Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Serikali imeanza mpango wa kurejesha viwanda vyote vilivyobinafsishwa kwa zaidi ya miaka 15 bila kuendelezwa hatua ambayo itasaidia kuchochea uchumi wa Mkoa na kutoa fursa ya ajira kwa vijana.
Babu ameyasema hayo leo wakati wa kikao cha Baraza la wafanyabiashara wa mkoa huo, kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Moshi, Mkoani humo.
Amesema Mkoa huo una viwanda vingi ambavyo havijaendelezwa na kwamba vingeendelezwa vingewezakutoa fursa ya ajira kwa vijana wengi ambao hawana ajira.
“Kipo kiwanda cha viberiti cha Kibo Match na Kiwanda cha Magumia ambavyo vilikuwa mjini Moshi, lakini havifanyi kazi na badala yake viberiti Sasa hivi vinaagizwa nje ya nchi,” amesema RC Babu.
Babu amesema “Mkoa tumedhamiria kufufua viwanda na wale wote waliobinafsishwa viwanda ambavyo vimekaa zaidi ya miaka mitano, 10 na 15 waturudishie viwanda vyetu maana wameshindwa kuviendeleza,”amesema RC Babu.
Amesema”Wewe umepewa Kiwanda miaka 20 alafu hufanyi chochote unaenda kufanya mambo yako mengine, huku tunapiga kelele vijana hawana ajira, yaani wewe unapewa nyumba alafu nyumba hukai, tunachukua nyumba yetu na kumpa mtu mwingine mwenye uwezo wa kufanya hilo jambo.”
Pamoja na mambo mengine, amesema serikali inatambua mchango wa sekta binafsi nchini na kwamba itaendelea kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitatua ili kurahisisha shughuli za ufanyaji biashara hapa nchini.
“Nasisitiza umuhimu wa kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu za biashara ikiwemo kulipa kodi na tozo stahiki, nimesema hapa Mkoani staki mfanyabiashara yoyote anafungiwa biashara, kama anadaiwa TRA wakae naye, waandikiane mikataba tujue analipaje hizo fedha.Maana yake ukimfungia akapate wapi hizo fedha wakati umemfungia, ndio maana unaona tunakwenda vizuri.”
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Yusuf Kisseo, amesema viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi na tayari vimerejeshwa serikalini ni Kiwanda cha kukoboa mpunga, Kiwanda cha madawa ya kilimo na Kiwanda cha kuzalisha bidhaa za mbao ambavyo vinatafutiwa wawekezaji.
“Hivyo wawekezaji waliopewa viwanda na kushindwa kuviendeleza na kuzalisha ajira ili vijana wetu wapate ajira, serikali imedhamiria kuviendeleza ili kukuza uchumi wa Mkoa na kutoa fursa ja ajira kwa vijana,”amesema Kisseo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoani hapa, Patrick Boisafi, amesema kufufuliwa kwa viwanda vilivyokuwa vimefungwa mkoani humo kutachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
Boisafi ameeleza kuwa kufufua viwanda kutafungua fursa nyingi za ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla, jambo litakaloongeza kipato cha kaya na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
“Kilimanjaro ina fursa kubwa ya kuwa kitovu cha uzalishaji endapo viwanda vitarejeshwa katika uzalishaji wake wa awali. Viwanda ni mhimili muhimu wa uchumi na vinasaidia kuongeza thamani ya mazao, kukuza biashara na kuongeza mapato ya Serikali” amesema Boisafi.
Kwa upande mwingine, amewataka wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kufanikisha mpango huo, huku akisisitiza umuhimu wa kupenda kazi, uadilifu na kuacha mazoea kazini.
Amehimiza Watanzania kufanya kazi kwa bidii, hofu ya Mungu, bila ubinafsi wala chuki, na kuwakaribisha wadau na wawekezaji mbalimbali kuja kuwekeza mkoani Kilimanjaro kwa maendeleo ya pamoja.