Dodoma. Serikali inaendelea kutekeleza mpango maalum wa kutoa elimu na kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuzuia maambukizi mapya na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu kinga, upimaji na matibabu ya ugonjwa huo.
Maelezo hayo yametolewa bungeni leo Alhamisi, Januari 29, 2026 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, kufuatia swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Naomy Mwaipopo, aliyehoji mpango wa Serikali katika kutoa elimu ya homa ya ini kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma, akizingatia athari za ugonjwa huo kwa afya ya jamii.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na homa ya ini kupitia vituo vya kutolea huduma za afya, vyombo vya habari pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram, TikTok na Facebook.
Amesema katika Mkoa wa Kigoma, mpango huo unatekelezwa kwa kutumia wahamasishaji wa ngazi ya jamii wanaotoa elimu kuhusu umuhimu wa upimaji wa Homa ya Ini, njia za kujikinga na upatikanaji wa matibabu kwa wananchi.
“Serikali imeendelea kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ili waweze kutoa elimu sahihi kwa jamii, hadi sasa jumla ya watoa huduma 102 wa Mkoa wa Kigoma wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu ugonjwa wa homa ya ini, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa huduma za kinga na matibabu,” amesema.
Amesema wizara imekuwa ikitoa elimu ya homa ya ini kupitia vyombo vya habari kwa makundi ya vijana, watu wazima, akina mama wajawazito, viongozi wa dini, wanahabari na viongozi wa ngazi ya jamii.
Kundi lingine ni madereva wa magari ya masafa marefu, watu wanaojidunga dawa za kulevya, wachimba madini, wavuvi, wenzi wenye majibu tofauti ya maambukizi pamoja na watoa huduma za afya.
Amesema wananchi wameendelea kupata elimu na ushauri kupitia namba za bila malipo 117 na 199, ambapo washauri nasaha waliopatiwa mafunzo maalum kuhusu homa ya ini wanatoa maelekezo na msaada wa kitaalamu.
Katika swali lake la nyongeza, Mwaipopo amehoji Mkoa wa Kigoma una viwango vikubwa vya maambukizi ya homa ya ini ikilinganishwa na mikoa mingine, hali inayochangiwa na jiografia yake ya kupakana na nchi jirani ikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia.
Ameiomba Serikali kuongeza juhudi zaidi za kudhibiti ugonjwa huo, akibainisha kuwa njia za maambukizi ya homa ya ini zinafanana kwa kiasi kikubwa na zile za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Aidha, amehoji mpango wa kimkakati wa Serikali kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa kabisa katika Mkoa wa Kigoma.
Akijibu swali hilo la nyongeza, Naibu Waziri wa Afya amesema ugonjwa wa homa ya ini una chanjo kwa watoto na watu wazima, na kuwataka wananchi ambao hawajapata chanjo kujitokeza kuchanjwa ili kujikinga dhidi ya maambukizi.
Amesema Serikali imeanzisha huduma za matibabu ya Homa ya Ini katika hospitali za rufaa na hospitali za kanda, hivyo kuwawezesha Watanzania kupata tiba ndani ya nchi bila gharama kubwa.
Amesema Serikali itaendelea kufanya usimamizi shirikishi katika mikoa iliyoathirika zaidi ikiwemo Rukwa, Katavi, Simiyu, Kigoma na Songwe ili kudhibiti maambukizi.
Akihitimisha majibu yake, Naibu Waziri ametoa rai kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kupima afya zao mapema, akisisitiza kuwa upimaji na chanjo ni nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya ini.