TANESCO YAWEKA WAZI TARATIBU ZA UPIMAJI NA MAUNGANISHO YA UMEME RUVUMA.

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma, Allen Njiro, amesema kuwa wananchi hawatakiwi kulipa fedha zozote kwa maafisa wanaofanya upimaji wa umbali wa kufikisha huduma ya umeme, kwani kazi hiyo ni sehemu ya majukumu ya watumishi wanaolipwa na serikali.

Njiro ameyasema hayo leo Januari 29, 2026, wakati akizungumza na wakazi wa Kituro na Mpandangindo wilayani Songea mkoani Ruvuma, katika mwendelezo wa ziara yake ya  utoaji elimu kwa wateja wa TANESCO inayolenga kuwawezesha wananchi kuelewa taratibu sahihi za kuomba na kuunganishiwa umeme.

Ameeleza kuwa upimaji wa eneo au uchunguzi wa awali wa umbali wa kufikisha umeme hufanyika bure kabisa, na kwamba wananchi wanapaswa kufahamu kuwa hakuna mtu anayepaswa kudai au kupokea malipo yoyote kwa kazi hiyo, kwani ni jukumu la moja kwa moja la TANESCO.

Aidha, Njiro amesema kuwa maombi ya kuunganishiwa umeme hufanyika bila malipo, isipokuwa malipo halali ya Shilingi 27,000 kwa vijijini, ambayo hulipwa baada ya kukamilika kwa taratibu zote, kupitia namba ya kumbukumbu ya malipo (Control Number), kama inavyoelekezwa na TANESCO.

Ameongeza kuwa ili kuomba huduma ya umeme, mwombaji anatakiwa kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA), na maombi yanaweza kufanyika kwa njia tatu, ambazo ni kupitia simu janja kwa kutumia programu ya NikoNekti, simu ya kawaida maarufu kitochi, au kwa kufika moja kwa moja katika ofisi za TANESCO zilizo karibu na mteja.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya ufungaji wa nyaya ndani ya nyumba, Njiro amesema kuwa mteja ana uhuru wa kumtafuta fundi yeyote kwa ajili ya kufunga mifumo ya nyaya, baada ya hapo, mteja anatakiwa kumtafuta mkandarasi aliyesajiliwa na EWURA kwa ajili ya kukagua kazi hiyo na kuandaa mchoro utakaowasilishwa TANESCO.

Amesisitiza kuwa malipo ya mkandarasi huyo ni makubaliano binafsi kati ya mteja na mkandarasi husika, na TANESCO haihusiki kwa namna yoyote Ile kwani haina jukumu la kumpangia bei Mkandarasi.

Elimu inayotolewa na TANESCO Ruvuma, inalenga kuongeza uelewa kwa wananchi ili waweze kufuata taratibu sahihi za kuomba umeme, kuepuka mkanganyiko usio wa lazima, na kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa uwazi, usalama na kwa kufuata miongozo iliyopo.