikana sasa, umekuwa na kuimarika kwa ufaulu katika ngazi ya upimaji wa darasa la nne na mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Takwimu za upimaji wa kitaifa darasa la nne mwaka 2022 hadi mwaka 2025 zinaonesha kupungua kwa wanafunzi wasiomudu stadi za KKK na mwaka 2022 waliofika darasa la nne walikuwa 25,841 waliokosa stadi hizo.
“Mwaka 2023 walipungua na kufikia 15,616, mwaka 2024 wakapungua tena na kufikia 8,960 na mwaka jana walifika 5,847, huu ni ushahidi kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali zimekuwa na matokeo chanya,” amesema.
Akizungumzia uwekezaji katika sekta ya elimu, Rais Samia amesema katika kipindi cha miaka minne Serikali imefanya jitihada kubwa kuboresha upatikanaji wa elimu kwa kuongeza kiwango cha uandikishaji na kuimarisha miundombinu katika shule za msingi za sekondari.
Katika elimu msingi madarasa yameongezeka kutoka 151,315 mwaka 2021 hadi madarasa 184,550 mwaka 2025 na sekondari madarasa yakitoka 64,204 mwaka 2021 hadi 101,473 mwaka 2025.
Pia, amesema katika ahadi zake za siku 100 za uongozi waliahidi kuajiri walimu 7,000 na hadi sasa 6,044 wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi na wengine 956 wako kwenye mchakato kujaza nafasi zilizobaki ili kufikia Februari 3 nafasi zote 700 ziwe zimekamilika.
Awatwisha zigo akaguzi
Rais Samia amesema maboresho hayo hayatoshelezi ikiwa hawatasimamia ubora wa mafunzo yanayotolewa hasa katika hatua za mwanzo za ukuaji wa mtoto na hapo inakuja haja ya kuimarisha kitengo cha ukaguzi.
“Katika hili wakaguzi mna kazi kubwa, twendeni tukasimamie haya, tuhakikishe watoto wetu yale yaliyopangwa kwenye mpango huu wa kuhakikisha darasa la awali hadi la pili wanatoka wakijua KKK, hiyo ni kazi yenu wakaguzi nami nawatia moyo nendeni mkafanye kazi yenu,” amesema.
Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha walimu wanakuwa suluhisho la kudumu katika utekelezaji mkakati huo kwa kuwapatia nyenzo na mafunzo; pamoja na kuwaongezea ujuzi ili wapate mbinu za kisasa za ufundishaji na ufuatiliaji wa karibu.
Ametaka mkakati huo usiishie kwenye karatasi bali ubebe matokeo yatakayopimika na manufaa kwa walengwa na Taifa kwa jumla huku akitaka ufuatiliaji wa matokeo ya utekelezaji wa mkakati huo kuwa sehemu ya uwajibikaji katika ngazi zote kuanzia mwalimu, mkuu wa shule, ofisa elimu wa wilaya hadi mkoa.
“Kusiwe na ripoti za kuandika tu, tunataka mabadiliko yaonekane kwa mtoto, tunapotembelea sehemu, tukisimamisha mtoto wa darasa la pili akijiandaa kwenda darasa la tatu tuhakikishe amesoma, ameandika na ameweza kuhesabu kwa jinsi ilivyopangwa,” amesema Rais Samia.
Ili kufanikisha hilo alielekeza tathmini za mafunzo zifanyike mapema ili kubaini wenye changamoto kwa lengo la kupatiwa msaada kwa wakati, kwa kuwa stadi za KKK ndiyo daraja linaunganisha sera, mitalaa na matokeo halisi ya elimu, hivyo upimaji na tathmini endelevu ni muhimu ili kubaini mapema changamoto na kuchukua hatua stahiki.
“Nitoe wito kwa wazazi, jamii na walezi kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kufanikisha mkakati huu. Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mkakati, itahakikisha rasilimali mifumo na usimamizi vinakwenda sambamba ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wakati,” alisema.
Alichokisema Waziri Mkenda
Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda amesema mkakati huo utakwenda kuimarisha ufundishaji kwa kufanya mafunzo endelevu kwa walimu na kusimamia namna bora ya kufundisha elimu ya awali, darasa la kwanza na pili.
“Pia, tutakuwa na maendeleo endelevu ya walimu ya kuwaandaa, kuwashirikisha hasa katika kuandaa vifaa vya kufundishia, tutahakikisha kunakuwapo na nyenzo za kufundishia na kujifunzia ambazo zinapatikana kila eneo nchini, miongoni mwake ni vizibo vya chupa za soda,” amesema.
“Mbali na hayo, utafanyika upimaji ili kuhakikisha mpango unaenda vizuri kama ilivyokusudiwa kupitia tathmini na upimaji.
“Mwisho ni ushirikishwaji wa wazazi, walezi na jamii kwa jumla wake. Sisi hatutaeleza mengi sasa hivi, tutakusikiliza lakini kuanzia hapa baada ya uzinduzi, tutakuwa tunaeleza, kusimamia na kufuatilia; na wenzetu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,” amesema.
Profesa Mkenda ameahidi kila mwaka wizara itakuwa inatoa mrejesho kuonesha mwenendo wa utekelezaji wa mpango huo utakaochukua miaka mitano kuanzia mwaka 2026 hadi 2030/2031.